Wakati mwingine yapo mambo yanayofanywa na idara au taasisi za umma ambayo ukiyatafakari unashindwa kuelewa mantiki yake.

Matokeo yake huwa unabakia umeshangaa na kujiuliza maswali, lakini kila ukitafakari utapata jawabu gani linazuka swali jingine. Hatimaye, unajiliwaza kwa kujiambia ‘ndiyo mambo’.

Miongoni mwa taasisi za Zanzibar ambazo mwenendo wa kuendesha shughuli zake unanipa shida ni mabaraza ya miji na halmashauri za wilaya.

Hivi karibuni Halmashauri ya Wilaya iliamua kufunga baadhi ya masoko iliyogharamia kuyafanyika ukarabati wa fedha nyingi, moja wapo likiwa la Bububu, nje kidogo ya mji wa Unguja.

Wafanyabiashara zaidi ya 10 wa nyama, samaki, muhogo na matunda waliokuwa wanafanya shughuli zao hapo wakatakiwa kuondoka na sasa hakuna kinachouzwa hapo sokoni. Unachokiona hapo ni paka wenye miayo ambao walizoea kutupiwa dagaa na matumbo ya masikini, lakini sasa watafute njia nyingine ya malisho, kama kwenda kuvizia kitoweo katika nyumba zilizopo eneo hilo.

Sababu iliotolewa ya kufungwa soko ati ada wanazotozwa wafanyabiashara waliokuwapo hapo haziingii katika mfuko wa wilaya.

Wafanyabiashara walilalamika kwamba wao wanalipa ada zilizowekwa kila siku na wengine kuonyesha stakabadhi. Jawabu walilopewa ni kwamba licha ya wao kulipa, fedha hazifiki wilayani na kwa hivyo uamuzi uliofikiwa na uongozi ni kulifunga soko.

Haya ni maajabu makubwa. Hata huo ukarabati mkubwa uliofanywa hapo wa soko, ikiwa pamoja na kulitanua kidogo kwa fedha nyingi ulinishangaza kwa sababu haukujumuisha na ujenzi wa choo.

Si kawaida kuona popote pale katika dunia yetu ya hivi leo kujengwa kitu kama soko au kituo cha mabasi pasiwepo vyoo.

Kwa Zanzibar huwa inaonekana mara nyingi na hizi taasisi zetu za umma ujenzi wa choo katika sehemu kama hizo si jambo muhimu. Lakini swali ni kwamba kwa nini soko lifungwe kutokana na kutopatikana mapato badala ya kuwabana na kuwawajibisha waliopewa kazi ya kukusanya mapato.

Kufunga soko si kuwakomoa wafanyabiashara wanaojipatia riziki hapo na familia zao tu bali pia ni kuwapa shida wananchi wanaopata huduma mbalimbali kutoka katika soko hilo, pamoja na paka wanaotegemea kupata chochote hapo.

Nadhani umefika wakati wa kufanya utafiti wa kina wa namna ambavyo watumishi wa mabaraza yetu ya miji na halmashauri za wilaya wanavyofanya kazi.

Nasema hivi kwa sababu yao malalamiko mengi. Kwa mfano kila siku wanaongeza katika mji wa Unguja ada za kuegesha magari ambazo ni kubwa kuliko pahala popote Afrika Mashariki.

Malipo ni Sh1,000 kwa saa hadi usiku. Duniani kote, hata Tanzania Bara, ada za kuegesha gari huwa hazitozwi baada ya saa kazi au siku za mapumziko, lakini si Zanzibar.

Baya zaidi ni kwamba hata gari iliyoegeshwa karibu na msikiti kungojea kwenda kumpeleka aliyetangulia mbele ya haki au watu walioweka hapo vyombo vyao kwenda kumuabudu Mola wao hutakiwa walipe ada za kuegesha magari. Kwa kweli huu si uungwana na umekosa utu na imani.

Vilevile umezuka mtindo wa hawa askari wa mabaraza ya miji na wilaya kupiga wafanya biashara bakora na kuchukua vitu vyao vya biashara kama meza, mabirika ya kahawa na kupeleka wanapotaka.

Unaweza kusema hao wajasiriamali wanafanya makosa kufanya biashara katika eneo ambalo haliruhusiwi, lakini kitendo cha kuwapora bidhaa zao ni dhuluma.