In Summary
  • Natamani mbegu hii isambae maeneo yote nchini, kutokana na ukweli katika siku za hivi karibuni, tumeanza kushuhudia matendo yanayoashiria ubaguzi wa kiitikadi jambo ambalo ni la hatari sana.

Jumamosi iliyopita yalifanyika maziko ya Diwani wa Kata ya Mawenzi mjini Moshi (Chadema), Hawa Mushi yaliyohudhuriwa na viongozi wa Serikali, wanasiasa na wananchi kwa umoja wao na udugu wao.

Natamani mbegu hii isambae maeneo yote nchini, kutokana na ukweli katika siku za hivi karibuni, tumeanza kushuhudia matendo yanayoashiria ubaguzi wa kiitikadi jambo ambalo ni la hatari sana.

Ipo mifano mingi ya aina hii hapa nchini na hii si kwa Tanzania Bara tu, hata Zanzibar, ambako hata kutambulishwa tu kwa viongozi mnaotofautiana nao kiitikadi inaonekana ni nongwa.

Sote tulisikia na haijawahi kukanushwa, kwamba baadhi ya wabunge wa CCM waliotaka kwenda kumsalimia gerezani, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema walipigwa mkwara.

Tulishuhudia namna viongozi wa Chadema na baadhi ya viongozi wa dini katika msiba wa wanafunzi 32 wa shule ya Lucky Vincent walivyopatwa na misukosuko inayoashiria ubaguzi wa kiitikadi.

Kumekuwa na sintofahamu kuhusiana na matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu anayetibiwa nje ya nchi ambayo yalipaswa kugharamiwa na Bunge.

Mbegu hii inayooteshwa katika taifa letu ni mbaya sana kwani kuna uadui unaoasisiwa baina ya viongozi na wafuasi wa vyama vya upinzani, na kufanya siasa hapa Tanzania kuwa ni uadui mkubwa.

Leo hii Zanzibar, kuna mgawanyiko mkubwa kati ya viongozi, wanachama na wafuasi wa chama cha wananchi (CUF) kwa upande mmoja, na wale wa CCM kwa upande wa pili. Watu wananuniana.

Katika baadhi ya misiba na shughuli za kiserikali, tumeshuhudia hata suala la kuwatambulisha baadhi ya viongozi fulani wa kisiasa kunakuwa na figisufigisu nyingi.

Baba wa taifa, Mwalimu Nyerere aliwahi kusema dhambi ya ubaguzi kwa watu wa taifa moja ni mbaya sana na haufi, sawa ni kula nyama ya mtu.

Nimetangulia kurejea msiba wa Diwani Hawa, kwa sababu ni msiba ulioonyesha utanzania, utu na upendo wetu, ambapo kila kiongozi awe wa chama tawala au upinzani, alitambuliwa na kupewa heshima yake.

Ni msiba uliohudhuriwa na viongozi wa kisiasa na kiserikali, akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira na hakika upendo ule ulioonyesha katika msiba huo unapaswa kuenziwa.

Wabunge 10 akiwamo Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Steven Ngonyani, aliyekuwa mgombea ubunge Moshi mjini 2015 kwa tiketi ya CCM, Davis Mosha na makada kibao wa CCM walihudhuria.

Mwenyekiti wa CCM Moshi mjini, Alhaji Omary Shamba alipata fursa ya kutoa salamu za rambirambi kwa niaba ya chama. Huu ndio undugu na mshikamano aliotuachia Nyerere.

Baba wa Taifa aliwahi kusema katika hotuba zake ambazo zinaishi hadi leo kuwa “kutafuta uongozi wa kutumia dini au ukabila unagawa watu. Kazi ya kiongozi ni kujenga watu wawe kitu kimoja”.

Watanzania tunapaswa kukataa kupandikiziwa mbegu zozote za chuki ya ukabila, itikadi au ukanda yenye lengo la kutugawa Watanzania kwani hilo ni bomu na likilipuka madhara ni makubwa.

Tuhubiri amani, upendo na mshikamano kutoka moyoni na si usoni tu na tufanye hivyo tukitambua kuwa kuna maisha nje ya siasa.

Nikimnukuu baba wa taifa alisema dhambi ya ubaguzi haiishi inaendelea tu. Leo utabagua kwa kusema sisi Wazanzibari hawa Watanganyika, kesho utasema sisi Wapemba na wale Waunguja.

Tusipodhibiti ubaguzi wa kiitikadi katika misiba na baadhi ya shughuli za kiserikali, tutaenda mbele zaidi na kuanza kubaguana katika shughuli za kijamii kama utoaji wa huduma kwa wananchi.

Tutumie mfano ulioonyeshwa katika msiba wa Hawa, kurejesha upendo, undugu na mshikamano wetu kama taifa na tukariri maneno kuwa Tanzania kwanza, siasa baadaye.