In Summary

  • Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema dhamana kwa watuhumiwa wanaokamatwa katika inapaswa kutolewa saa 24 na siku zote za wiki bila visingizio vya kwamba wikendi hawatoa dhamana.

Nimefarijika sana nilipomsikia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akikemea utaratibu mbaya polisi kuwanyima dhamana watuhumiwa siku za mapumziko kwa kisingizio kwamba sio siku za kazi.

Nathubutu kusema katika mambo ambayo ni kero ndani ya vituo vya polisi ni kukatalia dhamana kwa makosa yenye dhamana, na baadhi ya maofisa wa polisi hugeuza suala hili kuwa mradi wa kujiingizia pesa.

Ni kutokana na utaratibu huo ambao unakwenda kinyume na mwenendo mwema wa Jeshi la Polisi, ndio maana hata raia wakaja na usemi maarufu kuwa “Kuingia Polisi ni bure ila kutoka ni pesa”.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Busanza wilayani Uvinza Septemba 30, 2018, Lugola alisema dhamana inapaswa kutolewa saa 24 na siku zote za wiki bila visingizio.

“Hii tabia sijui imetoka wapi na imejengeka kwa baadhi ya polisi. Eti mtu akiingia mahabusu siku ya Ijumaa ikifika Jumamosi na Jumapili hawatoi dhamana wakisema mpaka Jumatatu,” alisema Lugola.

Waziri Lugola alihoji tabia hiyo iliyojengeka kwa baadhi ya askari imetokea wapi na kutaka tabia hiyo ife mara moja na kusisitiza kuwa kwa makosa yale yanayodhaminika, watuhumiwa wadhaminiwe.

Kuna makosa hayana dhamana kisheria kama makosa ya mauaji, wizi wa kutumia silaha, usafirishaji dawa za kulevya, uhaini, utakatishaji wa fedha, lakini si tuhuma za kugombana baa au mtaani.

Si hivyo tu, kuna baadhi ya watu hula njama na polisi ili kumweka mahabusu mtu ambaye walikopeshana naye fedha na akashindwa kulipa, kama njia ya kumkomoa au kumshinikiza alipe.

Kuna majalada mengine hufunguliwa polisi lakini yanaangukia kwenye kesi za madai. Mtu anabambikiwa kesi ya wizi wa kuaminiwa badala ya madai, mpaka unajiuliza hao wanaoyapokea na kuyafungua walipitia vyuo gani?

Ndio maana nimetangulia kusema nimefarijika na maagizo haya ya Lugola, maana kuna michezo michafu hufanywa na baadhi ya maofisa wa polisi katika suala la utoaji wa dhamana.

Lakini Lugola kwa vile alikuwa ni ofisa wa Polisi, anapaswa kulisafisha jeshi hilo la Polisi na si tu kwenye upande wa dhamana, yapo mapungufu mengi anayotakiwa kuyafanyia kazi.

Nakumbuka kwenye miaka ya 2000 hivi, rafiki yangu alikuwa na jambo lake katika kituo kimoja cha polisi akaniomba nimsindikize ili akafungue shauri lake.

Tulifika na tukapokelewa vizuri, tukafungua jalada na kupewa RB namba, wakatuuliza kama tuna usafiri wa kwenda kumkamata mtuhumiwa, tukawaambia tutakodi teksi. Kweli tukaikodi.

Tuliondoka na polisi wawili hadi eneo alipokuwa mtuhumiwa na kufanikiwa kumkamata, wakamfikisha polisi na tulipotaka kuondoka wale polisi wakauliza mnatuachaje?

Nikawauliza kwani vipi, wakasema sisi ndio “tuliowafungulia duka” siku hiyo kwa hiyo tunatakiwa tuwaangalie (tuwalipe), vinginevyo wangemwachia mtuhumiwa. Nilisikitika sana.

Tukiachana na matendo ya askari hao wasio na maadili, upo ukiukwaji mkubwa wa taratibu kuanzia ukamataji, kumweka mtu mahabusu, upelelezi na utunzaji vidhibiti.

Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002, imeelekeza hatua kwa hatua ni taratibu gani za kufuata, kuanzia ukamataji hadi kumfikisha mtuhumiwa kortini.

Mathalan, sheria hiyo inataka maelezo ya mtuhumiwa yachukuliwe si zaidi ya saa nne tangu kukamatwa kwa mtuhumiwa, lakini wapo watuhumiwa wanakaa hadi saa 48 hawajatoa maelezo yao.

Sheria inataka mtuhumiwa atoe maelezo yake ya onyo ya kukiri kosa kwa hiyari, lakini kuna madai mazito ya baadhi kuteswa, na hii ni sababu ya maelezo mengi kukataliwa mahakamani.

Ushahidi muhimu unapotea na wakati mwingine hata mtuhumiwa kupoteza maisha, ni lazima sasa Jeshi letu la polisi lirudi katika kufanya kazi kwa weledi, hili la Lugola liwe mwanzo wa kuelekea huko.

Binafsi ninaamini tuna sheria nzuri sana kuanzia CPA hadi PGO, na kama jeshi letu likifanya kazi kwa weledi, bila upendeleo wala ubaguzi, hakika linaweza kuwa Jeshi bora zaidi ukanda wa Afrika.