In Summary
  • Kama hiyo haitoshi, Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage wamekutana na Waziri wa Biashara na Ushirika wa Uganda, Fredrick Ngobi Gume kujadili usafirishwaji huo wa kahawa unaodaiwa kuwa ni wa magendo.

Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa inayolima kahawa kwa muda mrefu. Hata hivyo, hivi karibuni soko la zao hilo limeingia utata na kuwafanya baadhi ya wakulima kuuza kahawa yao Uganda kwa kile wanachodai kuna bei nzuri ukilinganisha na masoko ya ndani. Hatua hiyo imeifanya Serikali kupiga marufuku wafanyabiashara wa kahawa kuisafirisha kwenda nchini Uganda na kuwalazimisha kuuzia kwenye vyama vya ushirika vinavyoipeleka kwenye mnada mkoani Kilimanjaro, jambo ambalo hata hivyo halijapokelewa vizuri na wakulima.

Kama hiyo haitoshi, Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage wamekutana na Waziri wa Biashara na Ushirika wa Uganda, Fredrick Ngobi Gume kujadili usafirishwaji huo wa kahawa unaodaiwa kuwa ni wa magendo.

Wakulima wanasemaje

Wakizungumzia sababu zinazowasukuma kuuza kahawa kwenye soko la Uganda, Gilbert Makwage ambaye ni mkulima wa kahawa katika manispaa ya Bukoba anasema bei ya Uganda ni kubwa ukilinganisha nay a nchini.

“Hapa Bukoba, tumekuwa tukiuza kahawa kwa Sh1,000 kwa kilo, wakati gharama za uzalishaji ni kubwa kuliko hiyo bei. Mkulima anapata tabu kutunza mikahawa pamoja na kununua dawa za kupuliza na kukatia maotea, wakati Uganda tunauza kilo moja Sh2,000 ya Tanzania.” Anasema wakati mwingine wanawauzia kahawa hiyo ikiwa bado shambani na wafanyabiashara wa Uganda hununua kabla hata ya kukoboa wakilenga kupata maganda kwa ajili ya shu huli nyingine.

“Wakichukua zenye maganda wanakuwa na faida mara mbili. Kwanza wanachukua kahawa, lakini pia wanatumia maganda yale kama mbolea kwenye mashamba yao au wakiyakausha wanatumia kuchomea matofali,” anasema Makwage. Anataja sababu nyingine ya wakulima kukimbilia soko la Uganda, wengi wana mashamba madogo hivyo wanataka kupata faida ya haraka kuliko kufuata mchakato mzima wa uuzwaji wa kahawa kupitia vyama vya ushirika.

“Ukichukua tangu kazi ya palizi, kukatia machipukizi, kupiga dawa, kuweka mbolea, halafu tena unakuja kwenye mchakato wa kuuza kwenye vyama vya ushirika hadi uje ulipwe, inachukua muda mrefu. Ndiyo maana wengi wanapeleka Uganda baada yua kuvuna,” anasema.

Hata hivyo, anasema amekuwa akiuzia kahawa yake kwenye vyama vya ushirika na ameshauri bei angalau iwe Sh1,800 kwa kilo badala ya bei ya sasa ina maumivu.

Malalamiko kama hayo pia yametolewa na Sabi Rwazo mkulima wa kahawa wa wilayani Karagwe.

“Tatizo lililopo ni utaratibu wa malipo, bado haujakaa vizuri. Mtu anauza kahawa yake anakaa siku mbili hadi wiki mbili hajalipwa chochote” anasema Rwazo.

Mkulima huyo anasema Serikali imeweka bei elekezi ya Sh1,400 lakini bado haijarasimishwa. “Waziri wa Kilimo alikuja hapa akatangaza bei ya elekezi kwa kilo moja ya kahawa ni Sh1,400, lakini haikuwa kwenye maandishi, matokeo yake wakulima wakienda kuuza wanasumbuliwa. Ukienda Uganda hawacheleweshi. Na sasa ndiyo msimu wa uuzwaji wa kahawa, wakichelewesha hadi Oktoba, Brazil nayo inaingiza kahawa yao kwenye soko la dunia, kwa hiyo kahawa yetu itakataliwa,” anabainisha mkulima huyo.

Akizungumzia malalamiko ya wakulima, Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Kagera (KCU), Onesmo Niyegila amekiri kuwapo kwa historia mbaya ya vyama vya ushirika iliyopoteza imani kwa wakulima.

“Tatizo zamani miaka 10 hadi 20 iliyopita, hakukuwa na uwazi katika uendeshaji wa vyama vya ushirika. Kuna malipo ya awali walitakiwa walipwe, lakini hawakulipwa. Ndiyo maana wakulima wengi wamekata tamaa,” anasema Niyegila. Hata hivyo, amekanusha kuwawekea bei ndogo wakulima akisema iliyowekwa inaendana na soko la dunia. Ametetea utaratibu unaotumiwa na vyama vya ushirika kuwa umethibitishwa na vyombo vya viwango.

