In Summary
  • Hadi wakati huu ninapoandika makala haya, Zuma, kama nyati aliyejeruhiwa ‘yuko msituni’ akiangalia uwezekano wa kumjeruhi mtu na kurejea Ikulu ya Pretoria.

Februari 15, ndiyo siku Jacob Zuma alishindwa kuhimili vishindo vya chama chake cha ANC vya kumtaka ajiuzulu. Hatimaye alitangaza kung’atuka akilalamika hajafanya kosa lolote na nafasi yake ya urais ikachukuliwa na aliyekuwa naibu wake, Cyril Ramaphosa.

Hadi wakati huu ninapoandika makala haya, Zuma, kama nyati aliyejeruhiwa ‘yuko msituni’ akiangalia uwezekano wa kumjeruhi mtu na kurejea Ikulu ya Pretoria.

Je, ataweza ndani ya ANC? Je, anaweza kutumiwa na upinzani?

Tutamtazama kwa kina Jacob Zuma na ili kuipata picha yake nitaanza na mifano miwili.

Novemba mwaka jana, Robert Mugabe alipoondolewa Ikulu wafuasi wake waliozoea kuishi kwa fadhila zake ghafla walijiunga na kumfuata nyumbani kwake mkononi mwao wakiwa na mpango mbadala wa kuiadhibu Zanu-PF.

Walipanga mkakati ukakubalika wakaanzisha chama kipya cha New Patriotic Front (NFP), yeye akiwa mshauri. NFP kikajipanga kushiriki uchaguzi kukabiliana na Rais Emmerson Mnangagwa wa Zanu-PF aliyepanda madarakani kwa mgongo wa jeshi.

Papara zimeiangusha NFP, haina umaarufu ikilinganishwa na Zanu-PF, na wiki iliyopita iliamua kuiunga mkono MDC-T kumkabili Mnangagwa.

Vilevile, mwanzoni mwa Mei, aliyekuwa waziri mkuu wa Malaysia, Mahathir Mohamed alifanya jambo ambalo halikutarajiwa na wengi. Aliamua kukitosa chama tawala alichowahi kukiongoza na kujiunga na chama cha upinzani, halafu akapitishwa kuwa mgombea nafasi ya waziri mkuu.

Japokuwa Mahathir alichukiwa katika utawala wake wa miaka 22 akiongoza kwa mkono wa chuma, wapigakura walimsamehe na wakampa kura nyingi zilizomwezesha kumwangusha Najib Razack, waziri mkuu aliyechafuka kwa kashfa ya ufisadi.

Ninapofuatilia mwelekeo wa siasa za Afrika Kusini, ninaposoma maandiko na makala mbalimbali, mjadala uliopo ni kuhusu uwezekano wa mpambano wa ikulu kati ya Zuma na Rais Ramaphosa ambaye ana miezi mitatu na siku kadhaa madarakani. Mipango inasukwa chini kwa chini.

Wafuasi kindakindaki wa Zuma wanaona bado ana nafasi. Wasiompa nafasi wanacheka na kukejeli ripoti za kuanzishwa chama kipya cha siasa au zaidi vyovyote ambavyo vyote Zuma anatajwa kuwa nyuma yake.

Wanaokejeli ni wale wanaohoji “hivi ni nani atampigia kura Zuma?” Pia wanawahoji wafuasi wake kuwa wanadhani ni kitu gani anaweza kukifanya sasa ambacho alishindwa kwa miaka 10 alipokuwa rais wa chama tawala cha ANC na miaka tisa ya urais.

Haya yanaweza kuwa maswali ya msingi, lakini kinachoangaliwa sasa ni juhudi za kumuibua upya Zuma kisiasa kutoka kwenye tope la ufisadi na kesi zinazomkabili mahakamani.

Katika hili Zuma atahitaji kuboresha kile kilichotokea miaka ya nyuma katika ardhi ya Afrika Kusini. Novemba 2008 ulitokea mgawanyiko ndani ya ANC. Watu waliokuwa watiifu kwa rais wa zamani, Thabo Mbeki walitangaza kujitoa ANC.

Mgogoro uliibuka baada ya ANC kumwondoa Mbeki. Hatua hiyo iliibua hasira na ghadhabu kwa wafuasi wake, wakaanza kujiondoa mmoja baada ya mwingine wakiwemo baadhi ya mawaziri ili kujenga mshikamano naye. Mwaka huo iliundwa Congress of the People (Cope) ili kupambana na ANC ya Zuma.

Waanzilishi wa Cope walidai kwamba walikuwa “wametoa talaka” kwa ANC iliyokuwa ikishutumiwa kwa kuongoza nchi “nje ya sera za kipaumbele na taratibu za kidemokrasia za ANC”. Lengo lao lilikuwa kuanzisha ‘ANC imara’ nje ya ANC iliyopo.

Wanasiasa waliokuwa wakiondoka ANC na kujiunga na Cope walikuwa wanadai walifikia hatua hiyo ya kuhama baada ya kumpa taarifa Mbeki. Hivyo, hoja ikawa kwa nini waasi hao wampe taarifa Mbeki? Mbeki alikana kuhusika na chama hicho lakini madai kwamba yeye aliridhia kuondoka kwao yalimshona barabara.

