In Summary
  • Sababu ni wito wa kuwataka akina mama waliotelekezwa na baba wa watoto wao, kujitokeza na kutoa malalamiko yao. Mamia ya wanawake wamejitokeza na watoto wao.

Hivi sasa nchi imejielekeza Boma la Ilala katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Sababu ni wito wa kuwataka akina mama waliotelekezwa na baba wa watoto wao, kujitokeza na kutoa malalamiko yao. Mamia ya wanawake wamejitokeza na watoto wao.

Kumekuwa na ukosoaji, vilevile pongezi. Wanaopongeza wanamsifu Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda kuwa anawapigania wanawake na watoto kupata matunzo. Wakosoaji wanasema utaratibu uliotumika haufai, unawadhalilisha watoto na kuwaumiza.

Hata Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alitahadharisha dhidi yas utaratibu uliotumika, maana umevuruga hifadhi ya watoto kama ilivyotolewa mwongozo na Sheria ya Watoto namba 21 ya mwaka 2009. Kimsingi suala la watoto kutelekezwa limewateka watu wengi.

Hali kama hiyo ndiyo inafanya Tanzania iende kama daladala. Abiria anapopanda daladala maana yake safari yake ni fupi. Daladala huwa na vituo vingi, ndani ya kilometa moja, gari linaweza kusimama hata mara tatu.

Daladala linapokuwa kwenye mzunguko, lugha yake hubadilika kulingana na vituo. Ikiwa kituo kinachofuata kinaitwa Mfuga-Nyati. Utingo atawatangazia abiria kuwa wanaoteremka kwa Mfuga-Nyati, washuke.

Gari likishaondoka Mfuga-Nyati, habari zote za Mfuga-Nyati huishia hapo. Utingo hutoa tangazo jingine kuwa abiria wanaoshuka Chungu-Tamu wajiandae kushuka. Hapo kwenye gari kila mmoja fikra zake huwa kwenye lile tangazo la Chungu-Tamu.

Habari zote za Chungu-Tamu huisha mara tu utingo anapotangaza kuhusu ujio wa kituo kingine cha Pombe ya Chatu. Hivyo, fikra za abiria kwenye daladala hubadilika ndani ya muda mfupi.

Kama ilivyo kwamba ndani ya kilometa moja, agenda za abiria, utingo (konda) na dereva huweza kubadilika mpaka mara tatu, ndivyo hali ilivyo kwa Tanzania ya sasa. Taifa limekuwa na agenda za muda mfupi.

Afadhali daladala na vituo vyake kwa sababu gari likifika abiria hushushwa na kuwa mwisho wake na wale wa kituo cha mwisho hungoja mpaka tangazo la konda kwamba gari limefika mwisho. Agenda za nchi zenyewe hazina mwisho.

Upepo hubadili agenda kila baada ya muda mfupi. Bahati mbaya agenda hizo zinakuwa hazina matunda, kwamba lipo jambo lilisimamiwa mpaka kufika tamati yake. Hakuna, ni kizungumkuti.

INAENDELEA UK 24

INATOKA UK 23

Ucheshi wa ‘No Agenda’

Katika urushaji wa matangazo ya kidigitali, wajasiriamali wa Marekani, Adam Curry na John Dvorak, kuanzia Oktoba 16, 2007, walianzisha programu ya “No Agenda” ambayo ni ya vichekesho vinavyojadili hali halisi ya kisiasa.

Kama lilivyo jina la programu, Curry na Dvorak hawana agenda ya kuzungumzia isipokuwa huendesha mijadala kutokana na upepo wa kisiasa unavyokuwa ndani ya wakati husika.

Kwamba Curry na Dvorak wanapotoka kwenye kipindi kimoja, huwa hawajui nini watajadili au mazungumzo gani wataendesha kwa njia ya ucheshi (comedy) katika programu inayofuata. Upepo wa kisiasa kwa namna vyombo vya habari vinavyoripoti, ndivyo huamua nini wakifanye.

Tanzania ya sasa, ipo kama programu ya “No Agenda”. Kwamba kama nchi hakuna agenda ambazo taifa linazishika na kupanga kufika nazo mwisho. Ni upepo tu, ukivuma kushoto ndiko hukohuko fikra zote zinaelekea. Upepo ukivuma kulia kila mtu anafikiria kulia.

Ukiwa upepo ni wa kaskazini, mijadala yote ni kaskazi. Wanaopinga kaskazi na wenye kutetea mchuano unakuwa mkali. Siku upepo ukiwa wa kusini, habari zinakuwa za kusi, mijadala ya kutetea au kuushambulia upepo wa kusi.

