In Summary

Sipingani na tamko hilo na wala sina nia ya kupinga. Bali ni lazima tufanye uchambuzi, maana mtu asiyefanya uchambuzi na kubungua bongo, huyu ni mfu. Mawazo tofauti si kupinga, bali ni kujenga. Mtu yeyote mwenye nia njema na mkweli, atakubaliana na mimi kwamba mkoani Kagera hivi sasa, kuna usumbufu mkubwa kwa wakulima wa Kahawa.

Sina uhakika kama tamko la serikali kwamba kahawa ni lazima iuzwe kupitia vyama vya ushirika ni la nchi nzima au ni la mkoa wa Kagera peke yake. Kwa vile nimebahatika kufanya utafiti wa jambo hili Kagera pekee, nitaliongelea kwa msisitizo wa mkoa huo, lakini nikilenga taifa zima.

Sipingani na tamko hilo na wala sina nia ya kupinga. Bali ni lazima tufanye uchambuzi, maana mtu asiyefanya uchambuzi na kubungua bongo, huyu ni mfu. Mawazo tofauti si kupinga, bali ni kujenga. Mtu yeyote mwenye nia njema na mkweli, atakubaliana na mimi kwamba mkoani Kagera hivi sasa, kuna usumbufu mkubwa kwa wakulima wa Kahawa.

Watekelezaji wa agizo hili wamelielewa vibaya na sasa watu wanajuta kulima kahawa, maana wanakamatwa, wanawekwa ndani kwa kuvuna kahawa bila kibali au kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji ili waruhusiwe kuvuna kahawa yao.

Na wale wanaofanikiwa kuivuna, na kuiuza kwenye chama cha msingi, hawapati malipo yao papo hapo. Vyama hivi vya msingi, havina fedha, pamoja na taarifa kwamba serikali imetoa fedha kwa vyama vya ushirika, lakini hazipo. Watu wanawekeza kahawa zao, wana matatizo chungu nzima – karo za shule, matibabu na mambo mengine, lakini hawapati fedha zao kwa wakati.

Sote tunaamini nia njema ya serikali yetu, lakini ni bahati mbaya kwamba nia njema hii, inakuja bila elimu, inaingiliana na siasa chafu za ushabiki na mipasho, inavuruga nia njema na kuleta balaa kubwa kwa wananchi wa vijijini.

Mkoa wa Kagera una bahati moja kubwa ambayo baadaye hugeuka na kuwa balaa. Una zao la kudumu la biashara na zao la kudumu la chakula. Kahawa ni zao la biashara na ndizi ni la chakula.

Mazao yote mawili kwa vile ni ya kudumu, yanaweza kuendelea kutoa matunda hata kama mkulima hayatunzi vizuri. Kwa hiyo mkulima wa kahawa na migomba ana uhakika fulani wa kipato bila kutegemea ubora wa zao lenyewe na hii huua kabisa ubunifu na kuchochea uvivu katika jamii.

Umuhimu wake

Kabla na miongo mwili baada ya uhuru, zao la kahawa mkoani lilikuwa ni msingi wa kila kitu. Lilisimika mfumo wa kijamii na kuathiri kwa namna nzuri, nyanja za elimu, siasa, utamaduni, dini na uchumi kwa ujumla.

Kielimu zao la kahawa lilikuwa na mfuko maalumu wa kusomesha watoto wote wa mkoa wa Kagera kuanzia shule za kati mpaka vyuo vikuu. Chama cha ushirika cha kahawa kilianzisha na kuendesha shule za kwanza za sekondari na watoto wote wa wakulima wa kahawa walipata ama punguzo maalumu katika ada au walisoma bure.

Si jambo la kutia chumvi, nikisema wasomi wa kwanza wa mkoa wa Kagera ama walisomeshwa na mfuko wa elimu wa zao la kahawa, au wazazi wao waliwasomesha kutokana na fedha zilizotokana na zao la kahawa.

Kisiasa, zao la kahawa ndilo lililokuwa agenda kuu ya wanasiasa wa mkoa wa Kagera. Mwanasiasa alihukumiwa na kupimwa uwezo wake kutokana na maono yake katika kuliendeleza zao la kahawa.

Kwa hiyo haishangazi sana kuona kuwa viongozi wengi wa kijamii wa wakati ule walikuwa ama ni wale waliokuwa na mashamba mazuri ya kahawa au waliozaliwa na kukulia katika mashamba yale na kwa hiyo walikuwa na uwezo wa kueleza shida na baraka wazipatazo wakulima wa kahawa.

