Kwa kizazi cha sasa, unapotaja jina la Chama hisia zitakwenda kwa mchezaji wa kiungo wa kimataifa wa Simba, Clatous Chama.

Lakini kwa mashabiki wa soka kati ya mwaka 1977 hadi 1991, jina hilo linawakumbusha mabeki wawili shupavu waliowahi kuwika katika kikosi cha Yanga na Taifa Stars.

Rashid Idd ‘Chama’ na Athumani Juma ‘Chama’ ni wachezaji wawili tofauti, lakini wote wamewahi kucheza Pamba na Yanga katika nafasi ya ulinzi.

Wachezaji wote wawili walibatizwa jina la utani la Chama wakifananishwa na beki nyota wa zamani wa Zambia, Dick Chama aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kucheza nafasi ya ulinzi.

Katika makala haya, tunamzungumzia Rashid Idd ‘Chama’ mmoja wa mabeki wa Yanga aliyekuwa na uwezo wa kucheza nafasi zote za ulinzi.

Chama aliyecheza kwa mafanikio kwa takribani miaka 11 katika kikosi cha Yanga, anaanza na simulizi ya timu ya Taifa, kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa Huru ya Afrika ni mafanikio makubwa katika historia ya soka nchini.

Anasema baada ya kupita miaka 39, hatimaye Tanzania itacheza tena fainali hizo zilizopangwa kuanza Juni hadi Julai nchini Misri na ambazo sasa zinajulikana kama Fainali za Mataifa ya Afrika baada ya bara zima kukamilisha harakati za ukombozi kutoka ukoloni.

Taifa Stars iliweka historia hiyo ilipoifunga Uganda ‘The Cranes’ mabao 3-0 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Matokeo hayo yaliiwezesha Tanzania kushika nafasi ya pili katika Kundi L ikiwa na pointi tisa, nyuma ya Uganda ambayo ilishafuzu baada ya kukusanya pointi 10 katika mechi zake tano za awali.

Cape Verde na Lesotho, zilizokuwa kwenye kundi hilo, hazikufuzu.

Nguli huyo ni miongoni mwa wachezaji wakongwe waliotoa hamasa kwa timu hiyo baada ya kuitwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) akiungana na nyota wengine walioipeleka Tanzania katika fainali hizo mwaka 1980.

“Wachezaji wetu ni wazuri wana nafasi ya kushinda mechi na Uganda na kufuzu fainali hizi,” alisikika Chama ambaye pia amewahi kucheza Pan African na Majimaji ya Songea akitoa hamasa kwa wachezaji muda mfupi kabla ya mchezo huo.

Mbali na Chama nyota wengine waliojitokeza kwenye mazoezi ya Taifa Stars ni pamoja na Hussein Ngulungu, Idd Pazi na Omari Hussein ambao kila mmoja alitoa kauli ya kuwatia moyo wachezaji wa Taifa Stars.

Akizungumza na mwandishi wa Mwananchi katika mahojiano maalum, Chama anaanza kwa kueleza safari yake ya soka tangu akiwa kinda mwaka 1971 alipokuwa mchezaji wa timu ya watoto ya Yanga.

“Nilianza Yanga Kids hadi mwaka 1977 nilipandishwa kikosi cha wakubwa na mwaka mmoja baadaye kulitokea mpasuko wengi walijiunga na Mseto ya Morogoro na Pan African mimi nilibaki.

“Nakumbuka wazazi wangu walinitaka niache kucheza mpira walitaka niendelee kusoma, lakini baadaye waliniruhusu. Baadaye nilijiunga na Pan African kabla ya kurudi Yanga,” anasema Chama.

Nini kilitokea baada ya Chama kurejea Yanga na kukutana na idadi kubwa ya nyota waliounda ngome imara katika kikosi hicho, fuatilia makala haya wiki ijayo.