In Summary
  • Unapotaja filisofia kuwa mtindo wa sanaa, unakuwa unagusa uwezo wa medulla na hisia za binadamu husika katika sekta anayoitumikia. Kwenye michezo kuna watu waliofanikiwa kutokana na sanaa yao ndani ya uwanja na nje ya uwanja pia.

Maisha ni sanaa na sanaa ni maisha. Kila unalofanya maishani ndio haswa sanaa yako mwenyewe na ni kitu ambacho kinaamua watu wakuchukulie vipi. Biashara ni sanaa, muziki ni sanaa, kusali ni sanaa, na muktadha unaoamua kuendesha maisha yako pia ni sanaa. Sanaa ni filosofia inayoamua uishi kwa mtindo gani kwenye jamii na mafanikio yako kwa ujumla.

Unapotaja filisofia kuwa mtindo wa sanaa, unakuwa unagusa uwezo wa medulla na hisia za binadamu husika katika sekta anayoitumikia. Kwenye michezo kuna watu waliofanikiwa kutokana na sanaa yao ndani ya uwanja na nje ya uwanja pia.

Cristiano Ronaldo ni mwanaume anayefanikiwa ndani ya uwanja kutokana na sanaa yake ya uchezaji lakini pia ni mchezaji anayeingiza fedha nyingi zaidi kutokana na sanaa yake ya kimaisha nje ya uwanja. Nenomuhimu hapa ni sanaa.

Mourinho ni kocha ambaye sanaa yake ilirudisha watu miaka mingi nyuma wakati Italia inaishi katika sanaa ya soka iliyoitwa catenaccio, yeye akapewa kupaki basi kutokana na tofauti ndogo ya kimtindo na ubunifu kati yake na waasisi wa Catenaccio.

Mourinho aliipatia kwelikweli na ilichukua muda wapinzani kufahamu namna ya kucheza naye, bahati nzuri sanaa yake nje ya uwanja ilimfanya kutambulika kama mjivuni na aliyekuwa na maringo kupita kiasi. Hizi sanaa mbili ndizo hasa zilizomtambulisha Mourinho. Ni muhimu kuwa na sanaa ya kazi na sanaa ya maisha.

Tanzania aliwahi kuishi Haruna Moshi, bahati mbaya pamoja na sanaa yake ndani ya uwanja ambayo ilikuwa ni furaha ya kila aliyemtazama, sanaa ya nje ya uwanja ilimwangusha siku zote. Hii ni sanaa ambayo ndiyo uhakikisha biashara yako wewe kama chapa imeimarika na inakuingizia kipato cha ziada na cha muhimu. Ni sanaa muhimu zaidi.

Sanaa ya nje ya kazi inabidi iwe inaunga mkono ama kutoa “sapoti” kwenye sanaa yako ya kazi ili uweze kueleweka kwenye jamii na uweze kuwa imara katika kuwasilisha jambo lako, wengine wanaweza kwenda mbali na kukueleza kuwa uwe na nguvu madhubuti.

Tanzania ni nchi ya wapenda michezo hususani soka. Wapo binadamu Tanzania ambao chakula chao cha kwanza kinaenda kwanza kwenye mboni zao kabla ya matumbo yao.

Kwa tafsiri ya moja kwa moja ni kuwa wapo binadamu wengi bila kujali makabila yao ambao Yanga na Simba zinawauma zaidi kuliko njaa ya siku tatu. Ni wazi kuwa hizi klabu zimeshika hisia za watu wengi kuliko hata baadhi ya nyumba za ibada.

Ni ndani ya taasisi hizi ambapo kuna John Bocco, Shizya Kichuya, Shomari Kapombe, Aishi Manula, Kelvin Yondani, Ibrahim Ajib na wengine wengi ambao jukwaani wanakuwa na wanunuzi wa sanaa zao ndani ya uwanja. Watanzania wanaofunga safari ama kuketi kwenye “televisheni” ili watizame namna gani furaha za mioyo yao zitatokana na kazi ya miguu ya wachezaji hawa.