Kiutamaduni, kahawa ni zao pekee lililokuwa na hadhi ya kutumika kama alama ya urafiki na hata kuunganisha koo mbili zilizoamua kuungana na kuwa na uhusiano wa damu.

Kwa hiyo ilikuwa ukiingia nyumba ya Mhaya ukakosa kupewa kahawa, ujue hutakiwi nyumba hiyo au utandawazi umemomonyoa mila katika nyumba hiyo. Kahawa ni alama ya utu, urafiki, undugu na uzawa. Wazazi huwarithisha watoto wao mibuni na mche wa kahawa ni alama ya rutuba (fertility) katika uzazi.

Kiuchumi, zao hili ndilo lililotawala medani hii. Ukubwa wa shamba la kahawa na ubora wake viliamua nani zaidi kati ya wawili washindanao. Na kwa sababu zao hili lilikuwa na uzalishaji na mapato karibu mwaka mzima, zao hili likabadili hali za watu katika familia mwaka hata mwaka.

Mathalani, baada ya mauzo halisi, bado mkulima alitegemea malipo ya baadaye, yaani tofauti ya bei kati ya soko la hapa nchini na soko la dunia. Baadaye wakulima walilipwa fedha maalumu kulingana na idadi ya miche ya kahawa aliyokuwa nayo mkulima.

Kutokana na hali ya hewa nzuri (kabla ya tabia-nchi), mibuni ilikuwa inapamba tena matunda ya kahawa lakini yasiyokuwa rasmi (endagashe), na hii ilitumiwa kwa kuvunwa na kupikwa kwa ajili ya kutafuna.

Hiki nacho kikawa chanzo maalumu cha mapato katika familia. Kwa hiyo mzunguko wa fedha katika familia ulikuwapo karibu mwaka mzima.

Mpaka miaka ya mwanzo ya themanini, hapakuwa na uhakika wa nani zaidi kati ya msomi mwenye kalamu na mkulima mwenye kahawa.

Kilichobadili mambo

Mpaka hapa mtu anaweza kuuliza nini kimetokea mpaka kuufanya mkoa wa Kagera uwe hoi kiuchumi na katika nyanja nyingine pia. Majibu yako mengi na wanasiasa ni mafundi wa kueleza ni nini kilitokea lakini bila kukidhi kiu ya wengi.

Kudorora na hatimaye kuanguka kwa hadhi ya zao la kahawa mkoani Kagera kumechangiwa na sababu nyingi, lakini zilizo wazi na kuu ni tatu. Sababu ya kwanza ni kuibuka na hatimaye kukubalika kwa ufisadi kama njia ya kuongoza vyombo vya kiuchumi hapa nchini.

Kwa miaka mingi, watumishi wa vyama vya msingi vya kahawa mkoani Kagera walifanya kazi kwa kuaminiwa na wakulima wenyewe, na sifa njema katika jamii ilikuwa ni msingi mkuu wa mtu kuajiriwa katika chama cha msingi cha kahawa. Taratibu utaratibu huu ulibadilika na ujanjaujanja ukawa sifa ya muhimu na kuwafanya makarani wa kahawa wabadhirifu na wezi wa jasho la wakulima. Hata hivi leo ukitembea vijijini unaweza kuona tofauti ya maisha kati ya makarani hao na wakulima wa kahawa. Makarani wengi na wajumbe wa halmashauri zao wanaishi katika ukwasi mkubwa wa mali wakati wazalishaji wanaishi katika umaskini mkubwa.

Hali hiyo inaonekana pia katika ngazi ya chama cha ushirika ambapo watendaji wanaogelea katika utajiri usioelezeka wakati wakulima wa kahawa hawawezi kununua hata chupa moja ya maji kwa kutumia kilo moja ya kahawa.

Hali hii haiwezi kujibiwa na maelezo ya wanasiasa kuwa bei ya kahawa imeshuka katika soko la dunia au kuwa ubora wa kahawa ya Kagera ni wa chini. Mbona makarani na watendaji wanatajirika kwa kutumia kahawa hiyo mbovu na bei hiyohiyo duni? Kwa msingi huu, rushwa iliyozaa ufisadi ni chimbuko la kahawa ya Kagera iliyokuwa baraka ya mkoa huo, kugeuka kuwa balaa na laana kwa wana Kagera.

Sababu ya pili, ni wanasiasa kugeuka wafanyabiashara ya kahawa na siasa kuingizwa kwenye vyama vya ushirika. Vyama vya siasa, na hasa chama Tawala, bado kina ushawishi mkubwa ndani ya vyama hivi.

