In Summary
  • Ukweli kuhusu rushwa kutamalaki katika maeneo mbalimbali nchini, ndio unaoilazimisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuwekeza elimu ya rushwa kwa wanafunzi ili kuwajengea uadilifu.

Wahenga walisema: ‘Samaki mkunje angali mbichi’. Usemi huu wenye maana katika malezi na makuzi ya watoto, ndio uliokuwa umetawala wakati wanafunzi wa shule za sekondari wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, walipokutana kujadili suala la rushwa.

Ukweli kuhusu rushwa kutamalaki katika maeneo mbalimbali nchini, ndio unaoilazimisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuwekeza elimu ya rushwa kwa wanafunzi ili kuwajengea uadilifu.

Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa Engera Kileo, akizungumza na wanafunzi wa vyuo vikuu katika ofisi za Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) hivi karibuni, alisema rushwa ya ngono ni kati ya vyanzo vikubwa vya maambukizi ya ukimwi nchini, na kwamba ili kupambana nayo ni lazima wanafunzi wapewe elimu.

Mkurugenzi wa Takukuru, Mkoa wa Pwani Suzan Raymond anasema hakuna namna Taifa linavyoweza kujenga kizazi kisichopenda rushwa bila kuwekeza elimu yake kwa wanafunzi.

Takukuru inaamini elimu ya rushwa shuleni ni nguzo ya msingi inayoweza kuwapika wanafunzi kuja kuwa raia wazalendo hapo baadaye.

“Rushwa zipo za aina nyingi, lakini mkakati huu tuliojiwekea kwamba kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu kuwa wanafunzi wapewe elimu ya rushwa, utasaidia kujenga taifa la watu wanaoweza kujitoa muhanga kupambana na rushwa,” anasema.

Meneja miradi wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenment), Nikodemus Eatlawe anasema elimu ya rushwa kwa wanafunzi ni muhimu.

“Elimu hii kwa wanafunzi ni muhimu kwa sababu itawasaidia wenyewe wasiwe tayari kufanya ngono ili iwe sababu ya kufaulu. Lakini pia watajengewa misingi mizuri na watakuwa na juhudu za kupata mafanikio endelevu,” anasema.

Eatlawe anasema madhara ya rushwa kwenye elimu ni pamoja na vyeti feki na uzalishaji wa wataalamu wasio na uwezo kitaaluma.

Hata hivyo, elimu ya rushwa kwa wanafunzi ina changamoto kwa kuwa ili wanafunzi waipate wanapaswa kujiunga kwenye klabu zilizopo shuleni kwa kupenda.

“Hakuna ulazima wa wanafunzi kujiunga kwenye klabu hizi au shule kukubali kuzianzisha, kwa hiyo si kila mwanafunzi anaweza kupata elimu ya rushwa,” anasema David Komba, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Lord Baen Powell.

Kutokuwepo kwa maswali katika mitihani ya kitaifa pia kunawafanya wanafunzi wasitilie maanani elimu dhidi ya rushwa.

Mwalimu wa shule ya Sekondari Efatha, Seif Peres anasema idadi ya wanafunzi waliojiunga na klabu za wapinga rushwa kupata elimu hiyo, bado ni kidogo kulingana na umuhimu wa jambo husika.

Anasema ili kulipa maana, lazima wanafunzi wote washiriki, ili kwa pamoja wapate uelewa dhidi ya rushwa.

Suzan anasema hicho ndio kikwazo kinacho zorotesha elimu hiyo kwa wanafunzi, kwa sababu wanajua hata kama watajikita kujifunza bado hakuna swali wanaloweza kukutana nalo kwenye mtihani.

“Niiombe wizara husika ione haja ya kuwa na mtalaa utakaohusu rushwa, ili kwa pamoja tuandae kizazi kinachochukia jambo hili kwa dhati kabisa,” anasema.

Agizo shule za Bagamoyo

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga anaamua kuagiza kila shule kwenye wilaya hiyo kuanzisha klabu ya wapinga rushwa.

“Kila mwaka nataka tuwe na kongamano litakalotoa mafunzo kwa wanafunzi wetu kuhusu rushwa, lakini huko shuleni kuwe na klabu za wapinga rushwa zilizo hai,” anasema.

Baadhi ya walimu wanasema ni changamoto kuendesha klabu za wapinga rushwa shuleni.

“Kuna wakati huwezi kuwapata wanafunzi kwenye klabu kwa sababu wanakuwa wametingwa na masomo ambayo wanaamini ndiyo muhimu kwa kuwa watakutana nayo katika mitihani,” anasema.

Anakiri kuwa ikiwa jambo hilo litaingizwa kwenye mtalaa, kila mwanafunzi atapata nafasi ya kujifunza na kuelewa kwa undani.

Baadhi ya wanafunzi wanasema wameshakutana na kesi za rushwa hasa wanapohitaji huduma za msingi.

“Nilishaona askari wa barabarani akipewa fedha nami nilikuwa kwenye gari karibu kabisa na dereva. Sijui kama aliyetoa na aliyepokea hawakujua kama ile ni rushwa? Nadhani kuna umuhimu mkubwa rushwa ikaingizwa kwenye mtalaa ili kujenga nchi ya wazalendo,” anasema David.

Mwanafunzi huyo ambaye alitumia zaidi ya dakika 20 kuwafundisha wenzake kuhusu rushwa, anasema kilichokosekana kwa wengi ni uelewa juu ya jambo lenyewe.

“Ukijua wazi hiyo ni haki yako una sababu gani ya kutoa rushwa? Ni vizuri watu wafundishwe hata namna ya kutoa raarifa za matukio husika; wengi ni waoga na wanaona bora alipe pesa ili mgonjwa wake atibiwe,” anasema.

Anasema rushwa inaweza kuwa kikwazo kikubwa cha kufikia Tanzania ya viwanda, kama hakutakuwa na jitihada za kupambana nayo kwa nguvu zote.

Mafanikio ya elimu kwa wanafunzi

Suzana anasema zipo kesi nyingi za rushwa zilizoripotiwa na wanafunzi ambao tayari wamepewa elimu dhidi ya suala hilo.

“Wanafunzi wanaokutana na vizingiti vya rushwa wamekuwa wakiripoti; wengine kesi zao zinaendelea na wengine zimehukumiwa, kwa hiyo faida ya jambo hili ni kubwa mno,” anasema.

Anasema kiuhalisia wanafunzi waliojiunga kwenye klabu hizo wamejua umuhimu na wapo mstari wa mbele kupambana na rushwa.

Mwanafunzi wa shule ya Sekondari ya Baobab, Pauline David anasema kamwe hawezi kukubali mtu atoe rushwa mbele yake.

“Siwezi kukubali kabisa mtu anidai rushwa au atoe rushwa mbele yangu. Naijua namba ya kupiga na najua namna ya kuwasiliana na Takukuru juu ya hili,” anasema.