In Summary
  • Mambo ya kujifunza kutoka nchi hizo tatu ni kwamba vyama tawala hasa vikongwe kokote duniani vina kila sababu ya kuhofia. Kwamba upinzani mkali au mgawanyiko wa ndani ni hatari kuliko hata upinzani wa nje.

Muda wa mageuzi ukifika katika taifa lolote lile, watu walewale wanaoshangilia vyama tawala hutumia sanduku la kura kufanya mabadiliko yasiyotarajiwa kuuingiza madarakani upinzani kama ilivyotokea Sierra Leone, Armenia na kwa kirefu nitaelezea mkasa wa Malaysia.

Mambo ya kujifunza kutoka nchi hizo tatu ni kwamba vyama tawala hasa vikongwe kokote duniani vina kila sababu ya kuhofia. Kwamba upinzani mkali au mgawanyiko wa ndani ni hatari kuliko hata upinzani wa nje.

Kwamba vyama vya upinzani vinahitaji sana wanasiasa mashuhuri kutoka kwenye vyama tawala kujiunga na upinzani ili kuvishinda vyama tawala na kuingia madarakani.

Mambo mengine ya kujifunza huko ni kwamba suala la umri wa rais au waziri mkuu halina maana kwani kinachohitajika ni hekima katika uongozi. Kwamba viongozi wastaafu wana fursa ya kurudi kwenye siasa na kusaidia upinzani kushinda ikiwa mifumo waliyoiacha itakuwa imeparaganywa na watawala wapya.

Vilevile mengine ya kujifunza ni kwamba kiongozi aliyeonekana mbaya katika kipindi chake anaweza kuonekana lulu akilinganishwa na kiongozi aliyeko madarakani. Kubwa zaidi ni ukweli kwamba mamlaka ya nchi yako mikononi mwa wananchi – wanaweza kutumia nguvu au kura kukipa chama chochote fursa ya kuongoza.

Matokeo ya uchaguzi uliofanyika Machi 31 nchini Sierra Leone yanaonyesha aliyewahi kuwa kiongozi wa kijeshi mwaka 1996 Julius Maada Bio ambaye alipitishwa kuwania urais na chama cha upinzani cha Sierra Leone People’s Party (SLPP) ndiye alishinda kwa asilimia 51.8 dhidi ya mgombea wa chama tawala cha All People’s Congress (APC) Samura Kamara aliyepata asilimia 48.1.

Pia, matokeo ya uchaguzi wa Armenia wa Mei 08 yanaonyesha, baada ya sarakasi nyingi na kuswekwa mahabusu, kiongozi wa upinzani Nikol Pashinian akiongoza muungano wa ‘Way Out’ Alliance (Yelk) japokuwa hakuwa na wabunge wengi, aliwavutia wabunge wa chama tawala cha Republican Party of Armenia (RPA) alichowahi kuwa mwanachama, wakamchagua kwa asilimia 59 dhidi ya 42 alizopata mgombea wa chama tawala. Pashinian alisaidiwa na umaarufu wake, alivyoendesha mapambano licha ya kutiwa jela na pia wabunge wa chama tawala kutaka mageuzi.

Pashinian anakuwa waziri mkuu mpya akichukua nafasi ya Serzh Sargsyan wa chama kilichoongoza tangu nchi ilipojiondoa kutoka iliyokuwa Soviet mwanzoni mwa mwaka 1991.

Siasa za Malaysia

Pengine mfano wa kuonyesha mabadiliko ya siasa ni kilichotokea Malaysia. Matokeo yanathibitisha kwamba watu wakikuchoka mfumo wa siasa unaosimamiwa na chama wako radhi hata kuchagua ‘jiwe’.

Malaysia waliamua Jumatano Mei 8 kwamba “Ya Kale ni Dhahabu” wakamrejesha madarakani aliyewahi kuwa waziri mkuu Dk Mahathir Mohamad (92) kuwa waziri mkuu mpya.

Uamuzi wa Wamalaysia ni wa kushangaza kwani katika kipindi chake cha uongozi kama waziri mkuu kwa miaka 22 (1981-2003), Dk Mahathir alionekana dikteta na mbaguzi na baba wa taifa lakini sasa anaonekana bora kuliko waziri mkuu aliyemaliza muda wake Najib Razak.

Kilichomponza Najib ni kushindwa kwake kutolea ufafanuzi tuhuma za ufisadi wa serikali yake na uchumi kuzorota. Kulikuwa na madai ya muda mrefu kutoka Marekani kwamba utawala wake ulihusika na upotevu wa dola za Marekani 4.5 bilioni (Sh10,265.175 bilioni) za mfuko wa uwekezaji (1MBD) kati ya mwaka 2009 na mwaka 2014.