“Kwenye vyama vya ushirika tunatumia mizani zilizohakikiwa na Wakala wa Vipimo, lakini kule Uganda wanakwenda kuuza kwa madumu, wanapunjwa. Isitoshe, wao wanakuja huku kujifunza jinsi ya kuendesha ushirika,” anasema Niyegila. Anasema hata bei ya Sh1,400 iliwekwa na mawaziri baada ya kuangalia mwenendo wa bei ya soko la dunia huku akisema bei ya kahawa isiyotumia dawa (organic) ikiwa Sh3,500.

Bei ya kahawa

Bei ya kahawa katika soko la dunia hutegemea uzalishaji hasa wazalishaji wakubwa ambao ni nchi za Brazil na Colombia. Uchunguzi wa Mwananchi umeonyesha bei ya kahawa katika masoko ya dunia ikitofautiana na muda uliorekodiwa. Kwa mfano katika mtandao wa Market Business Insider hadi Julai, kahawa iliuzwa Dola 2.8 sawa na Sh6383.16, huku mtandao wa Ycharts ukionyesha bei ya kahawa aina ya Arabica kuwa Dola 2.99 sawa na Sh 6816.303 kwa rekodi ya Mei, 2018. Katika tovuti ya International Coffee Organization, bei ya kahawa hadi Julai mwaka huu, inatajwa kwa Dola 134.07 (high season) sawa na Dola 2.2345 kwa kilo na 127.99 kwa gunia la kilo 60 (low season) sawa na Dola 2.13 kwa kilo. Kwa mujibu wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Tanzania huzalisha wastani wa tani 50,000 za kahawa kwa mwaka. Hata hivyo, kuna mpango wa kuzalisha tani 80,000 kuanzia mwaka 2016 na kufikisha tani 100,000 ifikapo mwaka 2021.

Kauli ya Waziri

Akizungumza na wadau wa zao hilo nchini Julai 10 kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Isingiro wilayani Kyerwa, Waziri wa Kilimo Dk Charles Tizeba alikemea biashara ya kuuza kahawa nje ya nchi kwa magendo.

Taarifa iliyotolewa na ofisa habari wa Wizara ya Kilimo, Mathias Canal ilisema agizo hilo lilihusisha pia zuio la wananchi kuuza kahawa mbichi ambayo bado iko shambani na haijakomaa (Butura).

Ilisema kufanya hivyo ni kudhoofisha na kuzorotesha juhudi za muda mrefu alizotumia mkulima wa kahawa na kumkosesha mapato stahiki.

Akiwa katika eneo la Mutukula, Dk Tizeba aliwashauri wakulima kutokimbilia bei kubwa nchini Uganda akisema siyo ya kweli.

“Kuna jambo hamlifahamu kuhusu bei ya kahawa huko Uganda. Wanaosema bei ya kahawa ni nzuri kuliko Tanzania wanawadanganya. Hakuna bei nzuri kule kinachofanya watu kupeleka kahawa Uganda ni kutokana na mikopo wanayokopeshana isiyo rasmi (Butura).

“Hivyo makubaliano ya kurejesha mkopo yanakuwa na masharti magumu yanayowataka wakulima wa kahawa nchini kulipa madeni kwa kupeleka kahawa si fedha,” alisema DkTizeba.

Alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, Shadrack Mhagama kukamilisha haraka iwezekanavyo kiwanda cha kukoboa kahawa cha Omkagando kilichozinduliwa na Mwenge wa Uhuru tangu 2016 kwa gharama za Serikali, lakini mpaka sasa kimeshindwa kufanya kazi.

Dk Tizeba akizungumzia kuhusu bei hizo, alitoa mfano wa mnada wa kahawa uliofanyika Moshi mjini Julai 12, bei ya kahawa ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Kagera (KCU) iliuzwa kwa kilo moja ya maganda kwa wastani wa Sh1,460 ya bei elekezi ya chini inayotolewa na Bodi ya Kahawa kulingana na bei ya kahawa katika soko la Dunia.

“Wakulima wa Tanzania watapata Sh1,900 zaidi watakapouza kahawa mnadani moja kwa moja tofauti na shambani, kwasababu kwa kuuza mnadani, mkulima anapata bei kutokana na ubora wa kahawa yake na ikiwa kwenye madaraja,” anasema. Akizungumzia bei ya kahawa nchini Uganda, Waziri wa Biashara na Ushirika, Fredrick Ngobi Gume alimhakikishia mwenyeji wake kuwa biashara ya kahawa nchini humo ina changamoto sawa katika nchi zote mbili kwa kuwa suala la mikopo isiyo rasmi inayowanyonya wakulima (Butura). Anasema hali hiyo nchini Uganda ipo kwa kiwango cha juu kiasi kwamba aliomba kuja nchini kuanzia Julai 16 hadi 19 kwa ahadi maalumu ya kujifunza kuhusu namna bora ya kuendesha ushirika na kuanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani. Serikali inapaswa kuwasikiliza na kuwapa mwelekeo sahihi wakulima wa kahawa kusudi wawe na uhakika wa soko la zao hilo.