In Summary
  • ‘Ole wako usichape barua yangu kwenye kagazeti kako. Lazima ukweli uchapishwe si maneno ya ajabuajabu’

Mnamkumbuka yule jamaa aliyejiita Musa Lendo? Alikuwa ameniachia siku nyingi lakini jana akajitokeza tena, duh! Kama kawaida yake, hakuna cha hodi wala habari. Anasukuma mlango kwa nguvu na kunifuata kana kwamba ana mpango mbaya juu yangu lakini anasimama na kunipa karatasi, huku akisema, kama kawaida yake:

‘Ole wako usichape barua yangu kwenye kagazeti kako. Lazima ukweli uchapishwe si maneno ya ajabuajabu’

Kisha, kabla sijaweza kutamka neno, anageuka na kuondoka huku akifunga mlango kwa nguvu hadi nyumba inatingishika. Dah! Lakini kuwa mambo ya siku hizi sote tunajua, nashukuru kwamba sijapotea na kuibuka kwingine. Na kulingana na vitisho vyake, hebu nitoe waraka wake kwa sisi sote.

Makengeza,

Bila shaka, wewe, kama wenzako wote mmeanza kubisha ooh, kwa nini CAG ‘haCAGui’ hadi migodini? Mambo gani yanafichwa hapo? Hakuna lolote. Hebu ni mimi niulize. Kwa nini ‘aCAGue’ wakati ni dhahiri kwamba ‘uCAGuzi’ ni uchafuzi? Tayari ameshachafua vya kutosha na uCAGuzi wake wa maeneo mengine, halmashauri, manispaa, mawizara, elimu, uchafu kila mahali. Sasa tukimruhusu kuingia migodini, badala ya kutuwezesha kupata faida zaidi na madini yetu, atazidi kuchafua. Ndiyo faida ya ukuta. Inazuia wizi na pia uCAGuzi.

Kweli nakuambia, huyu CAG ni hatari. Ni hatari sana maana kwa taarifa zake za uongo na ukweli, anajenga chuki dhidi ya Serikali. Nani kamwambia aanike uchafu wote hadharani. Hajui msemo wa ‘usimwage mchele kwenye kuku wengi’. Maana watadonoa, watadonoa, watachokonoa, wataleta ubishi na upinzani usio na maana yoyote.

Ndiyo. Utatoaje takwimu za upoteaji wa fedha, matumizi mabaya ya fedha, ukopaji wa hovyo na kadhalika hadi waheshimiwa mawaziri na heshima zao wanalazimika kusimama na kujitetea kama vile watoto walioiba pipi. Huu ni udhalilishaji kabisa wa Serikali yetu na ni lazima ukomeshwe mara moja. Hebu fikiria jinsi hawa wapinzani wasio na kichwa wala miguu wanavyofurahia. Hivi kweli huyu jamaa si mpinzani na yeye? Haoni aibu?

Hebu nichukue mfano mmoja tu, hali ya elimu. Yaani, baada ya kusoma takwimu zake kuhusu hali ya shule zetu, nimepigwa butwaa. Haiwezekani. Haiwezekani kwamba katika shule zetu za sekondari kuna upungufu wa madawati asilimia 86. Ni uongo. Ni uzushi. Ni uchafuzi.

Baada ya miaka yote ya kutoa ruzuku kwenye shule na kila awamu ikipiga kifua inavyopenda kuendeleza elimu, mchafuzi anawezaje kusema kwamba shule zetu zinakosa madawati kiasi hicho?

Na hakuishia hapa. Wakati tunafurahia kusema kwamba walimu wamejaa kiasi kwamba tunaweza kuwahamisha wengine shule za msingi, mchafuzi anasema kuna upungufu wa nyumba za walimu kwa asilimia 88. Bila nyumba, bila mahali pa kuishi, mwalimu atajiandaa vipi kufundisha, atafundishaje vizuri na atatuliaje na kusahihisha madaftari lukuki ya wanafunzi wake?

Haya. Wakati tunalalamika juu ya tabia mbovu ya wasichana, na viherehere vyao wanapolazimishwa kupanga mitaani bila mpangilio, mchafuzi anatuambia kwamba kuna upungufu wa mabweni asilimia 88. Washambenga wataanza kusema kwamba bila shaka kuna mahusiano kati ya upungufu huo na mlipuko wa mimba za watoto wa shule. Upuuzi mtupu.

