In Summary
  • Jambo la kusikitisha zaidi ni watu wanaojipambanua kuwa watetezi wa haki na uhuru wa mawazo ndio waliokuwa mstari wa mbele kunitusi na kunikejeli badala ya kunipinga kwa hoja. Sikusema katika makala ile kuwa ni lazima mtu akubaliane na mimi kama mimi nisivyolazimishwa kukubaliana nao.

Mara ya mwisho nilipoandika makala ikielezea mtazamo wangu kuhusu Rais Magufuli kuwa anashaurika, niliporomoshewa matusi katika mitandao ya kijamii eti kwa nini niseme hivyo. Jambo la kusikitisha zaidi ni watu wanaojipambanua kuwa watetezi wa haki na uhuru wa mawazo ndio waliokuwa mstari wa mbele kunitusi na kunikejeli badala ya kunipinga kwa hoja. Sikusema katika makala ile kuwa ni lazima mtu akubaliane na mimi kama mimi nisivyolazimishwa kukubaliana nao. Nilijenga ushawishi wangu kwa hoja, nikiamini kama ni kupingwa nitapingwa kwa hoja na si matusi. Haya yamepita na tugange yajayo.

Rais Magufuli karudi tena kwa kishindo baada ya kupokea ndege tuliyokuwa tumeaminishwa kuwa haipo kutokana na deni la mkandarasi wa barabara. Tuliambiwa hakuna mbadala zaidi ya kulipa na kuaminishwa haitakuwa rahisi kuipata kwani uwezo wa kulipa hatuna.

Tulisomeshwa vifungu vya sheria kutuonyesha itakavyokuwa vigumu kuafikiana na wadeni wetu na kurudishiwa ndege hiyo. Wapo tulioangalia nyuma na kukumbuka suala la makinikia na onyo tulilopewa na ndugu zetu wasomi kuwa tutaishia kulipa fidia kubwa kutokana na uamuzi huo wa kumwambia jirani kuwa asiniibie.

Ajabu mpaka sasa hatujaona hilo pigo la nguvu tulioahidiwa na Watanzania wenzetu kwa uthubutu wa Rais wetu wa kumwambia jirani imetosha kuniibia zaidi ya jirani kuwa mpole na kutafuta muafaka. Ndege imefika huku dua la kuku likishindwa kumpata mwewe kwa mara nyingine.

Rais na tanzanite

Rais Magufuli hivi karibuni amesema tanzanite ni yetu iweje jirani awe namba moja kwa uuzaji wake? Yaani hatujui tumeuza kiasi gani nje ya nchi wakati madini yakiwa yanapatikana Tanzania. Tunasubiri majirani waonyeshe takwimu za uuzaji wa tanzanite katika soko la dunia ndio turekebishe mahesabu yetu.

Rais Magufuli kwa kulitambua hili na akiwa mlinzi namba moja aliyekabidhiwa jukumu hilo na Watanzania, akasema imetosha. Kama kawaida yetu mara moja baadhi yetu tukabadili uelekeo na kuanza kumshambulia na kumkejeli kuwa hili halikutakiwa kufanyika maana tutawaumiza wachimbaji wadogowadogo wanaotegemea kuuza kwa matajiri moja kwa moja.

Tukasema huo ukuta hautamalizika na utumiaji mbaya wa pesa. Katika usiku mmoja tukasahau kilio chetu cha siku zote kuwa tunaibiwa na hatufaidiki na mali alizotujalia Mwenyezi Mungu. Rais Magufuli kama kawaida yake akagundua mtego uliopo na kuwaambia tanzanite itauzwa hapohapo Mererani.

Sijahakiki madhara ya uamuzi huu zaidi ya kujua kuwa kwa jirani usafirishaji wa tanzanite kwenda soko la dunia umepungua kama sio kuisha kabisa huku taarifa zikiionyesha mwenye tanzanite ameanza kuuza zaidi. Hesabu ya jirani ime-balance, hana machimbo ya tanzanite hawezi kuzalisha kuliko mwenye tanzanite.

Rais Mafufuli akaja na wazo la kujenga ukuta ili kulinda madini haya yanayopatikana nchi kwetu tu na pia kuhakikisha kodi inalipwa. Ukuta akawapa wanajeshi wetu kujenga huku baadhi yetu tukiwa hatuna uhakika kama kweli utakamilika. Umekamilikia! Tena kabla ya muda waliojipangia wanajeshi wetu.

Rais Magufuli amedhamiria kulinda mali zetu kwa faida yetu. Kama nilivyosema hapo juu, ni aibu kuwa hatukuwa hata tunajua tumechimba kiasi gani cha tanzanite mpaka Wahindi na jirani waseme wameuza kiasi gani ndio tu-balance mahesabu yetu. Ilikuwa ni mahesabu tu ya kiasi cha tanzanite kilichochimbwa na siyo kiasi cha pesa kilichopatikana maana hakikutuhusu.

