In Summary
  • Ni haki ya kila mmoja kumiliki ardhi. Kati na sheria nyingi za nchi zinatoa haki hiyo. Hakikisha unamiliki ardhi yako na kujiletea maendeleo kutoka na kipande utakachokuwa na mamlaka nacho.

Mwenye ardhi ndiye anayetunga sheria. Ardhi ni utajiri, dhamana, mali na urithi endelevu kati ya rasilimali muhimu za uchumi.
Huwezi kuzungumzia kilimo, makazi au nyumba bora kabla ya kujua zitakapojengwa. Ukigusia madini pia unaizungumzia ardhi yenye hayo madini. Maji safi na salama hayapatikani isipokuwa ardhini.
Zungumzia uchumi wa viwanda, lazima uitaje rasilimali adimu ya ardhi. Viwanda haviwezi kujengwa hewani na malighafi zake nyingi zinapatikana ardhini.
Utajiri wa mahali popote, pamoja na mambo mengine, unategemea namna ambavyo watu wanavyoweza kutumia ipasavyo ardhi yao.  
Sheria ya Ardhi ya mwaka 2002 inaitambua nafasi ya juu ya ardhi pamoja na vilivyomo ndani yake isipokuwa madini au mafuta.  
Kanuni za sheria hii zinatambua ardhi yote ya Tanzania ni mali ya umma chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye ni mdhamini kwa niaba ya wananchi kuhakikisha kuwa haki zilizopo au umiliki ambao umekuwepo tangu awali unatambuliwa na kulindwa na sheria.
Rais anajukumu la kuhakikisha kuna mfumo makini na ulio wazi wa usimamizi wa ardhi, kuwawezesha wananchi wote kushiriki kufanya uamuzi wa mambo yahusuyo ardhi.
Kuna sheria mbalimbali zinazozungumzia ardhi kwa namna moja au nyingine kama vile ya ardhi ya vijiji, ya mahakama za utatuzi wa migogoro ya ardhi, ya upangaji miji.
Pamoja na sheria hizi, bado Katiba ndiyo sheria mama ya ambayo inatoa haki ya msingi ya mtu kumiliki mali ikiwa ni pamoja na ardhi.  Jambo la kuzingatia katika sheria hizi ni kwamba, kila sheria inaeleza juu ya haki na wajibu ulio nao ambao unapaswa kuupata au kutimiza kabla hujapata haki zako.
Kwa ujumla, kila sheria ipo kwa ajili ya kutetea na kulinda haki zako. Unachopaswa kufahamu ni kujua jinsi ya kuitumia kila moja mahali panapostahili ili kufanikiwa kupata haki yako na jinsi ya kuisimamia na kuifuatilia.
Ufahamu utakaokuwa nao kuhusu sheria hizi utakufanya uchukue hatua thabiti zenye mwelekeo sahihi. Sheria inampa haki kila raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumiliki ardhi mahali popote atakapo.
Ukimilikishwa ardhi sio hisani bali ni haki yako ya kisheria na kikatiba. Hivyo kila raia wa Tanzania anapaswa kuamka na kuona ni jinsi gani ataweza kumiliki ardhi kulingana na uwezo wake.
Mwenyezi Mungu ameipendelea Tanzania na kuipa ardhi tele ambayo kila raia wa kizazi cha sasa na kijacho ana uwezo wa kuimiliki. Tofauti na nchi nyingine ambazo ardhi imeisha na hakuna tena fursa ya kupata kipande chochte zaidi ya kununua kutoka kwa yeyote aliye tayari kufanya hivyo.
Sheria imeigawa ardhi katika makundi makuu matatu ambayo ni ardhi ya akiba, ardhi ya kijiji na ardhi ya jumla. Ardhi ya akiba hutumika kwa shughuli za umma kama vile mbuga za wanyama, mapori ya akiba na maeneo yaliyotengwa kwa shughuli za kiserikali au kijamii.
Ardhi ya kijiji huwekwa chini ya Serikali ya Kijiji wakati ile ya jumla ipo chini ya halmashauri.
Sheria pia imeweka bayana kuwa Tanzania mtu hapewi haki ya kudumu ya umiliki wa ardhi bali upangaji kwa muda maalum au leseni ya makazi. Ndio maana hati zinazotolewa si za kudumu bali za kipindi cha miaka 33, 66 au 99 ingawa unaweza kuomba tena muda ukiisha.
Pamoja na kupatiwa muda huo wa kuitumia ardhi hiyo bado Rais anayo mamlaka ya kutengua au kufuta hati ya mtu yeyote kwa masilahi ya umma au utakiuka masharti ya umiliki.