In Summary
  • Mwakilishi wa Chaani, Nadri Abdul-latif Jussa ni miongoni mwa walioonekana kukerwa na lugha hizo na juzi wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa mwaka 2018/19, alibainisha kuwa viongozi hao wamekuwa wakiihusisha Zanzibar na ukwepaji kodi pamoja na kupitisha bidhaa za magendo, jambo alilodai si kweli.

Katika toleo la jana la gazeti hili kulikuwa na habari iliyowanukuu wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakilalamikia kitendo cha baadhi ya mawaziri na wabunge wa Tanzania Bara kutoa lugha za kuudhi kuhusu Zanzibar, wakisema ni dharau kwa wananchi wa visiwa hivyo.

Mwakilishi wa Chaani, Nadri Abdul-latif Jussa ni miongoni mwa walioonekana kukerwa na lugha hizo na juzi wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa mwaka 2018/19, alibainisha kuwa viongozi hao wamekuwa wakiihusisha Zanzibar na ukwepaji kodi pamoja na kupitisha bidhaa za magendo, jambo alilodai si kweli.

Lakini, mwakilishi wa Tunguu, Simai Mohamed Said alikwenda mbali kwa kumshauri Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi kuwashughulikia viongozi wa aina hiyo.

Kama hiyo haitoshi, mwakilishi wa Mfenesini, Machano Othman Said aliamua kupasua jipu kwa kueleza kuwa ili kila upande uheshimiane ni vyema kero za Muungano zikatatuliwa haraka.

Hoja ya Machano ndiyo imegusa msingi wa tatizo ambao ni kero za Muungano. Mwezi uliopita Watanzania waliadhimisha miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar huku kukiendelea kuwepo baadhi ya kero zinazotajwa mara kwa mara za Muungano.

Kuna kero zinazohusu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Muungano wa Tanzania kuhusu namna ya kugawana mapato na kuchangia gharama za Muungano. Pia kuna malalamiko ya baadhi ya bidhaa zinazotengenezwa Zanzibar kunyimwa fursa ya soko la Bara.

Wazanzibari wanalalamika na Watanzania Bara nao wanalalamika. Lakini pengine tatizo lipo kwenye kauli za kisiasa zinazotolewa na viongozi mbalimbali. Wako wanaosema kero za Muungano zimetatuliwa kwa kiasi kikubwa, lakini wapo pia wanaodai bado zipo na zinaendelea kuwapo.

Wakati wa maadhimisho ya miaka 54 ya Muungano, mwanasiasa mkongwe na mbunge mstaafu, William Shellukindo alijitokeza hadharani kueleza masikitiko yake kwamba mapendekezo ya Tume ya Shellukindo iliyokuwa ikishughulikia vikwazo vya Muungano, hayajafanyiwa kazi kwa takriban miaka kumi.

Tume hiyo, iliyofanya kazi tangu awamu ya pili ya serikali hadi ya nne, ilikuwa ikishughulikia eneo la kugawana mapato na kuchangia gharama za Muungano na walifanya ziara za mafunzo katika nchi zaidi ya 13 duniani, lakini tangu wakabidhi ripoti yao kwa maoni yao hadi sasa hayajafanyiwa kazi.

Kwa msingi huo vijembe wanavyopigana wawakilishi ndani ya Baraza la Wawakilishi na wabunge kwenye Bunge la Jamhuri vinatukumbusha umuhimu wa kuweka siasa pembeni na kushughulikia kero zote na kwa haraka.

Mtazamo wetu hapa licha ya juhudi zote ambazo zimekuwa zikifanywa na serikali zote mbili kama kuanzishwa wizara inayohusika na Muungano, mambo bado hayajakaa sawa na hili linajidhihirisha kutokana na malalamiko ya mara kwa mara kutoka kila upande.

Tunadhani umefika muda kwa kila upande kuwa na utashi wa kisiasa. Kutoka hadharani na kueleza maneno mazuri wakati chini ya zulia kuna malalamiko mengi, hakutasaidia.

Ushauri wetu kwa serikali zote, ya Muungano na ile ya Mapinduzi Zanzibar, wayafanyie kazi mapendekezo yaliyotokana na tume walizoziunda, kila upande ukubali kupoteza na kupata. Kuendelea kuvutana ni kuzidi kuwavuruga wananchi, tunasisitiza kuwa Muungano ni muhimu kwa taifa letu.