In Summary
  • Wasichana wanaopata ujauzito katika wilaya hii wanajikuta njia panda. Shuleni hawatakiwi, wazazi wanawasusa. Lakini hata wanaowapa mimba nao hawawapi matunzo.

Kuna dalili za mateso ya maisha katika chumba hiki finyu cha udongo kilichomezwa na giza. Kuna mafiga sufuria na mwiko ambavyo havionyeshi uhai wa kutumika usiku wa jana.

Pembe ya pili kuna mfuko wa plasitiki uliobeba nguo na karibu yake mkeka uliokunjwa ambao kwenye usiku wa giza hutandikwa juu ya nyasi.Hiki ndicho kitanda na godoro.

Mtoto Shedrack anapata hofu na kuanza kulia, mama yake anamkumbatia na kudondosha chozi.Kwa kuwa wote ni watoto namtatafuta mwenyekiti wa kijiji ili awepo kama mlezi.

Haya ni makazi ya Semeni John (sio jina halisi)mwanafunzi aliyepata mimba akiwa darasa la saba mwaka 2017. Amekataliwa na mfumo rasmi wa elimu pamoja na jamaa na amepewa chumba hiki na raia mwema ajitegemee.

‘’Nimefukuzwa shuleni na nyumbani wakati nasoma nilifikiria mambo mengi baada ya masomo sasa naona ni kama hayawezekani tena nimepewa chumba hiki niishi na kujitegemea’’anasema Semeni

Anakumbuka anguko lilianza siku ya mahafali ya darasa la saba mwishoni mwa mwaka 2016.Anaamini halikuwa kosa lake pamoja na kuwa tayari amehukumiwa.

‘’Natamani kurudi tena shuleni nilitaka kuwa muuguzi sikutimiziwa kila kitu nilichoomba nisingeweza kuvumilia nilikuwa nachapwa viboko kwa kukosa mahitaji ya shule’’anajuta Semeni ambaye wazazi wake wametengana

Anasema mitihani imeongezeka baada ya kuanza kuishi katika chumba hiki.Baada ya kuuza debe la mahindi ameanzisha mradi wa kupika chai ya tangawizi na wateja wake ni wanaume wenye familia.

Hali hiyo imemjengea uhasama na baadhi ya wanawake. Ametengwa na kupewa taswira ya binti anayehatarisha ndoa zao. Anasema ni maneno yanayochoma na kumkatisha tamaa.

Semeni (17) ni miongoni mwa mamia ya wanafunzi wanaopata mimba na kuachwa wapotee kwenye mazingira hatarishi zaidi, baada ya kukosekana sera rafiki za kuwalinda ili waendelea na masomo.

Hakumbuki kuwahi kupata elimu ya kupambana na changamoto za makuzi na hatua za kuchukua na hakujua kama anaweza kuadhibiwa kiasi hiki.

Ngazi ya darasa la sita alipoishia, hakuwahi kufundishwa hatari ya mtoto wa umri wake kubeba mimba na kuonywa juu ya uwezekano wa kupoteza maisha.

Kauli yake kuwa wanaume wote ni hatari inaonyesha chuki ambapo mtaalamu wa Saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam Ignatia Mbatta, anasema ni kauli ya mtoto mwenye hisia za maumivu aliyejeruhiwa na uhusiano usiofaa kabla ya wakati.

Badala ya kutelekezwa anasema asaidiwe kwani hawezi kuhimili mazito anayopitia, ikilinganishwa na umri wake mdogo na hivyo kustahili huduma ya kisaikolojia.

Kauli ya wazazi

Baada ya kufukuzwa kwa wazazi, ni mama yake pekee Leticia Francis, amefika katika chumba hiki kumfariji kutokana na hisia za uchungu wa mwana.

Anasema ilikuwa vigumu kukaa naye sehemu anayoishi sasa na hakuwa na chaguo mbadala zaidi ya kumuacha Semeni akajitegemee.

Baba yake John Mutasa anasema hajui mwanaye alipo wala kuwasiliana naye huku akitaka mambo yote aulizwe mzazi mwenzake ambaye wametengana.

Safari ya shuleni

Shule ya Semeni iko kilometa tisa kutoka anapoishi sasa na takribani dakika 50 kwa mguu kufika kitongoji alipokuwa akiishi na wazazi.

Mwalimu mkuu Anna Kingu, anasema Semeni alikuwa mwanafunzi wa shule hiyo na alipata mimba baada ya kumaliza shule.

