Mwaka wa 2018 utabakia historia katika maisha ya Watanzania hususani kundi la wadau wa siasa waliotumia zaidi fursa ya mitandao kupaza sauti zao katika kuchambua, kuhoji na kupashana habari zilizogusa maslahi yao.

Yapo matiko ambayo kamwe hayatasahaulika yaliyotikisa siasa za nchini likiwamo la wabunge 10 na madiwani 146 kuhamia CCM, matamko ya viongozi wa dini kupigania haki na usawa, viongozi zaidi ya 20 wa vyama vya upinzani kupandishwa mahakamani na mawaziri watatu kutumbuliwa.

Wakati hayo yakiwa vichwani mwa Watanzania, mwaka 2019 umefungua ukurasa mwingine unaotarajia kupandisha joto la kisiasa kupitia matukio mbalimbali yanayotazamiwa.

Matukio hayo ni uchaguzi wa serikali za mitaa, utekelezaji wa azimio la Zanzibar, maboresho ya Daftari la Wapigakura na muswada wa sheria ya vyama vya siasa.

Tayari vyama vya siasa vya upinzani vimeanza harakati ndani na nje ya mahakama kupinga muswada sheria. Huku vikiwa vimetoa tamko la Zanzibar dhidi yake, vyama hivyo vimeanza kulitekeleza kwa kufungua kesi mahakamani kuupinga.

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe anasema vyama hivyo vitautumia mwaka 2019 kudai demokrasia.

Wakati wanasiasa hao waliyatazama mambo kwa upande huo, msomi wa masuala ya siasa, Profesa Mwesiga Baregu anasema bado hali itakuwa ni tete katika kipindi hiki kwani ni mambo mengi yaliyolalamikiwa lakini hayajafanyiwa kazi.

“Kuna maazimio ya Chamwino hadi leo hayajatekelezwa, juzi kulikuwa na mikutano ya kutafuta maridhiano chini ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa vyama vyote vya siasa lakini yakasitishwa ghafla, najiuliza hivi ni kwa nini serikali haioni umuhimu wa kujenga maridhiano? Haya yatakayotokea mwaka huu ni kama vile Taifa tumechagua kutembea gizani,” anasema Profesa Baregu.

Profesa Baregu anasema endapo serikali ingekubali kujenga maridhiano, kusingekuwa na ulazima wa kuingia katika presha ya madai ya Tume Huru ya Uchaguzi au tamko la Zanzibar linalopigania uhuru na haki ya kufanya siasa nchini pamoja na ukandamizaji wa kisheria.

Profesa huyo anasema hakuna haja ya kukata tamaa kwa wadau wa siasa na badala yake kuhakikisha wanaendeleza mchakato wa maridhiano ulioanzishwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere ili kuepuka hatari inayoweza kujitokeza.

Wakili na mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, Dk Onesmo Kyauke anatoa tahadhari kuhusu namna ya kuyaendea matukio hayo, akishauri yanayohusu madai, upinzani utumie njia ya mahakama ili kupata uhalali wa kupigania hayo na siyo kutumia nguvu.

Dk Kyauke pia anassema joto hilo la kisiasa lisingeweza kujitokeza endapo uchaguzi wa serikali za Mitaa ungeunganishwa na uchaguzi mkuu wa 2020. “Tukiunganisha na uchaguzi mkuu itaongeza hamasa na kupunguza gharama,” anasema.

Maslahi ya kisiasa

Katibu Mkuu wa CCK, Renatus Muhabhi anasema kinachofanyika ni fursa iliyoandaliwa mahususi kupigania madai ya msingi kwa upinzani na haki wanayoikosa wananchi, kati si fursa ya kujitafutia umaarufu wa kisiasa.

Muhabhi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vyama 11 visivyokuwa na uwakilishi bungeni anasema watawala duniani ndiyo wamekuwa chanzo cha kuleta machafuko baada ya kukosa uvumilivu katika ushindani wa siasa za mfumo wa vyama vingi.

“Tatizo siyo wanasiasa ila ni watawala huwa hawapendi kutoka madarakani kwa hiyo hutengeneza mazingira ya kukandamiza yeyote anayeibuka kuwapa changamoto, ndiyo huleta hofu kwa wananchi. Sisi tunapigania haki ya kisheria na kikatiba ila wao wanatafsiri ni uchochezi,” anasema Muhabi.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Ahmed Msangi anatoa tahadhari ya kiusalama katika matukio hayo, akiwataka wanasiasa kuhakikisha wanafanya shughuli hizo za kisiasa kwa kuzingatia taratibu na sheria zilizowekwa.

“Watanzania tunatakiwa kufahamu hii ni nchi yetu, ndiyo mahali tunapoweza kujidai. Suala la utulivu na usalama hatuna budi kulishikilia kwa mikono miwili kwa kipindi chote, iwe katika uchaguzi au isiwe,” anasema.