In Summary
  • Kura hiyo ya maoni imejawa na utata mkubwa unaosababishwa na siasa za chuki hasa katika kipindi hiki cha kura ya maoni ambayo inapingwa na vyama vya upinzani, asasi za kiraia nchini humo na jumuiya ya kimataifa.

Wananchi wa Burundi kesho watapiga kura ya maoni kufanya mabadiliko ya Katiba ambayo yatamruhusu Rais Pierre Nkurunziza kuendelea kutawala nchi hiyo kwa vipindi vingine viwili vya miaka saba mpaka mwaka 2034.

Kura hiyo ya maoni imejawa na utata mkubwa unaosababishwa na siasa za chuki hasa katika kipindi hiki cha kura ya maoni ambayo inapingwa na vyama vya upinzani, asasi za kiraia nchini humo na jumuiya ya kimataifa.

Wananchi wamejaa hofu huku baadhi yao wakiripotiwa kuuawa na watu wanaodhaniwa kupanga njama za kuharibu mchakato wa kura hiyo ya maoni. Wanaharakati na wapinzani wa mabadiliko ya Katiba wanakamatwa na kufunguliwa mashtaka.

Serikali ya Rais Nkurunziza na chama chake cha CNDD-FDD wanafanya kampeni ya kuhamasisha watu kupiga kura ya “Ndiyo” wakati vyama vya upinzani vikihamasisha kura ya “Hapana” licha ya kwamba wanadhibitiwa kikamilifu wasiwafikie wananchi.

Nkurunziza ambaye ndiye Rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini humo mwaka 2005, alikuwa ni kiongozi wa waasisi wa CNDD-FDD na alipambana msituni kuhakikisha kwamba anaiondoa madarakani serikali ya mtangulizi wake, Domitien Ndayizeye.

Alikubali kuweka chini silaha na kushindana kidemokrasia, hatimaye akashinda. Alimaliza muhula wake wa pili mwaka 2015 kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo. Hata hivyo, kiongozi huyo alikataa kuondoka madarakani na kuitisha uchaguzi mwingine.

Chanzo cha mzozo wa Burundi kilianzia kwenye tafsiri halisi ya mihula miwili ya miaka mitano kila moja kama ilivyobainishwa kwenye Katiba. Ni wazi kwamba kama Nkurunziza aliingia madarakani mwaka 2005, alitarajiwa kuondoka mwaka 2015.

Rais huyo anajitetea kwamba alipoingia madarakani mwaka 2005 alichaguliwa na Bunge na siyo kwa kura za wananchi, kwa hiyo muhula wake wa kwanza haukupaswa kuhesabika katika muda wa utawala wake kwa sababu hakuchaguliwa na wananchi.

Baada ya kukataa kuondoka madarakani mwaka 2015, yaliibuka mapigano mapya ambayo yalisababisha vifo vya mamaia ya watu na wengine zaidi ya 400,000 kukimbilia nchi jirani. Hata hivyo, uchaguzi ulifanyika, akashinda na kuendelea kuongoza Serikali ya Burundi.

Kiongozi huyo alinusurika kuondolewa madarakani mwaka huo baada ya baadhi ya wanajeshi wake kuasi. Hata hivyo, alirejea nchini huko kutoka Tanzania ambako alikuwa anahudhuria mkutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Wachambuzi wa siasa wanasema uamuzi wa Nkurunziza kung’ang’ania madarakani utaathiri makubaliano ya Arusha ya mwaka 2000 ambayo yalihitimisha vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimedumu tangu mwaka 1993 – 2006 na kusababisha vifo vya watu 300,000.

Endapo kura ya “Ndiyo” itashinda kesho, basi Rais Nkurunziza ataendelea kutawala mwa miaka 14 ijayo kuanzia mwaka 2020. Hatua ya mabadiliko hayo inapingwa vikali si tu na vyama vya upinzani bali pia Jumuiya ya Kimataifa.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Burundi (CENI) imeandaa taratibu za kupiga kura hiyo nchi nzima licha ya uwezekano mdogo wa wananchi kujitokeza kwenye uchaguzi huo kwa sababu ya hofu ya usalama wao.

Tangu Mei 17 ilipotangazwa kuwa tarehe ya kupiga kura hiyo, mauaji yametokea sehemu mbalimbali huku wapinzani nao wakizuiliwa kufanya kampeni zao za kuhamasisha wananchi kupiga kura ya “Hapana”.

Tukio la hivi karibuni lilitokea katika jimbo la Cibitoke ambako kijiji kimoja kilivamiwa na watu wasiojulikana na kuua watu 26. Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) liliripoti kwamba wauaji hao waliingia nyumba kwa nyumba wakiwa na bunduki na mapanga na kuchoma nyumba.

Waziri wa Usalama wa Raia, Guillaume Bunyoni alisema mauaji hayo ni ya kigaidi na yametekelezwa na magaidi kutoka nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Alithibitisha kwamba watu 26 waliuawa na wengine saba kujeruhiwa vibaya.

Mtandao wa waandishi wa habari wa Burundi uliripoti kwamba zaidi ya watu 50 wanaounga mkono muungano wa wapinzani wa Amizero y’Abarundi walikamatwa mwezi uliopita kwa tuhuma za uchochezi.

Kumi kati yao, walikamatwa wakisherehekea mafanikio ya mwenzao kuwasilisha vema utafiti wake wa chuo kikuu.

Wanaharakati wengine 30 wa upinzani walikamatwa wakiwa safarini kuelekea kwenye mkutano wa kampeni Mashariki mwa Burundi. Polisi walisema watu hao walikamatwa kwa sababu walikuwa hawajabeba vitambulisho vya Taifa.

Sintofahamu ya hali ya kisiasa nchini humo, imesababisha baadhi ya wananchi wa Burundi kukimbilia nchi za jirani za Tanzania, DRC na Rwanda. Serikali imekuwa ikiwahakikishia kwamba hali ya amani imerejea nchini humo na kuwataka warejee kuijenga nchi yao. Ni wazi Taifa hilo litaingia kwenye mapigano mapya ambayo yatachafua taswira yake na kurudisha nyuma maendeleo.