In Summary

Unapowazungumzia manaibu waziri wachapa kazi bila shaka utamuacha Subira Mgalu. Huyu ni Naibu Waziri wa Nishati anayechanja mbuga kila uchao kuhakikisha anawasha umeme katika kila kijiji. Katika mahojiano na gazeti hili anaeleza mambo mbalimbali ikiwa mikakati yake

Mwandishi: Subira Mgalu unagawa vipi muda wako wa kazi na familia?

Mgalu: (Kicheko). Kwanza ninachoamini ukizaliwa mwanamke ni zaidi ya kuwa na mikono miwili na miguu miwili. Ninaweza kujigawa bila shida hata baada ya Serikali kuhamia Dodoma. Nashukuru familia yangu inatambua hilo akiwamo mume wangu na watoto wangu watatu ambao wanasoma, wananielewa na ninapokuwa nyumbani najitahidi kutimiza majukumu yangu kama mama.

Mwandishi: Mbali ya unaibu waziri ambao umekufanya uwe kazi nyingi, unapata nafasi ya kufanya siasa?

Mgalu: Nikiwa natimiza majukumu ya unaibu waziri ninakuwa nafanya siasa pia kwa sababu nafasi hiyo anapewa mbunge.

Ila ninapokuwa sina majukumu ya unaibu waziri huwa nahakikisha niko jimboni kwangu ambapo kwa mujibu wa sheria za nchi ninatumikia mkoa mzima wa Pwani.

Hivyo nazungukia wananchi wa eneo hilo, nasikiliza kero zao ninapoweza kutatua nafanya hivyo, ninaposhindwa nawasilisha kwenye ngazi husika.

Mwandishi: Umeingia ubunge wa viti maalumu kipindi cha pili, Je, una mpango wa kugomba jimbo kwenye uchaguzi ujao?

Mgalu: Kwa sasa sina jibu la moja kwa moja kama nitagombea au la. Bado najifunza zaidi nasoma wengine wanafanya nini. Mwaka 2020 bado mbali sijafika mtoni inakuwa ngumu kuzungumzia kuvuka mto, hivyo nitakapofika mtoni ndiyo nitajua kama nitavuka mto.

Mwandishi: Unaonaje siasa za majimboni, unadhani ni rahisi?

Mgalu: Siasa za majimboni zinafanyika na zipo imara sana, licha ya wabunge kuwa na shughuli nyingi lakini bado wanafika kwa wananchi wao na kutatua kero zao.

Hali hiyo pia inafanya iwe ngumu kukurupuka kuwania jimbo kwa sababu upinzani umekuwa mkali kila aliyepo kwenye jimbo anafanya kazi aliyotumwa na wananchi wake.

Mwandishi: Umewahi kujaribu kugombea jimbo hapo kabla?

Mgalu: Siyo kujaribu, niligombea kabisa mwaka 2015 katika Jimbo la Chalinze baada ya Jakaya Kikwete aliyekuwa mbunge kuteuliwa kuwania urais na mimi nikajitosa kuwania nafasi hiyo.

Ushindani ulikuwa mkali kulikuwa na wagombea 17 kati yao wanaume walikuwa 16 mwanamke nilikuwa peke yangu na sikufanya kampeni ya maana lakini nilishika nafasi ya nne, hivyo siasa za majimboni nazijua kabla sijateuliwa kuwa mbunge wa viti maalumu.

Mwandishi: Unadhani kuwa mwanamke peke yako ndiyo kilikuangusha?

Mgalu: Naamini katika maamuzi ya wengi. Nilishindwa na nilikubali matokeo. Nimerudi kujipanga kwa ajili ya nyakati zijazo.

Natambua siku za nyuma jamii ilikuwa inapata taabu kumuamini mwanamke kumpa jimbo au nafasi ya juu ya uongozi kwa sababu moja ama nyingine ikiwamo za kiutamaduni kutoka vizazi na vizazi. Tabia hiyo kwa sasa inabadilika na wanawake waliopata nafasi wanachapa kazi na wanaanza kuaminika.

Napenda kutumia nafasi hii pia kuondoa dhana ya wanawake wanaweza hadi wawezeshwe, ninachofahamu anayeweza anaweza na hata asipowezeshwa anajitahidi hadi wanaowezesha wamuone na kumuwezesha. Maana wapo waliowezeshwa na wakashindwa.

Mwandishi: mkoa wa Pwani ambao unauwakilisha bungeni upo nyuma kielimu, mikakati yako ni ipi kuhakikisha unainuka?

Mgalu: Nakubaliana nawe elimu mkoa wa Pwani inahitaji msukumo wa ziada, licha ya matokeo ya mwaka jana na mwaka huu kuonyesha tumepanda lakini ninahisi ni kwa sababu ya shule nyingi binafsi. Nataka niungane na watendaji wenzangu ikiwamo wakuu wa wilaya kuhakikisha elimu inapanda kwa mkoa mzima tukiangalia zaidi shule za kata.

Pia kuunga mkono kile kinachofanywa na mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo kutokomeza ziro ifanyike kwa wilaya zote na nitapita kwenye kata mbalimbali kuzungumza na wazazi kwa sababu ni bila kuwashirikisha wao ni ngumu kupata matokeo chanya.

Mwandishi: Umeonekana ukiwasha umeme kwenye vijiji mbalimbali. Hadi sasa umevifikia vingapi?

Mgalu: Sikumbuki vijiji vingapi ila kwa mikoa 26 ya Tanzania Bara nimefika mikoa 19 au 20. Lengo la sasa si kusambaza umeme bali ni kuona umeme huo unaleta mabadiliko kwa jamii.