Zuma awa kitisho kwa Ramaphosa

Mazingira ya mwaka 2008 ndiyo yanaikabili ANC hivi sasa. Zuma amepambana kulinda nafasi yake tangu mwaka jana. Katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa rais wa ANC, Zuma alikuwa akimpigia debe aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Afrika, Dk Nkosazana Dlamini-Zuma lakini hakufanikiwa, badala yake makamu wake, Cyril Ramaphosa ndiye aliyeshinda.

Miezi mitatu iliyopita Ramaphosa aliongoza ANC kumwondoa Zuma kama rais wa Afrika Kusini na kuhitimisha kwa aibu utawala wake wa miaka tisa.

Katika mazingira na muda sawa na Cope ilivyoanzishwa, mipango imebuniwa ya kuanzisha “ANC” nyingine itakayochukua mkondo “kinzani” wa ajenda na sera.

Hali haiko wazi sana lakini ripoti za chinichini zinaonyesha kwamba kuna makundi mawili yanayomzunguka Zuma ambayo kwa sasa yanahaha kuanzisha chama kipya.

Kundi la kwanza ni la viongozi wa dini chini ya mwavuli wa Baraza la Makanisa ya Kiroho, muungano unaojumuisha Kanisa la Mitume 12, Kanisa la Kibantu katika Kristo, Kanisa la Kikristo la Wazayuni na mengineyo.

Baraza hili limejiweka katika mkao unaokwenda tofauti na Baraza la Makanisa ya Afrika Kusini (SACC) ambalo linajumuisha pamoja makanisa makubwa (Kikatoliki, Kianglikana, Kilutheri nk). SACC lilichukua msimamo mzito dhidi ya Zuma na Taifa kutekwa na mafisadi katika miaka ya karibuni ya urais wake.

Ramaphosa anamhitaji Zuma

Fitina zinaandaliwa ionekane ikiwa Ramaphosa na ANC wanataka kupata theluthi mbili ya kura wanamhitaji Zuma.

Makanisa hayo yamefanya mikutano kadhaa katika majimbo ya Eastern Cape, Free State na KwaZulu-Natal tangu mwaka jana, yakihamasisha wafuasi wao kuunga mkono chama kipya cha siasa ambacho kitakuwa mstari wa mbele kushughulikia masuala kama kuchukuliwa ardhi bila watu kulipwa fidia, elimu bure na benki ya umma.

Baada ya Zuma kuondolewa mpango huo umepata nguvu na ndipo likazaliwa dude liitwalo Baraza la Congress la Mageuzi Afrika (ATC).

Ushahidi wa mshikamano wao ni kwamba viongozi wote wa makanisa ya kiroho (kilokole) walifika kwenye Mahakama Kuu Durban Aprili siku ambayo Zuma alifika kwa mara ya kwanza kusikiliza mashtaka dhidi yake yanayohusu ufisadi.

Hivi karibuni, makanisa hayo yalifanya mikutano miwili Durban, mmoja wa wanawake na mwingine wa viongozi wa kitamaduni katika juhudi za kuendeleza mashauriano kuhusu kuanzishwa kwa chama kipya. Zuma alihudhuria mikutano yote miwili.

Siku chache zilizopita, kikundi cha wanaharakati kutoka KwaZulu-Natal kilitangaza kwenye vyombo vya habari kwamba kinahamasisha uungwaji mkono wa chama kipya chini ya kaulimbiu “Mazibuyele Emasisweni”.

Hawa wanadai kwamba wanaungwa mkono na wafanyabiashara ya teksi na mabasi pamoja na makanisa kadhaa.

Baadhi ya viongozi wa Makanisa ya Kikristo walishtushwa na tangazo hilo kwani wao walitaka kubaki chinichini, wakihamasisha wafuasi kwa waumini wao.

Na wakati viongozi wa makanisa bado hawajaanza kumnadi Zuma kama ndiye taswira ya chama chao, msemaji wa kundi la Mazibuyele, alisema wanatumai kwamba Zuma “atainuka na kuendelea na programu zake”.

Alisema pia kwamba wanaungwa mkono na wanachama wa ANC wanaojaribu kufanya ushawishi Baraza Kuu la Taifa la ANC lifute lile azimio la kumwondoa Zuma.

Makundi haya yote na kiongozi wa kundi la wanaharakati wa Weusi Kwanza Ardhi Kwanza, walihudhuria hafla ya mapokezi ya Zuma alipokuwa anarejea Nkandla Mei 31, ambako alisisitiza alikuwa mhanga wa kisiasa na akakata mashtaka dhidi yake kuhusu Taifa kutekwa na mafisadi. Zuma ni kama alikuwa anawasilisha kwenye jimbo lake jipya utetezi wa maandishi.

Kiuhalisi, Zuma atasema hajui lolote wala hahusiki na umoja wowote ulioanzishwa kama mbadala wa ANC. Lakini watu wanaohusika na mkakati huo wanasema wameshauriana naye.

Wakati pekee unasubiriwa kuona kama Zuma atakabiliana na mrithi wake Ramaphosa ndani au nje ya ANC.