In Summary
  • Uongozi wa Wilaya waanzisha sensa majumbani na kubaini idadi kubwa ya watoto walemavu waliofichwa na hivyo kukoseshwa fursa za elimu.

Bado kuna baadhi ya jamii inaamini kupata mtoto mwenye ulemavu ni laana au mkosi.

Wengine hudiriki kuwafungia ndani watoto hao kwa kuona kama mzigo na hawana faida yoyote hata kama watawapeleka shule.

Dhana hiyo potofu imewanyima haki ya msingi ya kupata elimu baadhi ya watoto wenye ulemavu, kinyume na sheria ya haki ya mtoto ya mwaka 2009.

Wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa ni kati ya maeneo ambayo baadhi ya wazazi bado wana imani potofu kuhusu watoto wenye ulemavu.

Mkazi wa kijiji Cha kidabaga, wilayani hapo Elia Kilasi anasema; “Nimeshawahi shuhudia jambo hilo wengine wakiona wamepata mtoto mlemavu basi wanahisi ni mkosi au wamelogwa, kwa hiyo wanaanza kuwaficha ili wasionekane hasa kipindi wanapotakiwa kuanza masomo.’’

Utafiti wa shirika la Twaweza wa Julai 2014 kuhusu maoni ya wananchi juu ya ulemavu, unaonyesha kuwa mtu mmoja kati ya watatu anamfahamu mtoto mwenye umri wa kusoma shule ya msingi lakini hayupo shuleni.

Pia unaonyesha wananchi wawili kati ya kumi waliwajua watoto wenye umri wa kusoma shule ya sekondari lakini wanafunzi hao hawakuwa shule.

Mbinu ya sensa

Ofisa Elimu Maalumu wa Wilaya ya Kilolo, Biliel Maketa anasema unyanyapaa dhidi watoto wenye ulemavu umewafanya kuja na mbinu ya kufanya sensa ili kila mtoto mwenye umri wa kuanza masomo ili aingie darasani.

Anasema, sensa hiyo imesaidia kufichua watoto wenye ulemavu waliokuwa wamefichwa.

Simulizi ya kufungiwa watoto

Mwaka jana mzazi wa kijiji cha alificha mtoto wake ili asianze masomo kwa sababu ya ulemavu.

Baadhi ya wananchi waliamua kutoa taarifa za kufichwa kwa mtoto huyo kutokana na kuwepo kwa shughuli ya sensa.

“Tulipigiwa simu na wananchi wakatueleza kuhusu kufichwa kwa mtoto, tukafuatilia na kubaini ni kweli,” anasema.

Anasema baada ya kukutana na wazazi wakagundua walimfungia mtoto kwa sababu ya mtizamo finyu kuwa hata kama angeenda shule, asingefanikiwa kwa sababu ya ulemavu wake.

“Wazazi waliona mtoto wao kama mzogo lakini kumbe kutompa elimu ni mzigo zaidi. Usipomsaidia mtoto kupata elimu, unamuandalia mazingira magumu ya maisha yake na kuishia kuwa tegemezi,” anasema.

Anasema baada ya wazazi kuelewa mtoto huyo ameanza masomo ya elimu ya msingi na ni kati ya wale wanaofanya vizuri.

Anasema Septemba hadi Disemba ndicho kipindi ambacho wataalamu wa elimu wilayani Kilolo huambatana na viongozi wa vijiji kupita nyumba kwa nyumba kujua idadi ya watoto walemavu wanaotakiwa kuanza masomo ya awali.

Anasema sensa waliyoifanya mwaka jana iliwasaidia kuwapata watoto 86 wenye ulemavu mbalimbali ambao tayari wameanza masomo ya awali na walioanza darasa la mwaka huu wameanza masomo ya awali na darasa la kwanza.

Maketa anasema watoto wengi walikuwa wanafichwa na hivyo kukosa fursa ya kupata elimu.

“Kabla ya kuanza sensa hii tulikuwa tunaandikisha watoto 20 au 30 wilaya nzima, lakini tukashangaa baada ya sensa tulipata watoto zaidi ya 80, imesaidia sana,” anasema.

Anasema wananchi wenyewe walianza kutoa taarifa za wenzao kuficha watoto ikawa rahisi kuwafuatilia.

“Kwa hiyo kuna wazazi tuliwaita tukawaelimisha na kuwaambia wazi kwamba ulemavu sio kushindwa maisha, watoto wakipewa elimu wanaweza kufika mbali,” anasema.

Sensa inavyoendeshwa

Mratibu elimu kata wa kata ya Ng’uluhe, Joseph Donald anasema kwa kutumia mafunzo waliyopata, waliweza kufanya utambuzi wa watoto walemavu kulingana na mahitaji yao.

Donald anasema kuna wakati wakiwa kwenye sensa hiyo walipata taarifa ya kuwepo kwa nyumba zinazofunguia watoto ndani kwa sababu ya ulemavu.

Mwenyekiti wa kijiji cha Ng’uruhe, Simon Chivula anasema imani finyu kuhusu ulemavu ndio iliyowafanya baadhi ya wanakijiji kuwaficha watoto walemavu, wasio na hatia.

Mkuu wa idara ya watoto wasiosikia kutoka Shule ya Msingi ya Pomerini, Justine Katindasa anasema sensa imefanya shule hiyo kupata watoto wengi wasiosikia wanaofika 30 tofauti na ilivyokuwa, ambpao hawakuwa wakizidi wanafunzi 10.

Mkakati wa wilaya

Maketa anasema mkakati waliojiwekea ni kuhakikisha kila mtoto mwenye ulemavu anapata haki ya msingi ya kupata elimu.

Anasema wazazi wanaobainika kuwaficha watoto amekuwa akiwaita ofisini kwake kuwapa elimu kwanza kabla ya kuwachukulia hatua za kisheria kwa wale wanaoendelea kukataa kupeleka watoto shule.

Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdalah anaeleza kuwa wanachotaka ni kuhakikisha kila mtoto mwenye ulemavu anaanza darasa la kwanza bila kujali aina ya ulemavu alionao.

“Haijalishi ulemavu wake labda awe yule asiye amka kabisa, kila mtoto anatakiwa kuwa shuleni na hatutakubali kuona mzazi anamfungia mtoto ndani,” anasema

Anasema Serikali haitakubali kuona bado kuna wazazi wanakumbatia dhana potofu ya kuwanyanyapaa watu wenye ulemavu.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI) Jimson Sanga anasema mwamko ulioonyeshwa na na Wilaya ya Kilolo kuhusu watoto wenye ulemavu kupata elimu unapaswa kuigwa na wilaya nyingine.

‘’Kuwabagua walemavu sio kwamba wanavunjiwa haki za binadamu, pia wanaendelea kuwa mzigo kwa familia zao na taifa kwa kuendelea kuwa maskini,’’anasema.