In Summary
  • Ni katika mtizamo huo nakubaliana pia na nadharia na mifano halisi au uzoefu uliowahi kuonekana duniani ya kwamba sehemu kubwa ya mataifa au nchi ambazo zimeweka kando demokrasia na kwa hiyo kwenye nchi hizo hakuna utawala bora, sheria ni aliyeko madarakani na kikundi chake.

Wiki iliyopita nilisisitiza kwamba kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya demokrasia na maendeleo, na mara zote wito na msimamo wangu umebakia kuwa hivyo.

Sijaibuka na msimamo na mtazamo huu, historia ni rejea na tafiti lukuki ambazo zinaonyesha nchi zinazozingatia utawala wa kidemokrasia unaojikita kwenye utawala bora, utawala wa sheria, mgawanyo wa madaraka baina ya Bunge, Serikali na Mahakama, kuheshimu haki za msingi za raia, uwazi, uwajibikaji na mengineyo – ni nchi ambazo zimepata maendeleo ya uhakika sana, na hapa maendeleo nasisitiza kuwa ni maendeleo ya watu na si ya Serikali.

Ni katika mtizamo huo nakubaliana pia na nadharia na mifano halisi au uzoefu uliowahi kuonekana duniani ya kwamba sehemu kubwa ya mataifa au nchi ambazo zimeweka kando demokrasia na kwa hiyo kwenye nchi hizo hakuna utawala bora, sheria ni aliyeko madarakani na kikundi chake.

Pia katika nchi hizo Serikali ndiyo inakuwa muhimili wenye nguvu na wenye kuburuza na kuumiza mihimili mingine, suala la kulinda haki za kiraia ni hisani ya watawala na hasa kwa raia wale wasio na maoni tofauti na watawala, mambo ya nchi yanafanywa kwa siri kubwa na raia wanafanywa kuwa hawana haki ya kuyajua na suala la viongozi kuchukua hatua za uwajibikaji kutokana na maamuzi na matendo yao linakuwa ni ndoto za mchana – ni nchi ambazo ziko nyuma kimaendeleo na ama zimepata maendeleo ya Serikali zaidi kuliko watu.

Mwalimu Julius Nyerere

Kwa maneno yake mara zote alisisitiza taifa litakalo ng’ang’ania kujenga maendeleo ya Serikali na ukuu wa dola na siyo maendeleo ya watu wake, huishia katika mgogoro mkubwa wa wananchi wenye mamlaka ya kiasili dhidi ya Serikali yao ambayo ina mamlaka yanayolindwa na majeshi na dola.

Mwalimu Nyerere mara zote alitaka mataifa ya Afrika yajue yana wajibu wa kukuza uwezo wa nchi kwa uwiano wenye maslahi kwa wananchi, yaani maendeleo ya wananchi yawe kipaumbele kuliko maendeleo ya serikali.

Mwalimu alikuwa na maana kuwa, kama tunapaswa kujenga uwezo wa serikali yetu kwa kununua vifaa vya kijeshi zaidi au kuajiri askari zaidi, na wakati huohuo watu wetu wanakufa kwa kukosa matibabu, dawa, madaktari na manesi au hawana maji na miundombinu – basi Serikali inayozingatia uwiano wenye maslahi kwa wananchi lazima itaamua kuajiri madaktari kuliko askari, itaamua kununua vifaa vya hospitali kuliko magari ya kijeshi, itaamua kuleta miradi ya maji kuliko miradi ya kijeshi.

Jambo hili linaweza kuleta mjadala mkubwa sana, mjadala wenye mwelekeo wa hoja kwamba masuala yote hayo ni muhimu, ulinzi ni muhimu, matibabu ni muhimu na maji ni muhimu.

