In Summary
  • Hata hivyo, siyo dhambi kwa jamii hiyo kujifunza vitu na mambo mengine mazuri kutoka kwa jamii nyingine.

Jamii husika hutengeneza mfumo wa malezi na makuzi kwa watoto na vijana kutokana na historia yake.

Hata hivyo, siyo dhambi kwa jamii hiyo kujifunza vitu na mambo mengine mazuri kutoka kwa jamii nyingine.

Kwa mfano, kupitia mfumo wa maisha ya utandawazi, jamii nyingi zimejikuta zikishindwa kudhibiti baadhi ya mifumo yao ya maisha waliyoishi vizazi vyao viwili (au kimoja) vilivyopita.

Hujikuta zikikibadili baadhi ya misimamo ambayo hapo awali haikuwezekana kufanyika lakini kupitia utandawazi imewezekana.

Awamu ya tano ya mfumo wa utawala nchini imekuwa na msisitizo mkubwa wa kujenga uchumi wa kati.

Msisitizo huo umelenga katika kuanzisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vya uzalishaji wa bidhaa katika ubora unaotakiwa.

Viwanda hivi vingi havina budi vitokane na kazi za mikono za kiufundi kama vile ususi, uchoraji, uashi, uchomeaji na uyeyushaji wa malighafi za asili ya chuma. Pia, usindikaji wa malighafi za kilimo na ufugaji kama vile matunda, mbogamboga, nafaka, maziwa, nyama na mayai.

Wataalamu wa elimu wamekuwa na mijadala mbalimbali kuhusu ni kwa kiwango gani mifumo yetu ya elimu rasmi inavyoweza kuchangia malengo hayo. Wamekuwa wakiangalia uwezo wa wasomi wetu wanaozalishwa, ni kwa kiwango gani wana uwezo wa kufanikisha hili.

Pia, wataalamu wa saikolojia ya jamii, nao wamejaribu kutazama ni kwa kiwango gani malezi na makuzi yetu yamekuwa yakitoa fursa ya kubaini vipaji vya ubunifu na kuvikuza.

Makundi yote hayo yana lengo moja la kuhakikisha yanatoa mchango wao katika kukuza uchumi na hali za maisha ya wananchi kiuchumi, kimaadili, kisiasa na kitamaduni.

Uwekezaji kwa watoto

Makala haya yanachambua namna ambavyo ni muhimu kuwekeza katika kutoa fursa za watoto na vijana ili kukuza stadi na umahiri katika ubunifu na vipaji.

Zipo sababu za kibailojia, kimazingira na mifumo ya tamaduni za kijamii inayoathiri maendeleo ya watoto na vijana kufikia kujiamini na kuthubutu kufanya mambo makubwa.

Tuone vipindi vya makuzi na malezi vinavyoweza kusababisha tupate vijana na jamii yenye kuwa na ubunifu na uthubutu wa kujaribu mambo mapya:

Malezi katika kipindi cha kati ya miaka 3-6

Kipindi hiki ni muhimu kwa wazazi na walezi kuwapa fursa watoto kujiachia kucheza aina ya michezo mbalimbali.

Jukumu la wazazi liwe ni kuhakikisha usalama wa kimazingira na kuwawezesha katika vifaa vya kuchezea. Kipindi hiki huwajenga katika hali ya kuwa na malengo na uwajibikaji.

Katika kipindi hiki wazazi wasitake kwa kiasi kikubwa kusimamia sheria fulani fulani za kucheza.

Kwa mfano, watoto wanapotaka kuchukua baadhi ya vyombo vya ndani ili wakachezee, wazazi au walezi wawe tayari kuwaruhusu.

Wanapotaka kucheza katika mchanga au nje na watoto wenzao mtaani wawaruhusu pasipo kuhofia kuchafuka na wawaruhusu wacheze mpaka hamu zao za kucheza zinapoisha.

Watoto wana kawaida ya kujitengenezea ratiba zao za michezo ambazo wakati mwingine ni tofauti kabisa na ufikiri wa watu wazima. Hivyo, wanapojitungia michezo yao fulani, watu wazima wasiwaingilie, labda pale inapoonekana ni hatari au kuna maadili yanakiukwa.

Watoto wanapocheza katika mazingira ya shuleni au nyumbani wanakuza fikra na ndoto zao za maisha ya baadaye. Ndoto hizo zinapaswa kukuzwa. Huwawezesha kujenga picha ya ni kina nani wanataka wawe baadaye katika jamii yao na dunia kwa jumla.

Familia nyingi na jamii kwa ujumla zimekuwa haziwekezi katika vifaa na viwanja vya michezo ya watoto. Kweli ni gharama, lakini hatunabudi kufanya hivyo.

Malezi katika kipindi cha kati ya miaka 6- 11

Kipindi hiki watoto wengi wanakuwa tayari wako shuleni. Inafahamika kuwa shule ni wakala mkubwa wa mabadiliko. Kuwepo kwa sera ya elimu bure kumeongeza idadi ya watoto wanaoandikishwa katika ngazi ya elimu ya msingi.

Wajibu wa jamii uwe kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa. Lakini pia jamii isisahau kuwawezesha watoto hao katika mahitaji mengine muhimu shuleni kwa kushirikiana na uongozi wa shule.

Shuleni wanafunzi wapate fursa ya kushiriki michezo mbalimbali na kazi za sanaa na ubunifu. Tumeshuhudia idadi kubwa ya vijana wakitaka kushiriki katika shughuli na sanaa ya uigizaji, uchekeshaji, uongozaji wa sherehe na matukio, muziki na urembo. Ni vema pia mkazo ukawekwa katika shughuli zinazohusisha ufugaji, kilimo na elimu ya ujasiriamali.

Kipindi hiki cha malezi ni muhimu kwa makuzi ya mtoto, kwani ndicho ambacho hujifunza zaidi kutenda na kushirikiana na wengine.

Kama mtoto hakutendewa vizuri katika kipindi kilichopita, hukua akiwa amejenga hisia za uoga wa kushindwa kujaribu.

Hali hiyo isipogunduliwa na walimu, wazazi au walezi, huweza kusababisha kuwepo kwa baadhi ya vijana na watu katika jamii ambao hukosa ubunifu na kuthamini bidhaa kutoka nje ya jamii yao.

Hivyo basi, changamoto za kundi fulani katika jamii kuonekana kukosa macho ya kuona fursa na kuthubutu, zina mizizi katika mifumo yetu ya malezi na makuzi ya vijana.

Jamii inaposisitiza uanzishwaji wa viwanda mbalimbali, ni vyema sasa ikawekeza kwa jamii kuanzia utotoni ili kupata suluhu ya kudumu na isiyo na kipindi kifupi.

Msisitizo mkubwa uwekwe katika elimu ya sayansi na ufundi, sambamba na kutengwa kwa maeneo ya viwanja vya uwekezaji kwa vijana.