Tunaishi kwenye zama ambazo mtu kuwa na kundi kubwa la ‘marafiki’ kwenye mitandao ya kijamii inachukuliwa kuwa mafanikio.

Uhusiano huo wa mitandaoni, ni nadra kuleta tija kwenye maisha halisi. Ndiyo kusema, umuhimu wake unabaki kuwa kwenye matangazo ya biashara, kubadilishana taarifa na shughuli nyingine zisizohusisha uhusiano wa karibu baina ya watu.

Kwa upande mwingine, tunafahamu mafanikio yetu kibiashara, kazini na kwenye maisha kwa ujumla yanategemea kiwango cha ukaribu tunaoujenga na watu na wala si idadi ya watu tunaofahamiana nao.

Namna gani tunaweza kuaminika na watu tunaofahamiana nao na kujenga mtandao wa watu tunaoweza kuwategemea? Ni ujuzi tunaouhitaji. Hapa ninakuonyesha mbinu tano zinazoweza kukusaidia kujenga mtandao imara na watu.

Lenga kundi mahususi la watu

Unataka kuwa karibu na watu wa kundi gani? Unalenga watu unaoweza kujifunza kwao, waajiri, wafanyakazi wenzako, wateja, watu uliowahi kusoma nao au wenye utaalamu fulani?

Tengeneza orodha ya watu wachache wanaokidhi malengo yako kisha hakikisha unawasiliana nao mara kwa mara.

Unapowatafuta usiishie kusema, “nilikuwa nakujulia hali tu” bali nenda mbele kufahamu wanapendelea nini, vitu gani vinawagusa zaidi na shughuli wanaipa uzito zaidi. Hata hivyo, katika kuwasiliana nao epuka kuonekana wewe ni mtu usiye na shughuli unayepotezea watu muda.

Pia unaweza kuwa na kundi jingine dogo la watu ambao pengine huwahitaji kwa sasa lakini wanaweza kuwa msaada mkubwa huko uendako. Hawa wanaweza kuwa watu waliopo kwenye ofisi mbalimbali za umma. Jiwekee utaratibu wa kuwasiliana nao mara kwa mara. Tumia WhatsApp, SMS, mitandao ya kijamii kufanya mawasiliano nao hata kwa mambo ya kawaida.

Jifunze kuwasiliana na watu

Watu wengi hatujui nguvu ya mazungumzo tunapokuwa na watu. Hatuelewi siri ya kugusa mioyo ya watu tunapozungumza nao. Unaonana na mtu lakini huonekani kuheshimu muda wa mtu unayezungumza naye.

Mtu anaongea wakati huo huo anahangaika kushika shika simu, haoneshi uzingativu, hachangamki lakini bado anashangaa inakuwaje watu hawaendelezi mawasiliano baada ya kuachana naye.

Ikiwa unataka watu wavutiwe na wewe na watamani kuendeleza ukaribu na wewe, jifunze mbinu za mawasiliano. Unapokutana na mtu, kwa mfano, changamka, tabasamu, itikia vizuri kile anachozungumza mtu, ongea kwa ujasiri, uliza maswali ya maana na jibu maswali kwa ufasaha. Unapofanya hivi unaongeza uwezekano wa kujenga mahusiano ya kudumu.

Wafanye watu watamani kukufahamu

Moja wapo ya mambo yatakayoongeza uwezekano wa watu kuendeleza ukaribu na wewe ni uwezo wako wa kuwafanya wakudadisi kwa lengo la kukufahamu zaidi. Usifanye kosa la kumfanya mtu akiachana na wewe awe tayari amechoka na asiwe na shauku ya kukutana na wewe tena.

Kuongea sana, kujisifu, kulalamika, kuwasema watu ni baadhi ya tabia zinazoweza kumfanya mtu makini asitamani kukutana na wewe tena. Ukitaka kujenga udadisi wekeza kwenye maarifa na ujuzi adimu. Jifunze mambo kwa kina kwenye eneo lako la utaalamu. Bobea kwenye kitu na uhakikishe unakijua kwa kina chake.

Unapopata nafasi ya kuzungumza, usifanye kosa la kuonyesha unababaisha mambo. Tumia fursa vizuri kuthibitisha una kitu cha tofauti ndani yako na mtu akiwa karibu na wewe kuna kitu atakifaidi. Huwezi kusahaulika.

Usisubiri uwe na shida uwatafute watu

Jifunze kumwagilia mtandao wako hata kabla hujaanza kuuhitaji. Wafanye unaowafahamu wawe sehemu ya maisha yako na wasikuone kama mzigo. Hakuna mtu angependa kuwa karibu na mzigo utakaomchelewesha kwenda kule aendako.

Usiwatafute watu pale tu unapokuwa na shida. Usiwe mtu wa kukopa kopa bila sababu. Kumbuka kila anayekusaidia anapunguza wajibu wake kwako. Utakapomtafuta siku nyingine wakati wa shida anaweza kukukatatilia kwa ujasiri kwa sababu humdai fadhila.

Jifunze kula na ‘kipofu.’ Wakumbuke watu hata kwenye nyakati ambazo huonekani kuwa na shida. Kama umeajiriwa, wakaribishe watu wako kwenye shughuli zinazohusu kazi. Ikiwa kuna mikutano inayokaribisha watu kutoka nje ya taasisi, tumia fursa hiyo kuwaita watu wako.

Tafuta fursa za kuwasaidia watu

Kanuni rahisi kwenye maisha ni kuwasaidia watu kabla hujatarajia wakusaidie wewe. Jifunze, watu wako wa karibu wanahitaji msaada upi na jitahidi uwasaidie. Unaposikia mtu unayemfahamu amepatwa na matatizo usisubiri uombwe msaada. Changamkia matatizo ya watu kwa kutumia uwezo wowote mdogo ulionao.

Unapofanya hivyo unawafanya watu wakuone kama mtu wa msaada anayeweza pia kutegemewa katika nyakati fulani. Kwa namna hii, unavuta watu kwako na haitakuwa rahisi wakupuuze pale utakapohitaji msaada wao.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Mawasiliano 0754870815, twitter: @bwaya