Ni hapo inakuwa rahisi kujionyesha kwamba kama ambavyo Tanzania inaweza kufananishwa na programu ya ucheshi ya “No Agenda”, vilevile inafanana na daladala kwa agenda zake fupi kulingana na vituo.

Katika hili la nchi kutokuwa na agenda yenye kusimamiwa mpaka mwisho kisha matokeo yaonekane, makosa yanaanzishwa na viongozi serikalini, vyama vya siasa hasa vya upinzani vinacheza mdundo wa Serikali mwisho kabisa wananchi wanageuka wafuata mkumbo.

Taifa ambalo watu wake wanajadili mambo yake kwa kufuata mkumbo (band wagon), maana yake halina agenda. Na agenda ndiyo dira ya nchi. Kama nchi haina agenda maana yake haieleweki barabara uelekeo wake.

Sasa basi, tatizo la nchi kutokuwa na agenda linaanzia kwenye masuala ya maendeleo mpaka matukio yanayojiri. Vyama vya upinzani vinakosa agenda, vinapumua kwa udhaifu au makosa ya Serikali.

Kwa mwendo huohuo, Serikali nayo inafanya makosa mengi, kwa hiyo vyama vya upinzani vinajikuta vinahamia kosa la pili la Serikali kabla ya lile la kwanza halijapatiwa ufumbuzi. Mwisho kabisa, unaona kwamba hakuna mahali ambapo Serikali ilibanwa sawasawa na wapinzani mpaka mwisho.

Wakati mwingine unaona kabisa kuwa Serikali inawageuza wanasiasa inavyotaka yenyewe, kwa makosa yake au kupatia kwake. Wanasiasa nao wanacheza mdundo huohuo. Wanavurugwa na wanavurugika, matokeo yake Serikali inabaki yenye afya ndani ya vipindi visivyo na matumaini.

Agenda za upepo

Hivi karibuni kulikuwa na mtikisiko wa kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini aliyepigwa risasi Februari 16 alipokuwa kwenye daladala wakati polisi walipokuwa wanazuia maandamano ya Chadema. Likaja suala la kutekwa au kujiteka mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Abdul Nondo. Ikaibuka tamthiliya ya Nondo na polisi.

Hakuna tena anayemjadili mwandishi wa kujitegemea ambaye huripoti gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda, aliyepotea au kupotezwa tangu Novemba mwaka jana. Haijadiliwi tena miili ya watu wengi waliookotwa mfululizo wakiwa wamekufa kwenye fukwe za Bahari ya Hindi na Mto Ruvu.

Desemba mwaka juzi, nchi ilitekwa na kupotea kwa kada wa Chadema, Ben Saanane ambaye pia ni msaidizi wa mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe. Ben alitoweka katika mazingira yenye kuacha viulizo vingi tangu Novemba, mwaka juzi.

Kufikia Januari mwaka jana, habari za Ben zilififia kabisa. Tangu Desemba mwaka juzi, tukio la Ben lilihusishwa na vitendo vya utekaji, vyombo vya usalama vilizungumzwa katika nadharia mojawapo ya kupotea kwa Ben kuwa vyenyewe ndivyo vilimteka.

Kufikia Februari mwaka jana, Taifa likatekwa na habari za biashara ya dawa za kulevya, baada ya Makonda kuanzisha mapambano.

Hapa kuna tafsiri mbili, kwanza Makonda kama gavana wa mkoa ambao anaishi Ben, hakuwahi kuonyesha kuguswa popote na kutoweka kwa Ben. Hili ni kosa, kwa kuwa kwa kulikuiwa na wasiwasi mkubwa. Makonda hakupaswa kukaa kimya, ukizingatia yeye ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama.

Tafsiri ya pili ni siasa, kwamba Makonda ni CCM, wakati Ben ni Chadema, hivyo pengine hakuona ulazima wa kumtafuta mtu wa chama wanachopingana nacho. Ukizingatia kuwa Ben ni mkosoaji mkubwa wa mfumo mzima wa CCM na Serikali inayoongozwa na chama hicho.

Kitendo cha Makonda kuanzisha mapambano ya dawa za kulevya, kilibadili upepo. Habari za Ben zilifukiwa. Akina sisi ambao tuliandika mwendelezo wa makala za kuhoji kuhusu Ben, tulionekana tunatoka nje ya mdundo wa wakati husika ambao ni dawa za kulevya.

Mvurugiko wa agenda

Wakati agenda ikiwa ya dawa za kulevya, mara yakaibuka madai ya dhidi ya elimu ya Makonda, akihusishwa na mtu anayeitwa Daudi Bashite, ambaye alipata daraja sifuri kwenye mtihani wa kidato cha nne pia kuhusishwa na mtu anayeitwa Paul Christian Malanja aliyekuwa na cheti chenye matokeo mazuri ya kidato cha nne.

