In Summary
  • Wataalamu wanasema kuna aina kuu mbili zinazojulikana zaidi duniani kote za kisukari. Aina ya kwanza huitwa ‘diabetes type one’, na ya pili huitwa ‘diabetes type two’.

Kisukari ni ugonjwa unaoshambulia watu wengi. Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinasema takriban kila watu wanane wenye umri wa miaka 20 hadi 60, kuna mmoja anaugua ugonjwa huu.

Kisukari, ugonjwa unaojulikana kwa jina la kitaalam ‘Diabetes mellitus’ ni hali ya mwili kutokuwa na nguvu sawasawa kwa sababu kiungo kiitwacho ‘Pancreas’ kinashindwa kutoa homoni iitwayo ‘Insulin’ sawasawa au kutotoa kabisa na hivyo kusababisha sukari hiyo kuenea kwenye damu badala ya kugeuzwa nishati za kuufanya mwili kuwa na nguvu. Ni kawaida kwa wanaume wengi wanaougua ugonjwa huu kulalamikia pia tatizo la kupungua nguvu za kiume bila kujua kuwa si nguvu hizo pekee zinazopungua bali ni mwili wote hukosa nguvu na tatizo hili huwakuta hata wanawake pia na kujikuta wakishindwa kumudu kufanya tendo la ndoa.

Wataalamu wanasema kuna aina kuu mbili zinazojulikana zaidi duniani kote za kisukari. Aina ya kwanza huitwa ‘diabetes type one’, na ya pili huitwa ‘diabetes type two’.

Lakini leo tutazungumzia aina nyingine ya tatu ambayo haifahamiki sana kwa kuwa imejificha katika aina ya pili ya ugonjwa huu.

Hii ni muhimu kwa wagonjwa kuijua kwa kuwa wengi wamejikuta wakinunua kila aina ya dawa inayotoa ahadi ya kuponya na kujikuta wakipoteza muda na fedha bila mafanikio. Hii ni kwa sababu ya kutojua aina ya ugonjwa unaougua na hivyo dawa unazotumia si sahihi.

Kisukari aina ya kwanza

Huu ni ugonjwa ambao mtu hujikuta akiugua toka akiwa mdogo. Kwa kawaida aina hii ya ugonjwa huwa haina dawa na utatakiwa uwaone wataalamu wa afya ambao wakigundua hali hii kwa kawaida watakushauri utumie sindano au vidonge vya kuzalisha homoni ya insulin bandia kwa maisha yako yote.

Hoja hapo ni kwamba, kiungo kiitwacho pancreas hakifanyi kazi kabisa hivyo mwili wako hauzailishi homoni iitwayo Insulin. Kadiri unavyoweza kuwaona watu wenye ulemavu wa viungo kwa nje, basi ieleweke pia kuwa wapo watu wenye ulemavu wa viungo kwa ndani ya mwili hivyo ni kawaida mtu kumtokea mtu yeyote akazaliwa na pancreas yenye ulemavu na kujikuta akiugua aina hii ya ugonjwa wa kisukari aina ya kwanza.

Kisukari aina ya pili

Wakati wagonjwa wenye kisukari aina ya kwanza wako wachache, lakini aina hii ndiyo yenye wagonjwa takriban asilimia 60 hadi 70 ya wagonjwa wote wa kisukari. Huu ni ugonjwa ambao watu wengi hukutana nao wakiwa watu wazima wenye umri wa miaka 35 na kuendelea. Sababu za kuugua ugonjwa huo zipo nne ambazo ni muhimu kuzifahamu ili kama unaugua, uelewe namna ya kupambana nao.

Sababu ya kwanza ni kunenepa kupita kiasi. Ifahamike kuwa unapofika umri wa miaka 35 na kuendelea ni kipindi ambacho unauhama utoto na kuwa mtu mzima na hapo majukumu hukuandama.

Kipindi hiki ubongo hutumika sana na bila kujua watu hula sana bila kujijua kwa kuwa ubongo hutumia takriban asilimia 30 ya kila unachokula. Hivyo usipojijua utajikuta unakula zaidi na hatimaye utajiona umenenepa na hata kuota kitambi. Kwa kawaida, mwanaume anatakiwa ale kilo za calories 1,800 hadi 2,200 tu kwa siku wakati mwanamke anatakiwa ale kilo calories 1,600 hadi 1,800 tu kwa siku.