Halafu, nani atasahau jitihada ya awamu iliyopita pawe na maabara shuleni. Sasa Mchafuzi anatangaza kwamba, licha ya amri na shuruti zote zile, bado kuna upungufu wa maabara asilimia 84 Ni uongo nakuambia, uongo mtupu.

Hatimaye mchafuzi anatangaza kwamba kuna upungufu wa madarasa asilimia 52. Najua washambenga, wambea, mashilawadu, maYuda na wengine watalinganisha hali hii na matokeo mabaya ya shule za Serikali lakini mimi siamini. Siamini kweli kwamba hali hii inachangia kitu chochote. Ni uzushi wa kujenga chuki dhidi ya serikali yetu isiyolala katika kutafuta kuleta elimu. Ni uzushi tu wa kujaribu kukejeli jitihada za kuboresha na kuimarisha miundombinu za nchi yetu.

Haya na tunapokuja kwenye shule za msingi, huyu mchafuzi anazidi kutuchanganya. Angalau amekubali kwamba kutokana na kampeni murua ya awamu hii, upungufu wa madawati umeshuka hadi asilimia 14, lakini mengine, duh! Upungufu wa vyumba vya madarasa asilimia 85, nyumba za walimu asilimia 66, na matundu ya vyoo asilimia 83. Matundu ya vyoo! Yaani huyu mchafuzi anataka kutuambia kwamba, kwa miaka yote hii tumeshindwa hata kuchimba vyoo? Sisi tuliokuwa mstari wa mbele katika elimu ya kujitegemea? Hatuna majembe na sululu? Hatuna nguvu kazi? Kulikoni? Tunaambiwa kwamba hali hii si tu inaathiri afya ya watoto wetu shule, inasumbua hasa mabinti zetu wanapoanza kupevuka. Inazuia wasichana wengine hata wasifike shule siku kadhaa katika mwaka, kisha mchafuzi anataka kutuaminisha kwamba tunashindwa kuchimba matundu ya vyoo.

Nakuambia, bahati nzuri huyu mchafuzi hakuongelea pia suala la vitabu. Nisingependa kusikia kuhusu mabilioni yaliyotumika kutengeneza na kuteketeza vitabu vyote vile kutokana na makosa licha ya Serikali kujichukulia jukumu la kutunga vitabu wao wenyewe. Na asiguse kabisa maandalizi ya walimu, sifa zao, mipango ya kuwaendeleza na kadhalika. Yote hayo ni ya kuchafua tu.

Kinachoudhi kabisa ni kwamba miaka yote hii wanaharakati na mashilawadu wenzao wameimba kuhusu ubora, ubora, ubora wa elimu. Haina maana kumweka mtu ndani ya chumba na kusema anapata elimu iwapo elimu yenyewe ni finyu au haipo kabisa. Lakini, tumeweza kuwanyamazisha kwa kutaja idadi ya shule, na madarasa, na nyumba za walimu na mabweni, na madawati, na matundu ya vyoo tunayojenga. Kazi ya serikali ni kujenga, ubora baadaye.

Wanaharakati wasitusumbue. Sasa huyu mchafuzi ametoa nafasi kwa maadui wetu kusema kwamba hata kujenga ni janga pia. Hatuwezi kujisifia kwamba tumejenga hiki na kile wakati hiki ni kile ni kama tone la maji ndani ya Ziwa Tanganyika. Duh! Kwa kanuni za Wizara ya Mashule yenyewe, tunapaswa kufunga mashule kibao kwa kukosa sifa za kuitwa shule. Kumbe kanuni hizi ni kwa ajili ya shule binafsi tu!

Na bila shaka sasa wataamka wapumbavu wa kila aina na kusema:

‘Si tuliwaambia!’

‘Eti kuna haja ya kujiuliza kwa nini matokeo ya shule za serikali ni mabaya. Iwapo hakuna mazingira yanayofaa kusoma, tunategemea nini?’

‘Elimu ya watu wazima inahitajika upya maana tumerudi nyuma. Lakini sasa, badala ya kuwalenga wazee wasiopata nafasi ya kusoma mashuleni, inabidi kuwalenga vijana licha ya wao kupitia shule.’

Takwimu hizi ni mwiba mkubwa sana. Ndiyo maana naona, ili kuwanyamazisha wote hawa maadui, inabidi tutangaze hali ya dharura kabisa ili bajeti itoe kipaumbelembele kwa elimu kurekebisha hali hii na kuziba mdomo wa mchafuzi na washambenga wanaotaka kutumia kazi yake kuhalalisha kutudhalilisha. Ushilawadu mtupu!