Ijumaa ya Desemba 28, 2018, Rais John Maguful alifanya uamuzi ninaoweza kusema ni mgumu wa kurejesha kikotoo cha zamani cha malipo ya mkupuo kwa mtumishi anapostaafu kazi.

Uamuzi huu ulikuja baada ya kukutana na viongozi wa vyama vya wafanyakazi ikulu Jijini Dar es Salaam, ambapo kila kiongozi aliyepata fursa alipinga vikali kikokotoo kipya cha asilimia 25 kwa 75.

Uamuzi wa Rais kurejesha utaratibu wa zamani kwa kila mfuko katika kipindi cha mpito hadi 2023 kimerejesha nyuso za furaha kwa wafanyakazi na kurejesha ari ya kufanya kazi iliyoanza kupotea.

Rais alisema haileti maana kwamba mtu amefanya kazi kwa uaminifu mkubwa, lakini anapostaafu anaambiwa atapewa asilimia 25 ya mafao yake na nyingine atalipwa kidogokidogo hadi atakapokufa.

“Hata waziri hapa (akimlenga Jenister Mhagama) akimaliza ubunge wake ukimwambia utampa asilimia 25 kisha nyingine utampa kidogokidogo hawezi kukubali,” alisema Rais Magufuli.

Naungana na Rais kuwa mantiki haiingii akilini na binafsi nilijiuliza kwamba hawa wasomi wetu waliotunga kanuni hii kandamizi wanafikiri kwa kutumia ubongo gani.

Lakini mara baada ya kuchukua uamuzi huo, kumeibuka kejeli katika mitandao ya kijamii, wakiweka vikatuni kuwa ili upande chati kisiasa unatakiwa kutengeneza tatizo halafu ulitatue.

Hakuna ubishi kuwa sheria ya kuunganisha mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini ilitungwa na Bunge na baadaye Rais kuiidhinisha, lakini kanuni, ambazo ndio kiini cha tatizo, hazikutungwa na Rais.

Utaratibu ni kwamba Rais akishasaini sheria kuanza kutumika, anayetunga kanuni na kuzichapisha gazeti la Serikali ni waziri mwenye dhamana na katika hili waziri mwenye dhamana ni Jenister.

Kuna utamaduni unaanza kujengeka hapa nchini wa kumkosoa tu Rais kwa minajili ya kukosoa, hata afanye jambo gani jema kwa maslahi ya Watanzania. Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.

Mimi nilitarajia tungewashikia bango wanasiasa na hata baadhi ya wanahabari, ambao walihama kutoka kusimama katika maslahi ya umma, wao wakajikita katika kuimba wimbo wa “kikokotoo ni bora”.

Namshukuru Rais kwa kuwaumbua wanasiasa wa aina hii na wengine ni wa chama chake. Hata baada ya Rais kusimama upande wa wafanyakazi, nao watu walewale wamerudi kushangilia. Huu ni unafiki.

Sielewi wanasiasa wa aina hii, tena mmoja yuko ndani ya Baraza la Mawaziri, ambao walituma ujumbe kupitia Twitter wakiwadhihaki wafanyakazi wanaopinga kikikotoo, wanajisikiaje huko waliko.

Kama mwanasiasa huwezi kusimama na matatizo ya kundi kubwa kama la wafanyakazi, unataka usimame na nani? Nitumie fursa hii kuwashauri wabunge wengi wa CCM, wasome alama za nyakati.

Alilolifanya Rais limetukumbusha pale mlipopitisha sheria mbovu ya madini ya mwaka 2010 kwa mbwembwe licha ya wabunge wenzenu wa upinzani kuikosoa vikali, Rais Magufuli aliporekebisha makosa yenu na vilevile mkashangilia.