‘’Alisoma na kumaliza. Asiitie doa shule yetu, alipata mimba baada ya kuondoka tunafanya upimaji kila baada ya miezi mitatu mwenye ujauzito lazima atagundulika’’anasema Kingu

Hata hivyo, hakuna kumbukumbu zinazoonyesha kuwa alifanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba. Semeni anadai alifukuzwa shuleni tangu Machi 2017 baada ya kugundulika kuwa na hali hiyo.

Mwenyekiti wa kijiji, Adonia Simoni anasema tatizo la Semeni kupata mimba linafahamika na hawakuchukua hatua kwani halikuletwa kama tatizo.

Ujauzito Missenyi

Tatizo la watoto wanaopata mimba chini ya umri katika wilaya hiyo linaongezeka kila mwaka.Mathalani idadi ilifikia 131 mwaka 2015 na kupanda hadi 191 mwaka 2016.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk Khamis Abdalah kwa mwaka 2017 kati ya wazazi 5,959 waliosajiliwa, 211 ni wazazi wenye umri chini ya miaka 17 na kuwa hakuna kifo kilichotokea.

Dawati la Ustawi wa Jamii limejaa manung’uniko ya wanafunzi wenye ujauzito na watoto mgongoni. Hata shauri la Semeni liko hapa na halikupata ufumbuzi kwa madai ya mtuhumiwa kukimbia.

Ofisa Ustawi wa Jamii, Anold Nkongoki anasema kwa wastani watoto wawili wenye mimba hufika kila mwezi kuomba msaada na mwaka 2017 wanafunzi wanane wameunganishwa tena na familia zao. Wako kwenye hatari ya maambukizi ya Ukimwi.Kwa mujibu wa Nkongoki vijana 33,636 wa miaka 10-24 waliopima mwaka 2016, kati yao 386 walikutwa na maambukizi. Mwaka 2017 vijana 286 waligundulika kuwa na maambukizi kati ya 23,902 waliopima.

‘’Wanafika kuomba msaada baada ya kupewa mimba, wengine wanaolewa na kuachika kutokana na umri wao mdogo. Watoto nane waliofukuzwa tumefanikiwa kuwaunganisha tena na familia zao’’anasema Nkongoki

Tatizo la Semeni kupewa mimba lipo kwenye dawati la jinsia na watoto la Polisi Wilaya ambapo msimamizi wake Rashid Ramadhani, anasema hakuna kesi inayoendelea kwani mtuhumiwa alikimbia.

Anasema kesi 22 kati ya 34 tangu 2017 upelelezi wake umekamilika na watuhumiwa kufikishwa mahakamani, huku changamoto ikiwa watuhumiwa kufanya mapatano na wazazi na hivyo kudhoofisha ushahidi.

Nguvu ya watuhumiwa

Wanafunzi wanaopata mimba wanafukuzwa shuleni, huku watuhumiwa wakipata dhamana mahakamani na kufanya ushiwishi wa kuharibu ushahidi.

Mathalani katika kesi namba 79/2016 mwanafunzi kutoka Wilaya ya Missenyi alieleza mahakama jinsi mtuhumiwa alivyompa Sh10,000 ili asifike kutoa ushahidi.

Hukumu iliyosomwa tarehe Juni 15 mwaka 2017 katika mahakama ya wilaya ya Bukoba, ilimtia hatiani Stephene Michael aliyefungwa miaka 30 na adhabu ya viboko 12 kwa kosa la ubakaji.

Wakili kutoka Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkoa wa Kagera,Chema Maswi anasema katika kesi za mimba mashahidi wa msingi hurubuniwa na watuhumiwa.

Anasema mwanafunzi aliyebakwa ndiye shahidi wa msingi na kuwa wazazi hudhani wajibu wao ni kutoa taarifa polisi na sio kutoa ushahidi.

Mikakati ya Wilaya

Kutokana na ukubwa wa tatizo la wanafunzi kupewa mimba katika shule za msingi na sekondari, Serikali ya Wilaya imeimarisha mikakati ya kupambana na hali hiyo.

Mkuu wa Wilaya hiyo Kanali Denis Mwila anasema juhudi za kuwasaka watuhumiwa zinafanyika huku kampeni ya kutoa elimu shuleni ikiendelea kwa kushirikiana na wadau.

Anasema ukosefu wa mahakama ya wilaya ni tatizo kwa kuwa kesi huendeshwa Bukoba mjini na kuwa suala hilo tayari limefikishwa kwenye mamlaka husika.