Basi kama huo ndiyo utetezi, uzoefu wa Mwalimu Nyerere na fikra zake vinatukumbusha kugawa rasilimali za taifa letu kwenda kwenye maeneo hayo kwa kuzingatia uwiano ambao mwisho wa siku utapeleka fedha nyingi zaidi kwenye maslahi ya moja kwa moja ya watu ambayo ni matibabu na maji kuliko ajira za kijeshi.

Mifano halisi

Kwa taifa kama la kwetu, kama tuna Sh100 mkononi na tuna mahitaji ya maji, matibabu, ajira za madaktari na manesi pamoja na kuajiri askari zaidi – busara zinapaswa kuwa Sh30 iende kwenye maji, Sh30 iajiri madaktari na manesi, Sh20 inanunua dawa na vifaa tiba na Sh20 iajiri askari.

Hoja ya Mwalimu Nyerere ya kuwekeza kwa watu badala ya Serikali inakuwa na mashiko makubwa zaidi kwa sababu kwa mchanganuo huo watu wanakuwa wamepata Sh80 na Serikali imewekeza Sh20 tu kwenye ujenzi wa uwepo wake. Serikali nyingi za Afrika zinatumia nguvu kubwa mno kujenga Serikali, watu na vikundi vya watu vitakavyoendelea kushika madaraka kuliko kuwekeza kwenye maisha na huduma za wananchi. Unakuta Serikali inawekeza bajeti ya kutosha kwenye majeshi na kuwakirimu watendaji wa idara za kiusalama na kudharau idara zingine.

Mara nyingi jambo hili hufanywa kwa usiri mkubwa, ndiyo maana bajeti za majeshi kwa Serikali nyingi za Afrika kufanywa kuwa siri – tofauti na mataifa yanayojiendesha kidemokrasia ambako suala la uwekezaji kwenye majeshi halipaswi kuwa siri – linawekwa hadharani ili wananchi waweze kulijadili na kutoa maoni yao. Ile hoja ya uwazi inarudi mahali hapa. Jambo hilo linawezekana kwa sababu serikali hizo zimejijenga kwenye misingi ya uwazi na uwajibikaji. Kila lifanyikalo halifanyikii gizani.

Faida kuliko hasara

Faida wanayopata wenzetu ni Serikali zao kuwajibika kupanga vipaumbele na bajeti zake kwa ulinganifu na uwiano ambao unaleta picha ya maendeleo ya watu na si ya Serikali. Inamaanisha kuwa Serikali yoyote itakayoingia madarakani inajua upangaji wa vipaumbele lazima mwisho wa siku uchukuliwe na upimwe na kutazamwa kama uliolenga kuleta maendeleo ya watu.

Huenda masuala ya ulinzi ni muhimu sana na hilo nakubaliana nalo, lakini uwekezaji mkubwa sana kwenye eneo hilo unahitaji kwanza uhakika wa eneo au taifa lenyewe, kama taifa lenu ni la amani na utulivu, kimyakimya uwekezaji na bajeti za ulinzi zinapaswa kuwa za kawaida na fedha nyingi ziwekwe kwenye maendeleo ya watu. Somalia kwa mfano, kipaumbele chao ni ulinzi, watu wanakufa kila sekunde kila mahali, hali ni mbaya. Nigeria hivi sasa wanapambana na kundi la kigaidi la Boko Haram, wanalo jukumu la kuwekeza fedha nyingi kwenye ulinzi.

Cha ajabu ni kuwa, unakuta barani Afrika, nchi ambayo imo vitani na inapambana na waasi inawekeza asilimia 20 – 30 ya bajeti yake nzima kwenye ulinzi, lakini unakuta pia nchi ambayo imo kwenye amani ya kudumu bado inawekeza asilimia 20 - 30 ya bajeti yake kwenye ulinzi. Na hata nchi iliyomo kwenye vita na machafuko, inaporejesha amani ya ndani – bado inatenda asilimia 20 – 30 ya bajeti yake kwenye majeshi. Yaani ni kama tumerogwa hivi.

