In Summary
  • Na shukrani za pekee zaidi ni kwa yeye Rais kukubali kuja yeye mwenyewe na kujionea hali ya watu ambao mara nyingi anasikia tu kwa wabunge wao jinsi walivyo, wanavyowakilisha na kuwasilisha huko mjengoni.

Kama ni bahati basi hii ni ya kuku kutaga yai la dhahabu katika zizi la nyumbani. Tunawashukuru sana wale wote waliofanya mpango na mikakati yote ya Rais zkuja kututembelea na kuweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa barabara ya Kidatu-Ifakara (km 66.9) na ufunguzi wa daraja lililopewa jina la Magufuli Bridge lenye urefu wa mita 384.

Na shukrani za pekee zaidi ni kwa yeye Rais kukubali kuja yeye mwenyewe na kujionea hali ya watu ambao mara nyingi anasikia tu kwa wabunge wao jinsi walivyo, wanavyowakilisha na kuwasilisha huko mjengoni.

Ujio wa Rais Magufuli haukuwa wa ghafla, watu walijiandaa sana na mwisho yakawa yale tuliojionea, wakuu wa idara mbalimbali katika halmashauri tatu na wabunge wa majimbo yetu manne ya uchaguzi tumewaona walivyowasilisha maoni yao kwa kisingizio kuwa tumewatuma sisi, kwa kweli tuna safari ndefu mno ya kujifunza.

Kwa maofisa utamaduni wa wilaya za Ulanga, Malinyi na Kilombero pamoja na waandamizi wenu, kiweledi na utashi wenu mlishindwa kabisa kupata ngoma ya asili ya kutumbuiza kwa ghani na kutupa ujumbe kwa mgeni wetu, na hivyo kutuwekea CD ya makirikiri? Mtutake radhi sana sisi Wapogoro, Wandamba, Wabena, Wambunga, Wangoni, Wandwewe na Wangindo.

Mnajua kuna ngoma za asili zaidi ya 30 za hayo makabila machache yaliyotajwa hapo juu, zenye msisimko wa hali ya juu, Sangula ikiongoza, sega dansi, njinganjinga, nusu kufa, kibangasera, n.k, lakini kwa akili mgando na kukaa maofisini tu mkashindwa hata kuagiza wanafunzi waimbe shairi lenye ujumbe, hiyo ni aibu yenu idara ya utamaduni.

Mheshimiwa Goodluck Mlinga, Mbunge wa Ulanga Mashariki, kaka, mila zina wenyewe. Pamoja na jopo lako la washauri wanaokushauri juu ya uwakilishi na uwasilishaji, utuombe radhi wananchi wako kwani hujui hata maana ya hilo neno ‘shikambaku’, aliyekwambia amekudanganya, huwezi kumwambia baba au mkuu wako shikambaku, nafahamu wewe ni mbunge lakini hilo hujaagizwa, Ulanga kuna shida ya maji, barabara, huduma za afya, ikama za watumishi hazina uwiano kwenye maofisi na taasisi zetu, wewe hulijui hilo? Hujui kwamba kuna mpango wa barabara ya kupitia Chikuti, Lukande, Mwaya mbuga kuvuka mto Luwegu hadi Liwale mkoani Lindi?

Mbunge wangu wa Ulanga Kusini, Haji Mponda, tena wewe ndo mkongwe, unayo magari mangapi ya wagonjwa? Nafahamu kwako barabara si shida, hospitali yako ya wilaya je? Zahanati na vituo vya afya? kama vyote viko salama au katika kiwango nadhifu kidogo basi ungetoa neno la shukrani kwa mheshimiwa Rais wetu, kwa kweli Ulanga yote ni aibu yetu.

Tukija hapo Ifakara, Mbunge wangu kutoka Mlimba, ni kweli yote uliyoyaongea ni matatizo, ni kero, lakini hata kama uongeeje, kule ni kwa mwanao nafikiri hapo kesho anaweza akakukimbia na kuwa chokoraa mtaani, sasa ni kwa mkuu wako, unaomba unakemea au unaamrisha?

Dada yangu, kwa mtu mzima hoja na takwimu ndio mpango mzima, tena kumbuka wewe mama, jitahidi uunde lugha ya kuongea, hoja si mkazo wa sauti, ni uchaguzi wa maneno na mvuto wa sauti katika kutamka.

Na mwenye kaya wangu, Mbunge wangu Lijualikali, kwa ufupi tu hukujiandaa, pole sana. Kwa hiyo ukiipakua ile video, haya ninayoyaeleza ukiwa makini na mwenye kumakinika utaungana nami.