Ilikuwa ni tanzanite ya Wahindi na jirani ambayo imehifadhiwa katika ardhi ya Tanzania. Tulipewa jukumu la kuihifadhi chini ya ardhi ya nchi yetu na siyo kufaidika nayo. Ilikuwa ni dhamana tu ya kuwa ndani ya nchi yetu na si vinginevyo. Hata mswahili aliyeigundua hakuwa anajulikana huko nje bali mjamaa fulani aliyedhulumu haki ya ugunduzi.

Tulipewa haki moja tu ya kuichimba na kuwapelekea Wahindi na jirani yetu kwa magendo kwa bei ya kutupa na wao kuiuza kwa bei nzuri sana na kutambulika kama wauzaji wa madini haya dunia.

Ujenzi wa ukuta

Rais Magufuli akaamua kujenga ukuta huo ili kuhakikisha madini yetu tunayauza wenyewe na kufaidika nayo huku kodi yetu ikilipwa ili kusaidia mambo mengine.

Kwangu mie ukuta ni ishara tu zaidi ya ngome ya matofali ili utukumbushe kuwa mali zetu lazima tufaidike nazo. Ni alama ya kuamusha uelewa wa Watanzania kuwa imetosha kufaidisha wageni au kikundi kidogo cha Watanzania kwa mali zetu zinazotakiwa kutunufaisha wote kwa sasa na vizazi vyetu vijavyo.

Ukuta wa Mererani unatakiwa uwe kielelezo cha dhuluma iliyodumu tangu mwaka 1967 wakati madini ya tanzanite yalipovumbuliwa na pia madini yote tuliyojaliwa hapa nchini lakini hatufaidiki nayo.

Ukuta wa Mererani hautakiwi uangalie kwa uimara wake bali kwa lengo lililokusudiwa na Rais Magufuli kuwa sasa madini yetu yawe yetu na kutufaidisha sisi. Hivyo ujumbe usitokane na uimara wa ukuta bali kujitambua kwa Watanzania kuwa imetosha kuibiwa mali zetu, kuwe na ukuta au usiwepo. Ukuta umemalizika na kuzinduliwa huku ukiacha ujumbe murua kuwa wizi wa mali zetu sasa mwisho kuwe na ukuta au usiwepo.

Kuibuka Mzee Ngoma

Pamoja na kuzindua ukuta wa Mererani, Rais Magufuli katukumbusha jambo lingine muhimu sana, tuthamini chetu. Mwaka 1967, Mzee Jumanne Mhero Ngoma alivumbua tanzanite na tukamsahau. Zikapigwa porojo huko nje kupitia wababe wa habari dunia kuwa mvumbuzi wa tanzanite ni mjamaa fulani na siyo mswahili mwenzetu. Dunia ikaamini kupitia nguvu za hawa wababe wa habari. Akasifiwa na kutajirika kupitia dhuluma aliyomfanyia Mzee Ngoma. Sasa historia imeandikwa kwa wavumbuzi wa vitu tulivyokuwa tunavijua kama milima, mito, na hata maziwa utadhani Tanzania haikuwa na watu.

Mzee Ngoma aligundua tanzanite na kusahaulika. Huyu ni Mtanzania aliyetuletea heshima na utajiri kwa uvumbuzi wake. Si ajabu wakoloni wangejua kuna tanzanite hapa Tanzania, labda wangemega kipande hicho na kukiita ni nchi fulani.

Mzee Ngoma siku yake imefika na Magufuli ametambua mchango wake katika madini haya. Rais Magufuli ametukumbusha kuwa wako akina Mzee Ngoma wengi tu hapa nchini ambao wameiletea sifa nchi hii na sasa hawajulikani au kusahaulika kabisa. Hawako katika vitabu vya historia wala makala za wababe wa habari dunia maana sio wazungu. Si ajabu kesho vijana wetu wasiwajue majenerali kama Mayunga, Walden, Musuguri, na wengine wengi ni akina nani katika historia ya nchi hii.

Wataendelea kukariri majina ya wazungu huku wakiwa hawana habari za hao Watanzania walioliletea sifa na heshima taifa hili. Uamuzi wa Rais Magufuli kumtunuku Mzee Ngoma ilikuwa pia ni kuwakumbusha Watanzania kuhakikisha kuwa historia haiwafuti na kuwatoa katika kumbukumbu zetu mashujaa walikoliletea sifa nchi hii katika nyanja mbalimbali kwa vile tu ni waswahili na hawawezi kuingia katika makala za wababe wa habari duniani.

Historia ya Tanzania imeongezewa vitu vitatu: Rais Magufuli, Ukuta wa Mererani, na Mzee Ngoma.