Lakini bahati mbaya ni kuwa jungu kuu la wachezaji hawa limeshafishwa likamalizika yaani ukoko umekosekana kabisa. Hakuna namna unaweza kukuta sanaa yao ikitambulika nje ya uwanja na hakuna shabiki ambaye amewahi kukutana na namna ambayo inaweza kumfanya kuunga mkono juhudi za kibiashara za wachezaji hawa.

Sanaa ya biashara kwa wachezaji mara nyingi inaanza na wasimamizi wa wachezaji hawa lakini si ajabu kukawa na wasimamizi wa wachezaji kipindi cha mishahara pekee. Dunia imehama na inakimbia kwa kasi kuliko kawaida. Sekunde hazijabadili kasi yake lakini akili zinakimbia kuliko kasi ya dunia, na ndio namna mpya ya kuhesabu muda.

Maendeleo ya michezo yanatokana na kuunganisha sanaa ya ndani na nje mwa uwanja. Inawezekana vilabu vyetu vimeshindwa kufanya biashara ya bidhaa zao ikiwemo haki ya matumizi ya picha na sura za wachezaji wao lakini hata wadau nje wamekosa ubunifu wa kusimamia wachezaji hawa. Kimaisha, Kelvin Yondani anatumia siku sita kujipanga na mpinzani wake wa wikiendi na inapofika kipindi cha michezo ya Kombe la TFF au CAF basi anakuwa anatumia siku mbili kuwaza wapinzania wake tofauti na kupata maelekezo ya kocha.

Ni ngumu kwa mchezaji huyu mwenye fikra hizi kwa mazingira yetu kuweza kufikiria biashara inayohusiana na chapa yake, jambo ambalo linahitaji ubunifu mkubwa na kuweza kuonyesha sanaa yake ya upande wa pili.

Maisha ya wachezaji hawa ni biashara lakini nani atavutiwa na maisha ya Kichuya ambayo yanafanana na mimi Nicasius Agwanda ninayehangaika kutafuta fedha ili niwe shabiki yake. Hapa ndipo linapokuja suala la chapa ambayo lazima iandaliwe na watu wanaofahamu sanaa ya mchezaji husika na namna gani inaweza kupokelewa kwenye jamaii.

Cristiano Ronaldo ana mikataba zaidi ya ishirini nje ya ule aliosaini na Real Madrid. Hakeshi akiomba mikataba hii imfuate bali ana timu iliyokuwa nyuma yake iliyojenga sanaa yake na kuaminika kuwa ni mchezaji mbunifu mwenye mvuto ndani na nje ya uwanja. Unatengenezaje mvuto wa Ajib ambaye ni mbunifu ndani ya uwanja na unahusishaje na biashara za kampuni kadhaa zinazoweza kuvutiwa huko nje.

Wakati unajiuliza ni wapi na vipi wapenzi wa Simba watapenda boga ambalo ni Simba yenyewe lakini wakati huohuo wavutiwe na ua lake ambalo ni John Bocco unatakiwa uanze kutengeneza sanaa yenye umuhimu mkubwa ambayo ni nguvu ya mchezaji husika nje ya uwanja. Anawezaje kuwa kivutio cha maana na mfano wa kufuatiliwa na washabiki wengi huko kwenye jamii.

Sanaa ya michezo inaweza kuvutia kwa wakati mmoja watu wa muziki na michezo na kuwaweka eneo moja. Hakuna jambo ambalo msanii wa muziki anaweza kulifanya kimatangazo na chapa yake na mchezaji asiweze.

Muhimu ni kuwepo kwa watu watakaoweza kusimamia sanaa ya pili. Soka la Tanzania limewakosa hawa na ndio maana biashara ya kina Kichuya na Ajib nje ya uwanja inakuwa ngumu.

Umefika muda kasi ya ubongo wetu iendane na kasi ya dunia. Tuna wachezaji wenye vipaji Tanzania lakini hatuna wachezaji nyota ama wachezaji “mastaa”. Wakitoka uwanjani ni watu wa kawaida tu.