In Summary

 

  • Kufuata maelekezo au utaratibu fulani, ni kutekeleza matakwa ya mwongozo unaomsaidia mtu kutimiza malengo ya jambo husika kwa usahihi.

Maelezo ni ufafanuzi wa namna ya kufuata maagizo, mwongozo au mwelekeo wa kufanya jambo.

Kufuata maelekezo au utaratibu fulani, ni kutekeleza matakwa ya mwongozo unaomsaidia mtu kutimiza malengo ya jambo husika kwa usahihi.

Katika lugha ya Kiingereza, maelezo au mwongozo vimezoeleka kuitwa kwa majina kama ‘instructions, manuals, user manual, user guide, guidelines’.

Katika lugha ya kila siku kwa jamii, wanasiasa na vikundi, mwongozo huweza kuitwa sera, waraka, kanuni, mpangilio wa kazi, mpango mkakati, masharti na vigezo, sheria au katiba.

Shuleni neno “maelekezo ya mtihani” husisitizwa sana na walimu kwa watahiniwa kwa sababu wasiposoma ‘maelekezo’ kwa umakini na kuzingatia wanaweza kufeli.

Kushindwa huko hakutokani kwa sababu ya kutofahamu majibu sahihi, la hasha, bali kwa sababu tu hawakufuata maelekezo ya namna walivyopaswa kuwasilisha majibu.

Kiasili mwanadamu hapendi kufuata utaratibu; anataka awe huru zaidi wa kujiamulia mambo.

Huwa hapendi kufuata miongozo, hapendi kufuata maadili ndio maana kila siku viongozi wa dini huwa na wajibu wa kumkumbusha kufuata maagizo ya Mungu kupitia vitabu vitakatifu.

Madhara ya kudharau maelekezo

Tatizo la watu kutofuata maelekezo haliishii tu darasani kwa mwanafunzi kushindwa kufaulu mitihani au kuadhibiwa kwa kosa la kushindwa kufuata maelekezo, bali huenda mbali na kuathiri maisha ya watu wengi kila siku. Yafuatayo ni baadhi ya madhara ambayo husababishwa na watu kutofuata maelekezo:

Moja, kushindwa kufaulu masomo. Mwanafunzi anaposhindwa kufuata maelekezo ya shuleni yakiwamo wakati wa kufanya mitihani, hushindwa kufaulu. Jambo hilo huchangia vikwazo katika kutimiza ndoto zake za maisha.

Mbili, kusababisha ajali. Matukio mengi ya ajali za barabarani zinazohusisha vyombo vya moto, yamesababishwa na uzembe wa kibinadamu hususani watu kutozingatia maelekezo ya alama za usalama barabarani.

Tatu, uharibifu wa miundombinu. Kwa mfano, uharibifu wa barabara zetu unaotokana na madereva na matajiri wa malori ya mizigo kutofuata maelekezo na kuzidisha uzito. Hasara hiyo humgusa kila mmoja kupitia kodi anayolipa.

Nne, kuharibifu vifaa na mashine. Kwa mfano, vifaa vingi vya umeme, kielektroniki na mashine mbalimbali huwa na maelekezo kwa mtumiaji.

Maelekezo hayo hueleza namna nzuri ya kukitumia, kukabiliana na changamoto ndogondogo na mazingira ya sahihi ya kukihifadhi ikiwamo hali ya hewa inayoshauriwa.Haya hayazingatiwi na watumiaji wengi.

Mtumiaji asipozingatia hayo husababisha kifaa kushindwa kudumu kwa muda uliopaswa hivyo kumuongezea gharama za uendeshaji ambazo kwa bahati mbaya tena hupelekwa kwa mteja, kwa kosa tu la mmiliki wa kifaa kutozingatia maelekezo.

Mafundi wengi huneemeka kwa kutengeneza vifaa kila siku kwa sababu ya watu kutumia vifaa, vyombo au mashine hizo bila kuzingatia maelekezo ya utumiaji wake.

Hata Serikali inanufaika na faini wanazotozwa madereva au wamiliki wa vyombo vya moto kwa kutozingatia sheria za usalama wa barabarani, majini au angani.

Jambo hilo siyo la kujivunia kwa sababu makosa hayo madogo madogo yanapokua, yanasababisha madhara makubwa ya mali na vifo.

Tano, kusababisha magonjwa na hata vifo. Kwa mfano, watu wasipozingatia kusoma maelekezo yaliyopo katika dawa au vipodozi huweza kuwasababishia madhara makubwa ya kiafya.

Katika upande wa vipodozi, vipo vyenye viambata vyenye sumu inayodhuru ngozi ya mtumiaji na kumsababishia madhara makubwa katika ngozi.

Pia, magonjwa mbalimbali yasiyo ya kuambukiza yanayotokana na mifumo isiyozingatia kanuni za afya bora. Kwa mfano, mifumo mibaya ya ulaji au mitindo ya maisha ya ‘usasa’ imesababisha magonjwa kama vile kisukari, moyo, kiribatumbo, mzio, saratani na kasi ndogo au kubwa ya msukumo wa damu mwilini.

Jamii iliyoelimika huzingatia maelekezo

Watu wanaweza kutafakari kuwa ni mazingira gani katika maisha yao watakosa utaratibu wa kufuata? Jibu ni hakuna. Kumbe, shughuli zote atakazofanya mtu huambatana na kutekeleza maelekezo ya mfumo wa jamii, ambao wakati mwingine unaitwa utamaduni, mila au destutri.

Kufuata maelekezo hakukwepeki kwani kila mahali mtu atapaswa kufuata utaratibu fulani.

Kwa mfano, maelekezo yapo katika matumizi ya dawa, upigaji kura, kufanya miamala ya kibenki, vifurushi vya muda wa hewani, vifurushi vya chaneli za runinga, michezo ya kubahatisha na vyama vya kijamii.

Hivyo, ni vema jamii ikasoma na kuzingatia maelekezo mbalimbali siyo tu yakabakia katika karatasi za mitihani shuleni na vyuoni.

Kufuata utaratibu ni sifa mojawapo ya jamii iliyoelimika na kustaarabika; hali hii ionekane katika shughuli mbalimbali za maisha za kila siku.

Jamii yetu ikijenga utamaduni huo, itasababisha kupungua kwa ajali nyingi, kupungua kwa magonjwa mbalimbali, kupungua gharama za uendeshaji wa biashara, kukuza uchumi kupitia kuongezeka kwa pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa jumla.

Hivyo ni jukumu la kila mmoja kujenga mazoea ya kukumbushana kufuata maelekezo katika upangaji, utekelezaji, usimamizi na ufanyaji wa tathmini wa shughuli mbalimbali za kila siku katika jamii na taifa.