Kwamba Najib mwenyewe aliwekewa kwenye akaunti yake ya benki dola 700 milioni (Sh1,596.805 bilioni) Mara zote alidai hakufanya kosa lolote.

Pia, alishindwa kusoma nyakati kwani alikuwa anakabiliana na mtu ambaye umaarufu wake ulipanda juu ghafla. Dk Mahathir aliliona hilo akaamua kurejea kwenye siasa baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa chama tawala cha Barisan Nasional (BN) ambacho kimetawala Malaysia kwa miaka 66 tangu ilipopata uhuru kutoka Uingereza.

Ukorofi wa Mahathir

Wamalaysia wanamjua Dk Mahathir? Katika uongozi wake Wamalaysia walishangazwa alivyokorofishana na naibu wake Anwar Ibrahim. Wawili hao walionekana kuwa karibu sana lakini mambo yalibadilika baadaye na kuwa mabaya kwa Ibrahim hadi akafukuzwa mwaka 1998.

Mahathir alimshutumu naibu wake kwamba hana “maadili mema” ya kiuongozi. Alishutumiwa pia kwa ubakaji na ufisadi na baadaye alifunguliwa mashtaka na mwishowe alifungwa miaka tisa japokuwa wakati wote amekuwa akikana.

Hivi sasa Mahathir ndiye amemwombea msamaha kwa Mfalme ili aachiwe. Lakini manyanyaso aliyopata Anwar kisiasa na yeye binafsi yalichochea vuguvugu jipya la Reformasi lililoandaa maandamano mfululizo dhidi ya serikali ya Mahathir na yakawa chanzo cha kuanzishwa chama cha Parti Keadilan Rakyat. Chama hicho pamoja na Democratic Action Party na Parti Islam se-Malaysia (PAS) viliunda ushirikiano ambao kwa mara ya kwanza ulikuwa kitisho cha kweli kwa BN.

Pia, katika utawala wake hakuwa mtu wa mzaha. Alikuwa akifukuza majaji anaotofautiana nao, aliwakataa waandishi asiowapenda na alikataa kuridhia masuala kadhaa ya haki za binadamu. Huyo ndiye aliyepewa kazi ileile ya uwaziri mkuu.

Kurejea kwake kwa ghafla kugombea nafasi hiyo ya waziri mkuu na hatimaye kushinda kunahitimisha utawala wa BN, muungano ambao uliiongoza Serikali ya Malaysia tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Waingereza.

Matokeo rasmi yalionyesha muungano wa Mohamad wa Pakatan Harapan ulishinda viti 113 kati ya 222 vya Bunge, hatua inayouwezesha kuongoza Serikali. Kwani Muungano wa Najib, ulipata viti 76 pekee.

Dk Mahathir alinukuliwa akisema hawana mpango wa kulipiza kisasi, dhidi ya Serikali ya Najib, iliyokuwa imeelemewa na kashfa za ufisadi, bali wanataka kurejeshwa utawala wa sheria.

Afukua makaburi

Dk Mahathir ameahidi kufanya upya makubaliano ya mikataba na China, pamoja na kubadilisha baadhi ya sera zilizotekelezwa na Serikali ya Najib, ambazo ni pamoja na kodi za bidhaa na huduma iliyoanzishwa na Najib na pia kupitia upya sheria ya uwekezaji wa kigeni. Atafanya hayo katika kipindi cha siku 100 tu za kuwa madarakani.

Tayari ameanza kutekeleza ahadi ya kufanyia uchunguzi kashfa za ufisadi zinazomkabili Najib na mkewe Rosmah Mansor. Mwishoni mwa wiki Najib na familia yake walizuiwa kuondoka nchini na polisi walivamia nyumba yao na kuifanyia upekuzi.

Kwamba hadi Mei 8 Najib alikuwa mwenye mamlaka makubwa, lakini baada ya kupoteza uongozi kwa upinzani polisi walewale aliokuwa anawatumia kukandamiza upinzani ndio wanatumika kumzuia, kumfanyia upekuzi na akikutwa na makosa atashtakiwa katika mahakama zilezile alizozitumia kwa manufaa ya mfumo uliokuwepo.

Rais wa Sierra Leone alisema serikali yake haitajikita kusaka mchawi, lakini waziri mkuu mpya wa Armenia tayari amewafukuza mkuu wa Jeshi la Polisi na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa.