Natanguliza shukrani zangu kwako Rais wetu mpendwa kwa utendaji wako wa kazi. Naamini si wote wataukubali lakini wapo wanaoukubali hivyo piga kazi kwa kiwango chako na uwezo wako hadi utakapofikia ukomo wa uongozi wako.

Mhe4shimiwa Rais hongera kwa uamuzi wa kuamua wastaafu wapewe stahiki zao kama zamani kitu ambacho kilikuwa kilio cha wananchi wengi ambao wapo kwenye ajira.

Dk Magufuli napenda nikupongeze kwa kutetea maslahi ya wakulima wa korosho nchini na umesema utatetea wakulima wote nchini bila kubagua kundi lolote.

Kuanzia siku zile kwenye mkutano wako shukrani sana kwa hatua uliyochukua baada ya kuona mawaziri wa wizara husika hawajiongezi na baada ya kuona bodi za mazao hazichukui hatua yeyote. Dk Magufuli Rais wangu, wakulima wa korosho hali bado mbaya sana kuliko mnavyofikiria na jinsi unavyofikishiwa taarifa. Yaani ukipita kwenye vijiji majina ya wakulima yamebandikwa kwenye ukuta wa vyama vya msingi lakini benki hakuna hela iliyoingia.

Mheshimiwa Rais, unafahamu fika asilimia kubwa ya wakulima wa Kusini korosho ndiyo uhai wao wa kuendesha maisha. Katika mashamba yao chini ya miti ile huwezi kulima mazao mengine ya kibiashara kwani hayapati hewa ya kutosha. Hayapati jua vilevile korosho inapulizwa dawa kali yaani zile sumu zinazopigwa zinarudi chini ya ardhi hata wakilima mihogo, karanga, njugu wanajikuta wanakula sumu ileile, watafanyaje na hakuna ardhi ya wazi kupanda chakula chao?

Hivyo korosho ndiyo mwongoza maisha. Watu wa kusini wanapopata hela za korosho ndio wananunua vifaa vya ujenzi na kodi inarudi serikalini. Wanalipa mafundi, wanachimba visima vya maji na hiyo ni ajira. Wananunua pembejeo kwa msimu ujao kodi hiyo wananunua sare za shule, madaftari, viatu watoto waende shule.

Wakulima pia wanatakiwa walipe vibarua watibue mashamba yao kuandaa kwa msimu ujao, kule vijiji vingi havina umeme wengi wananunua vifaa vya umeme jua wapate mwangaza na hapo kodi inapatikana.

Mheshimiwa Rais, naandika haya kwa uchungu mkubwa kwa kusemea wale wasioweza kufikisha taarifa mjini kwako na kwa kuwa wewe mpenda haki mpenda ukweli japo chungu na unatusihi tuwe wasema ukweli na kumuogopa Mungu.

Wakulima wa korosho wengi wanaishi kwa mikopo kwenye maduka ya watu vijijini na wengine wenye korosho zilizopo ndani wanauza kangomba kwa wenye nazo ili kuendesha maisha huku wengine wakibadilishana na mchele, mikate ili maisha yasonge. Huu ni ukweli kwa sisi tunaoishi vijijini tunaona haya. Naandika haya kwa dhati bila ushabiki wa chama, bila ushabiki usioleta maendeleo. Naandika haya kuwasemea wakulima wa korosho ili uone tunayoyapitia.

Rais wangu umeweka utaratibu mzuri wa uhakiki wa mkulima wa korosho mwenye kilo nyingi, tume inayoundwa na waziri wa kilimo ikijiridhisha ndiyo ilipe lakini wakulima wengi wenye kilo ndogondogo nao hawajapata hela zao. Kama huamini hili unda tume yako kinyemela ijifanye kaya masikini itembee na sisi vijijini ikiwezekana iende benki kuomba taarifa uone kama majina yaliyobandikwa kwenye kuta za vyama vya msingi na waliolipwa yanaendana. Utaona tatizo liko wapi mzee wetu kama hawakupi ukweli, wanakuongopea kwa “tunalipa”, baba huku hali mbaya sana. Ripoti inasema zaidi ya Sh200 bilioni zimelipwa kwa wakulima wa korosho, lakini hizo ni fedha ndogo kuliko tunachohitajika tulipwe.

Rais wangu, huku chini ya wizara husika na tume walizounda wanawaangusha sana, halafu wamekuja kuchuma hela si kufanya kazi waliyoagizwa. Sasa hivi kwenye uhakiki wanachukua rushwa tena wanadai kwa nguvu.

Tume ya uhakiki imekuwa na kasi ndogo sana kuliko inavyodhaniwa. Pia zile safari za mashambani hazipo kwenye hizi tume uhakiki wao ni wa kwenye makaratasi tu, nenda rudi nenda rudi kumaliza mafuta na vipuli kwenye magari wanayozunguka nayo vijiji, yaani kumekuwa na usumbufu badala ya msaada.

Ni bora hizi tume mngechukua watu kutoka mikoa ya kanda ya ziwa au kaskazini wasiojuana waje waifanye kazi kuliko hizi tume ambazo mmechukua watu hukuhuku kusini, wengine wanafanya kazi kwa kujuana na chama fulani cha msingi, wafanyabiashara wa korosho na baadhi yao ni wanunuzi wa kangomba, hivyo unachokitaka hutafanikiwa kwa asilimia 100, maana hawa wanakuangusha. Mimi pia ni muhanga wa kuombwa rushwa ya Sh100,000 na katibu tarafa ili asaidie uhakiki wangu uwe mwepesi nipate malipo ya korosho watakapoanza kulipa.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga nilimshtakia na akasema akalifanyia kazi lakini sijapata mrejesho pengine ni ana kazi nyingi.

Rais wangu mpendwa makatibu tarafa hawa wanakuchafua wanakufanya uonekane huna nia njema na zao la wananchi.

Rais wangu mpendwa, pembejeo nimezinunua bei ghali kuanzia dawa za maji mpaka sulphur za unga. Kulima korosho imekula muda wangu usiku na mchana maana muda mzuri wa kupuliza dawa za korosho ni usiku na mchana ni kulimia nakufagilia mikorosho nimeteseka kusomba maji shambani nimeingia gharama kubwa kuhudumia dhahabu nyeupe, leo niteseke pia kwenye kulipwa kwa sababu ya tume ya uhakiki kutafanyia figisufigisu?

Rais wangu mpendwa, fyekelea mbali watendaji hawa ukitaka nitakutajia majina na ushahidi unapatikana mbele yako nipo tayari kuwa muhanga kwa ajili ya wakulima wa korosho.

Tangu tufanyiwe uhakiki wa korosho kwa kujaza fomu na kujibu maswali waliyotuuliza mpaka leo hawajarudi kwa safari za kwenda kwenye mashamba tunayomiliki wakulima ili tuweze kulipwa fedha zetu tufanye maendeleo. Lakini hadi sasa tume ya uhakiki inatufanyia husuda kwa chuki kulazimisha hadi ofisa tarafa ananiambia nina korosho nyingi sana nitalipwa hela nyingi, kwanini ninakuwa bahiri wa kumpa laki moja?

Yaani anaona tunapesa za kuchezea kama mshahara wake haumtoshi aache kazi alime korosho apate zaidi yangu. nina mashamba zaidi ya manne ya korosho leo hii nitoe rushwa kupata haki yangu hili jambo mbele yako na mbele ya mungu halikubaliki.

Imeandikwa na mimi wako mkulima mtiifu

Hassan Yakub

Hayate Organic Farms Tandahimba