In Summary
  • Shinikizo linaweza kuwa la kihisia au hata kiuhalisia. Kihisia ni pale ndugu au wazazi wanapokushawishi mara kwa mara kuoa sababu umri wako unaonekana kwenda na wako wazazi wengine husisitiza kuwa wanataka wajukuu (utasikia mzazi anasema unataka nife sijawaona wajukuu zangu?).

Makala hii inaendelea kutoka wiki iliyopita. Leo nitaanza na kuzungumzia sababu ya kuolewa au kuoa kwa sababu ya shinikizo kutoka kwa wazazi, ndugu au marafiki.

Shinikizo linaweza kuwa la kihisia au hata kiuhalisia. Kihisia ni pale ndugu au wazazi wanapokushawishi mara kwa mara kuoa sababu umri wako unaonekana kwenda na wako wazazi wengine husisitiza kuwa wanataka wajukuu (utasikia mzazi anasema unataka nife sijawaona wajukuu zangu?).

Hata kama huhisi kulazimishwa lakini kwa kule kurudia rudia kwa kukumbushwa kila siku kunaweka shinikizo ndani yako, kunaathiri hisia zako na kuweza kukupelekea kuingia katika ndoa isiyopangiliwa. Shinikizo la kimwili au kihalisia ni pale wazazi wanapolazimisha watoto wao kuoa au kuolewa na watu fulani kwa sababu tu ni marafiki zao au kwa sababu ya kulinda utajiri na matarajio yoyote binafsi.

Ndoa nyingi za aina hii zimekuwa kero na dimbwi la maumivu na machozi, baada ya muda kidogo mnajikuta mali mnazo, wazazi wenu wanapatana na kupendana, lakini nyie kama wapenzi ni maadui wakubwa. Jiulizeni mnaingia kwenye mahusiano kwa furaha yenu au ya wazazi wenu?

Kuamua kuoa au kuolewa ili kupata uhuru.

Hii hutokea sana kwa wale waliozoea kubanwa sana na wazazi katika kila wafanyacho hususani katika maamuzi. Wengine huzikimbia familia zao maana hazieleweki, hazina mpangilio na hivyo kutamani kutoka ili wakaanzishe zakwao wenyewe. Kinadada na kinakaka wanachoka kuamuliwa na kuwekewa masharti ya kuvaa, kula, kufanya mambo, kutoka na kurudi kwa muda kwahiyo wanadhani ndoa ndio itawachomoa kifungoni hapo. Ninaushahidi wakutosha wa baadhi ya ambao walikimbilia katika mahusiano ili kuwa huru na kwa bahati mbaya waliyoyakuta huko kwenye mahusiano yaliwafanya watamani hali waliyoiacha nyumbani kwao ingawa kwa bahati mbaya wakati huo ‘it was too late’.

Matokeo ya kuingia katika ndoa kwa sababu mbovu

Lengo la kuingia kwenye ndoa, liwe zuri au liwe baya ndilo litakalotegemeza aina ya maisha yenu katika ndoa hiyo kuwa ya furaha au ya machungu. Baada tu ya kuoana na huyo mtu wako kwa sababu zisizo za msingi, siku, miezi au miaka siyo mingi utaanza kuchoka na kutamani kutoka nje ya hiyo ndoa kwa maana baina yenu hakuna muungano wa ndani baina ya wanandoa wawili. Na mara nyingi hali hii hupelekea msongo wa mawazo , mfadhaiko wa moyo na kukosa furaha ndani ya ndoa.

Matokeo ya hali hii kumfanya mwanandoa mmoja au wote wawili kuanza kutafuta kutoshelezwa na kuliwazwa nje ya ndoa na hapa vinazaliwa vitu vingine kama uzinzi, kutengana, talaka au magomvi na mifarakano isiyoisha.

Kwa nini ndoa na uhusiano mwingi hushindwa?

Kwa sababu ya kukosa maarifa.

Wanandoa wengi hawajui nini wafanye, nini waelewe ili kufanya ndoa yao zifanikiwe. Thamani ya ndoa na jinsi ndoa inavyochukuliwa sikuhizi ni tofauti sana na nyakati za wazazi wetu, na hii imewafanya wengine kujikuta wako wenye ndoa kwasababu mbovu na hivyo ndoa nyingi kuvunjika au kuyumba baada ya muda mfupi tu.

Vitu kama kudhamiria, heshima na uaminifu sio vya maana tena siku hizi, sababu watu wanaogopa kuonekana wa zamani na washamba.

Mtazamo wa ulimwengu juu ya ndoa umeharibiwa na magazeti, luninga na vitabu mbalimbali. Siku hizi kuishi bila ndoa ni kitu cha kawaida, kuwa na mpenzi nje ya ndoa sio kitu cha ajabu tena, mapenzi nje ya ndoa sio ya kushangaza hata kidogo. Kinyume chake ukionekana kuyashangaa haya, jamii itakushangaa wewe kwa jinsi ulivyo nyuma ya wakati.

Mambo yamebadilika sana, zamani binti akikutwa bikira wakati anaolewa ilikuwa sifa kwake na familia nzima, siku hizi binti akikutwa bikira atachekwa, na watu kumshangaa wakihisi ana matatizo fulani.

Hali kadhalika kwa kijana wa kiume aliyejitunza. Kwa bahati mbaya sana tunaishi katika jamii ya ajabu isiyoamini katika kujitoa kwa kweli na kudhamiria katika mahusiano.

Jamii isiyoamini katika uaminifu, na ndiyo maana magomvi mengi hutokea pale simu ya mmoja inapoguswa. Kuwindana na kuchunguzana kumekuwa kawaida, maadili sio jambo la kuzingatiwa tena. Wanandoa wengi ni wale wenye majeraha ya moyoni na walio umizwa, kwa hiyo hutoka nje ya ndoa zao wakitafuta mwingine aliyeumizwa kama wao ili waliwazane.

USULI

Sababu za msingi zinazoweza kukufanya uingie katika ndoa na usijute

• Ndoa ni mpango wa Mungu kwa mwanamke na mwanaume kuwa pamoja

• Ni nafasi ya wawili hawa kuonyeshana mapenzi yao

• Ni nafasi ya kutimiziana mahitaji ya mwili kupitia tendo la ndoa kwa muda sahihi, na kwa mtu sahihi, maadili yakizingatiwa.

• Hamu na kiu ya kutengeneza familia yenu.

• Kutimiza kiu ya kuwa pamoja kwa umoja

• Nia au kusudi la kushiriki vyote kwa pamoja . Kufanya kutenda kwa pamoja ili kutimiza mahitaji yetu wote.

• Nafasi ya kutumia kwa manufaa kila uwezo na vipawa mlivyokuwanavyo kwa maendeleo ya familia.

• Kuchangiana katika makuzi yenu ya ujumla, makuzi ya kimwili, kiroho, kihisia