Ushawishi huu unapelekea uongozi wa vyama hivi kushindwa kufanya maamuzi ya kujitegemea na kukubali kusikiliza maelekezo ya chama tawala na serikali.

Uongozi wa vyama vya ushirika umeingiliwa na siasa, hadi sasa huwezi kuwa mwenyekiti wa chama cha ushirika bila kuwa mwanachama wa CCM. Mfumo huu umevivuruga vyama vya ushirika na kuvirudisha nyuma kimaendeleo.

Bila vyama hivi kusimama peke yake na kuwa huru, itakuwa vigumu kuendeleza zao la Kahawa na mazao mengine ya biashara hapa nchini.

“Enzi ya Mwalimu” wanasiasa wa Kagera walichaguliwa kutokana na msimamo wao katika kutetea bei nzuri ya zao la kahawa. Hivi sasa wanasiasa wanachaguliwa kwa kuangalia utajiri wao walioupata kwa kufanya biashara ya kahawa au kwa kuwalinda walanguzi wa kahawa.

Wanasiasa wa sasa mkoani Kagera hawawezi kusimama na kutetea bei nzuri ya kahawa kwa sababu wao ndio walanguzi na wanunuzi wa zao hilo katika utaratibu wa sasa soko huria linaloangaliwa na walio wengi kuwa ni “soko holela”.

Sababu ya tatu ni magendo. Kansa kubwa ya taifa letu, ambayo bila elimu ya kutosha itaendelea kulitesa taifa letu.

Utafiti wangu kuhusu tatizo la magendo ya kahawa mkoani Kagera, unaoyesha kwamba tatizo hili linasababishwa na elimu ndogo waliyonayo wakulima juu ya athari za kuuza zao kuu la biashara kwa njia za magendo na kujua ni kiasi gani kufanya hivyo wananufaisha uchumi wa nchi jirani ambazo hazina huruma na maendeleo ya Tanzania, zaidi ya kuitumia Tanzania kujiendeleza na kujinufaisha kiuchumi.

Kati ya watu kumi wa Bukoba na Karagwe walioulizwa juu ya athari ya kuuza kahawa kwa magendo, wawili tu ndio walifahamu athari hizo na wengine nane walionyesha kuifurahia magendo wakitoa sababu nyingi za kupendelea kuuza kahawa kwa magendo kuliko kwa vyama vya ushirika:

Kwamba ukiuza kahawa yako kwa magendo unapata fedha mlangoni. Maana wale wanaonunua kahawa kwa magendo wanazifuata majumbani kwa watu na kukwepa gharama za kuisafirisha kutoka nyumbani kwenda kwenye vyama vya msingi.

Wanasema kama hujatumia baiskeli, pikipiki au gari utaibeba kahawa kichwani au kuwalipa watu wa kuibeba hadi kwenye chama cha msingi; kwamba ukiuza kahawa kwa magendo, huna shinikizo la kuisafisha kahawa yako kabla ya kuiuza, maana wale wa magendo wanainunua jinsi ilivyo, kinyume na vyama vya msingi wanaotaka uisafishe kabla ya kuiuza.

Wanadai anayeuza kahawa kwa magendo hana haja ya kununua magunia ya kutunzia kahawa na kuisafirisha kwenda kwenye kituo cha kuuzia kahawa, maana wanunuzi wanamfuata mlangoni kwa magunia yao.

Wanadai kwamba ukiuza kahawa kwa magendo unakwepa makato mengi: Ushuru wa halmashauri (asilimia 5), makato ya chama cha msingi (Sh90 kwa kilo), makato ya chama cha ushirika KCU au KDCU (Sh90 kwa kilo) na makato mengine kama michango ya kuendesha vikao vya ulinzi na usalama, kamati ya kuzuia magendo, ujenzi wa shule na zahanati na miradi mingine ya maendeleo.

Hivyo watu wanane kati ya kumi wanaangalia faida ya zao la kahawa kwa mtu mmojammoja badala ya kuangalia faida ya jamii nzima ya Kagera na taifa kwa ujumla. Wanaangalia kupata fedha nyingi na kwa haraka, maana kuna wakati vyama vya ushirika vinachelewesha malipo ya kahawa.

Kiasi kikubwa cha kahawa inayouzwa kwa magendo mkoa wa Kagera, inakwenda nchi jirani ya Uganda. Kiasi kidogo Rwanda na Burundi. Na bidhaa nyingi madukani, na hasa za kutoka nchi za nje zinatoka Uganda.