Ujinga wa nchi zenye amani

Kinachotokea ni kwamba, nchi ambazo zina amani ya kudumu na zinatumia nguvu kubwa kuwekeza kwenye majeshi kuliko huduma za kiraia, nchi hizo zinaingia kwenye mgogoro mkubwa wa kimaslahi baina ya serikali na wananchi. Wananchi wa nchi hizo wanakuwa na taarifa za uhakika ya kwamba maendeleo yao yametoswa ili maendeleo ya kijeshi na kiusalama yafanyike, magomvi yanaanza kati ya serikali na raia kwa sababu raia wanaona serikali haijawekeza kwao vya kutosha – mwisho wa siku nchi hizo huingia kwenye machafuko.

Ujinga wa nchi zenye amani pia hufanywa na nchi zenye vita na machafuko. Nchi hizi zenye vita na machafuko huwa kwenye hali hiyo kwa sababu ileile ya dola kuwekeza kwenye majeshi kuliko maendeleo. Nchi hizi hunusurika sana na labda kufanikiwa kutuliza vita na machafuko kwa njia zote zinazotumika na kukubalika. Baada ya kurejesha amani, nchi hizi hurudia makosa yaleyale yaliyozitumbukiza kwenye vita na machafuko.

Mnapotoka kwenye vita na machafuko kazi inakuwa ni kuondoa makosa yenu. Kama kosa lenu lilikuwa ni uwekezaji mbovu kwenye maendeleo ya watu basi huu ndiyo muda, mmeweza kurejesha amani basi sasa wekezeni kwa watu wenu, wapate maendeleo yao ya kisiasa, kiuchumi na kijamii – ili watu hawa wawaze kufaidi maendeleo haya wanayopata kuliko jambo jingine.

Tafsiri ya maendeleo ya watu

Badala yake unakuta taifa limetoka kwenye migawanyiko, machafuko, chuki na vita – linaanza tena kuwashughulikia watu wake, linawekeza kwenye majeshi zaidi kuliko kwenye maji, barabara, ajira, matibabu na mengineyo. Linatumia nguvu kubwa kupora haki na uhuru wa watu wake, haki na uhuru wa kuzungumza, haki na uhuru wa kutoa maoni, kuishi na mengineyo.

Haya pia hufanywa na zile nchi zenye amani ya kudumu, badala zijifunze kwa wenzao ambao amani iliwahi kupotea kwa sababu ya kuwekeza kwenye maendeleo ya serikali kuliko watu, zinafanya yaleyale yaliyopelekea amani zikapotea kwenye hizo nchi nyingine.

Maendeleo ya watu kwa mujibu wa Mwalimu Nyerere siyo ya uchumi au fedha au utajiri. Maendeleo ya watu ni mambo yote yanayogusa maisha yake ya kila siku kuanzia kwenye uchumi; namna anavyopata kipato, namna alivyo na ajira, namna alivyo na mazingira mazuri ya kazi na mengineyo. Kijamii na kisiasa; namna anavyohusiana na wenzake, namna anavyoheshimiwa katika kutoa maoni yake na kulindwa kwa haki zake, namna anavyochukuliwa kama raia mwenye thamani na asiyetwezwa wala kuteswa na Serikali yake, namna Serikali inavyompa haki zote za msingi, haki za binadamu.

Kama serikali haziwezi kuleta maendeleo ya watu wake kwa uhakika, maendeleo yote ya kiuchumi, kisiasa na kijamii – serikali hizo mwisho wa siku huangushwa na watu wake, maana Mwalimu Nyerere alitabiri kwamba, maendeleo hayana maana yoyote ikiwa hayawagusi na kuwahusu wananchi wenyewe moja kwa moja au kwa kuwagusa bila shaka.

Julius Mtatiro ni mchambuzi na mfuatiliaji wa utendaji wa Serikali barani Afrika na mtafiti, mwanasheria, mwanaharakati na ni mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF. Simu; +255787536759.