In Summary
  • Wakati mipango hiyo ikiendelea, tayari tunaarifiwa kuwa huenda umaarufu wa tamasha la utamaduni la kabila la wasukuma liitwalo ‘Bulabo’ ukapungua kutokana na kutoonekana kwa wanyama wakali aina ya fisi katika tamasha hilo kwa miaka ya hivi karibuni, na badala yake wasukuma wanacheza ngoma kwa kutumia ngozi tu za wanyama hao.

Serikali imeahidi kufanya maboresho katika Kituo cha Makumbusho ya Utamaduni wa Wasukuma Bujora kilichopo Kisesa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza ili kukuza na kuendeleza utamaduni wa kabila hilo.

Wakati mipango hiyo ikiendelea, tayari tunaarifiwa kuwa huenda umaarufu wa tamasha la utamaduni la kabila la wasukuma liitwalo ‘Bulabo’ ukapungua kutokana na kutoonekana kwa wanyama wakali aina ya fisi katika tamasha hilo kwa miaka ya hivi karibuni, na badala yake wasukuma wanacheza ngoma kwa kutumia ngozi tu za wanyama hao.

Bulabo hufanyika Juni kila mwaka kusherekea sikukuu za mavuno, tamasha hili limekuwa maarufu nchini Tanzania kutokana na kabila hilo kutumia wanyama kama chatu na fisi katika kucheza ngoma, jambo ambalo huwaduwaza watu wengi.

Lakini kwa sasa na miaka ijayo huenda fisi wasionekane kwenye tamasha hilo kwa sababu ya kukosa vibali.

Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Makubusho ya Bujora, Padri Fabian Mhoja anasema si kwamba vibali havikuwepo kabisa, isipokuwa wakurugenzi wawili wa wanyamapori waliopita walikuwa wanashirikiana nao kwa ukaribu na kutoa vibali vya kufuga wanyama hao, lakini walifariki dunia kwa nyakati tofauti.

Na kwa sababu hiyo au nyingine zinazotokana na mabadiliko ya sera kwenye utoaji wa vibali vya maliasili na wanyamapori, vibali vipya havikuweza kupatikana.

Mhoja anasema zamani vibali vilikuwepo na viliwaruhusu kufuga fisi, nyani na nyoka ili kuwatumia katika maonyesho hayo na kuvuta umati wa watu. Aliomba serikali kutoa ushirikiano zaidi ili kufanya maboresho ya miundombinu mbalimbali kituoni hapo.

Kutokana na changamoto hiyo, baadhi ya wapenzi wa tamasha hilo wanasema kwa sasa halitakuwa na maana tena kwani zamani walikuwa wanawaona wanyama hao.

Mkazi wa Kijiji cha Magu wilayani Magu, Shija Mpelwa anasema wakiwepo wanyama kama hao huvuta watazamaji wengi badala ya kuwaona kwenye runinga pekee.

Wakati malalamiko hayo yakiwasilishwa, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella anasema Serikali itaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha inatunza kituo cha Bujora ambacho ni kituo pekee cha kurithi utamaduni wa kabila la wasukuma nchini.

Kwa mujibu wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe, kitu kinachofanywa na kabila hilo ni cha muhimu kwani kikilindwa na kutunzwa kitasaidia katika vizazi vijavyo na kuvuta watalii.

Anasema kituo hicho kikiboreshwa kitasaidia kutunza kumbukumbu si tu za kabila la wasukuma bali Tanzania kwa ujumla.

Kwa hiyo, kuna umuhimu kwa Serikali kurudisha vitu hivyo shuleni, kwani mbali ya kuwajenga watoto ufahamu lakini pia vinaimarisha afya yao, kimwili na kiakili.

Mpango huo pia utasaidia kupata watu wa kuuhifadhi utamaduni wetu siku zijazo katika hali ya kisasa zaidi. Lakini, jamii pia iondoe mtazamo potofu kwamba ngoma hizo ni za watu wenye mawazo ya kizamani, wazee, wasioenda shule, washamba na kadhalika.

Tulinde na kuhifadhi tamaduni zetu kwa vizazi vya sasa na vijavyo tukiamini kuwa Taifa lisilokuwa na utamaduni wake linakuwa limekufa.