Tunachopaswa kuifanya

Panahitajika elimu kuelewa kwamba Waganda wananunua kahawa yetu kwa bei ya juu kidogo, wanaitumia kupata fedha za kigeni ambazo hununulia bidhaa kutoka nchi za nje, kisha hutuuzia bidhaa hizo kwa bei ya juu.

Serikali inatumia nguvu kubwa na fedha nyingi kuzuia magendo ya kahawa, badala ya kutoe elimu kwamba kuuza kahawa kwa njia ya magendo kunadhoofisha uchumi wa nchi, kwa vile nchi inakuwa na upungufu wa fedha za kigeni, ambazo zingepatikana endapo kahawa yote itauzwa kwenye mnada wa ndani na kuuzwa nchi za nje kutokea Tanzania.

Bila kuwaelimisha wananchi, wakafahamu faida na hasara za kuuza kahawa kwa magendo, hata ukitumia mizinga na vifaru, hutafanikiwa.

Hadi sasa asilimia kubwa ya watu wa Kagera, wanaamini kwamba ni ndoto kuikomesha magendo kwa sababu bei ya kahawa inaendelea kuwa chini upande wa Tanzania na kuwa juu nchi za jirani.

Pia kwamba ukiuuza kahawa hapa Tanzania, kuna makato mengi ambayo yanapunguza kwa kiasi kikubwa pato la mkulima.

Vilevile, Watanzania hatutumii kahawa yetu na kuikosesha soko la ndani. Endapo sote tungekunywa kahawa ni wazi bei yake ingepanda inataka isitake.

Bila sisi kutengeneza soko la ndani, bila sisi wenyewe kunywa kahawa yetu wenyewe, ni vigumu kuhakikisha bei ya juu. Nchi nyingi zinalima kahawa, na kwa kiasi kikubwa kahawa yao ni bora zaidi ya kwetu. Kati ya watu ishirini walihojiwa na mwandishi wa makala hii, mmoja tu aliyetaja kunywa kahawa.

Ukiwa Bukoba na Karagwe, ukitengenezewa kahawa ya kunywa, utaambiwa “Karibu ka chai”. Kasumba hii kwamba mtu anapokunywa kahawa, anakunywa chai ilitoka wapi? Hapa panaihitajika utafiti na uhamasishaji mkubwa.

Je, viongozi wa serikali wanafahamu kwamba tunaweza kupambana na magendo ya kahawa kwa kuhakikisha bei ya kahawa iko juu kuliko nchi zote zinazotuzunguka? Na kwamba tunaweza kupandisha bei ya kahawa kwa kuhakikisha watu wanakunywa kahawa kwa wingi? Badala ya kutumia fedha nyingi kwenye kamati za kuzuia magendo ambazo hadi leo hii hazijaleta matokeo mazuri, kwa nini fedha hizo zisitumike kuwaelimisha na kuwahamasisha watu kunywa kahawa?

Kwa kawaida bei ya kahawa inapanda kulingana na aroma (ladha) yake. Hivi kama mtu hanywi kahawa, anaweza kufahamu aroma yake? Kama mtu hanywi kahawa atafahamu njia za kutumia kuongeza aroma ya kahawa? Au utunzwaji wa kahawa ili kuongeza aroma ya kahawa?

Kwamba kahawa ikiwa chini ya kivuli aroma yake inaongezeka? Kwamba ukichanganya mbivu na mbichi unaharibu aroma, au ukiikausha ardhini, udongo unaharibu aroma? Hii ina maana kwamba hata kama wakulima wangeruhusiwa kuuza kahawa yao kwenye mnada, wasingeweza kupambana na kubishania bei, maana hawafahamu aroma ya kahawa.

Wakulima wa kahawa, wakinywa kahawa, watafahamu aroma ya kahawa na njia za kuongeza aroma ya kahawa, na kwa njia hii kahawa yetu itapata bei ya juu kwenye soko la dunia na kwa njia hiyo tutakuwa na bei nzuri na hakuna atakayeuza kahawa yake kwa njia ya magendo.

Hitimisho la utafiti huu juu ya magendo ya kahawa mkoa wa Kagera, hasa Bukoba na Karagwe ni kuhakikisha wakulima wanaelimishwa juu ya umuhimu wa zao hili la Kahawa kwa uchumi wa taifa letu ndipo tutafanikiwa kupambana na magendo ya zao hili inayoendelea kwa kasi ya kutisha mwaka hadi mwaka na sasa hivi ambapo msimu wa kuuza kahawa mwaka huu bado unaendelea. Hatuihitaji bunduki, mabavu au kuwafunga watu ili kuzuia magendo ya kahawa, tunahitaji elimu tu.

Padre Privatus Karugendo

+255 754633122