Masuala ya dawa za kulevya na Makonda yakaishia hapo. Kipindi cha mchakato wa vita ya dawa za kulevya kama ambavyo Makonda alikuwa akitekeleza, makosa mengi yalikuwa yakifanyika lakini watu walisahau kila kitu, hoja ikawa vyeti.

Ni kama ambavyo wakati huo wa sakata la dawa za kulevya na kipindi cha vyeti, mitaani maneno yaliyotamba sana ni “utaitwa Central”, kwamba ukiwa tofauti na Serikali au Makonda, wakati wowote unaweza kuitwa Kituo Kikuu cha Polisi, Mkoa wa Dar es Salaam.

Hoja ya vyeti ilinyamazishwa na tukio la Makonda kudaiwa kuvamia kituo cha matangazo cha Clouds TV na kulazimisha kipindi chenye maudhui ya kumshusha hadhi, kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kirushwe hewani.

Gwajima alikuwa mmoja wa watu ambao waliamua kuvalia njuga suala la vyeti vya kugushi ambalo lililomwandama Makonda. Hivyo tafsiri ya Makonda kulazimisha kipindi hicho kirushwe na Clouds TV, ni kwamba alilenga kulipa kisiasa.

Nchi ikasimama kwa suala la Clouds TV kuvamiwa na Makonda. Agenda zote za zamani zikanyamazishwa na tukio hilo. Agenda ikawa shinikizo kwamba ama Makonda ajiuzulu au Rais John Magufuli amfute kazi kwa makosa aliyofanya.

Kauli ya Rais Magufuli kuwa hapangiwi cha kufanya ambayo aliitoa siku mbili baada ya Makonda kudaiwa kuvamia Clouds TV, ikageuza agenda. Rais Magufuli hapangiwi cha kufanya na wakosoaji wa kauli hiyo.

Siku mbili baadaye, aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alipokea ripoti ya kamati aliyoiunda kuchunguza tuhuma hizo za Makonda kuvamia Clouds TV. Ripoti ilisomwa kisha akaahidi kuiwasilisha kwa viongozi wa juu, kwa maana ya Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais.

Lakini, kabla ya kufikia alichokusudia Nape aliachwa kwenye mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Magufuli. Nafasi yake ikachukuliwa na Dk Harrison Mwakyembe aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Upepo ukahamia kwa uamuzi wa Rais wa mabadiliko hayo madogo ya baraza ambao haukudumu.

Tukio la mtu ambaye anadaiwa ni ofisa wa usalama wa taifa kumtolea bastola Nape na kumtishia, alipokuwa anataka kuzungumza na waandishi wa habari, Oysterbay, Dar es Salaam, lilimeza mjadala wa Rais Magufuli na uamuzi wake kumtengua Nape.

Suala la Nape kutenguliwa likafunikwa na tukio la mwanamuziki wa rap, Emmanuel Elibariki ‘Nay Wamitego’, kukamatwa kwa tuhuma kuwa wimbo wake wa “Wapo” una maudhui mabaya kwa Serikali na viongozi wake.

Hali ikiwa hivyo, mara tamko la Dk Mwakyembe kuwa wimbo huo ni mzuri, na kwamba hata Rais Magufuli anaupenda, likabadili kibao. Wasanii na nyimbo zao nyingine za kuisema Serikali wakaonekana hawana soko tena.

Likafuata tukio la Rapa mwingine, Ibrahim Mshana ‘Roma Mkatoliki’ akiwa na wenzake watatu, jumla wanne, kuvamiwa na kupelekwa kusikojulikana. Mambo yote yakaisha, suala la utekaji likapata nguvu.

Baada ya Roma kupatikana na kueleza kidogo kilichotokea, maneno yanayotamba nchini kwa sasa ni “utatekwa”, siyo “utaitwa Central” tena. Ndivyo ambavyo fikra za watu zinavyogeuzwa kama chapati.

Tukio la Roma ndilo ambalo limesababisha hoja za kumdai Ben zirejee upya. Zimesababisha hata wabunge ambao ni waathirika wa vitendo vya utekaji waamke na kusema yaliyowapata. Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe alitoa ushuhuda bungeni kwamba yeye alipata kutekwa.

Ajabu ya jumla ni kwamba mwaka jana Bunge lilikataa kuundwa kwa Kamati Teule, kuchunguza vitendo vya utekaji. Hata hivyo, Bashe, ameshaweka kusudio la kuwasilisha hoja binafsi bungeni kuhusu vitendo vya utekaji na matukio mengine yenye kukiuka misingi ya demokrasia, utu na utawala bora.