Ukizidisha hapo utahisi uzito kuongezeka na utajiona umenona kwa kuwa ziada ya chakula mwilini hugeuzwa mafuta na kutunzwa kama akiba nje ya mwili kwenye ngozi na hapo mtu hujikuta amenenepa. Lakini viungo vya ndani ya mwili navyo pia hunona kwa mafuta hivyo pancreas ikizungukwa na mafuta mengi, hushindwa kutoa insulin sawasawa na hatimaye mtu kujikuta akiugua kisukari aina ya pili. Sababu ya pili ni matumizi mabaya ya pombe. Kwa kawaida pombe hususan bia, hutengenezwa kwa nafaka na sukari nyingi. Unywaji wa pombe wa kupitiliza humfanya mtu kunenepa na kuipa kazi ngumu pancreas ya kutoa insulin nyingi itakayowezesha sukari yote aliyokula igeuzwe nishati mwilini.

Licha ya kuua viungo kama figo, ini na vinginevyo, ulevi wa kupindukia huiharibu pancreas na baada ya muda mtu hujikuta akiugua ugonjwa wa kisukari wa aina hii ya pili. Ukiachana na ulevi, matumizi ya dawa kali kwa muda mrefu pia huwafanya watu wajikute wakiugua ugonjwa huu hatari wa kisukari. Sababu ya tatu ni ujauzito. Lakini kundi hili halina wagonjwa wengi japo wapo. Mwanamke anaposhika ujauzito hutokea mvurugiko wa homoni mwilini na hasa homoni iitwayo insulin na kumfanya awe na uwezekano wa kuugua kisukari kipindi chote cha ujauzito bila kujua sababu ni nini. Hata hivyo, wengi hupona miezi michache baada ya kujifungua.

Sababu ya nne ni uzee.

Takriban wazee sita katika ya 10 huugua kisukari aina ya pili. Hii hutokea kwa sababu uzee ni nyumba ya maradhi mengi. Ukimuona mzee utabaini kuwa ana nywele zenye mvi, hawezi kutembea sawasawa, ngozi ina makunyanzi na mengineyo mengi. Hapo unapaswa kuelewa kuwa sio viungo vya nje uvionavyo kwa macho tu ndio vimezeeka la hasha! Hata vya ndani ya mwili wake navyo huwa vimechakaa ikiwemo kiungo hiki kiitwacho pancreas. Hivyo pancreas ikichakaa ujue kuwa haitaweza kutoa homoni ya insulin sawasawa na kumfanya mzee augue ugonjwa huu.

Kwa bahati nzuri, wazee wengi wakipimwa sukari huwa haizidi 15 kiwango ambacho sio kikubwa sana ukilinganisha na makundi mengine ambayo kipimo hufikia hadi 30 ambayo ni hali mbaya. Wapo pia wanaokutana na ugonjwa huu kwa kurithishwa tu hivyo unapooa au kuolewa ni muhimu kuchunguza historia ya afya ya familia ya mwenza wako kabla hamjaoana ili msije mkazalisha familia itakayorithi maradhi baadaye.

Ukiugua Kisukari ufanyeje?

Tumeona jinsi watu wanavyojikuta wakiugua ugonjwa wa kisukari kwa namna mbalimbali. Hivyo kitu cha kwanza kufanya ni kutonunua dawa yoyote mtaani inayoahidi tiba kwa kuwa kisukari ni ugonjwa wenye aina tofauti zaidi ya tano kama tulivyoona hapo juu.

Ili kuutibu, mtaalamu wa afya ndiye mwenye jukumu la kukuhoji na kujua ni tiba gani itakufaa kulingana na unavyougua. Ukifika hospitali, daktari atakupima na akigundua unaugua ugonjwa huu, atakupeleka kwa daktari mwingine aitwaye ‘Dietician’ ambaye atakushauri namna ya kula vyakula salama kwa ugonjwa wako. Hii itahusisha kutokula sukari, mafuta, chumvi na baadhi ya vyakula vingine. Baadaye utapimwa macho ili kuona kama tayari ugonjwa huu umeanza kushambulia sehemu hizo, miguu, ini, figo n.k. na baadaye utapewa pia dawa kama itaonekana zinahitajika.

Dk John Haule (Dietician)

0768 215 956