In Summary
  • Baadhi ya wakulima wanaeleza chanzo kuwa ni upepo wa kusi, huku wafanyabiashara wakisema ni baadhi ya wakulima kuficha nazi ili waziuze kwa bei ya juu wakati wa mfungo wa Ramadhani unaotarajia kuanza Mei 16 au 17 kulingana na mwandamo wa mwezi.

Serikali yashtuka, yawaonya watakaopandisha bei

Tanga. Wakati wakulima na wafanyabiashara ya nazi wakieleza kuadimika kwa bidhaa hizo mkoani hapa, mtaalamu wa kilimo ameeleza sababu za kutokea hali hiyo.

Baadhi ya wakulima wanaeleza chanzo kuwa ni upepo wa kusi, huku wafanyabiashara wakisema ni baadhi ya wakulima kuficha nazi ili waziuze kwa bei ya juu wakati wa mfungo wa Ramadhani unaotarajia kuanza Mei 16 au 17 kulingana na mwandamo wa mwezi.

Ofisa kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Ramadhan Zubeir aliliambia gazeti hili kuwa uvunaji nazi umeshuka kwa takriban asilimia 50 kutokana na chumvi ya bahari kuenea ardhini, hivyo kuathiri mimea ikiwamo minazi.

“Uvunaji umeshuka mno ni kwa zaidi ya asilimia 50, hata nazi zinazotegemewa ni kutoka Bonde la Mauya lakini maeneo mengine hali ni mbaya,” alisema.

Zubeir alisema sababu nyingine ni ongezeko la ukataji minazi kwa ajili ya mbao zinazotumika kuezekea nyumba na kutengenezea samani, kwa kuwa hazishambuliwi na wadudu.

Ofisa huyo alisema changamoto nyingine ni minazi mingi iliyopo ni mikongwe iliyopandwa miaka zaidi ya 50 iliyopita.

“Sababu wanazotoa za upepo wa kusi na kaskazi ni za mazoea siyo za kitaalamu, kwa kuwa uzaaji wa nazi hutokana na maua yanayotokeza kila baada ya muda maalumu bila kuangalia ni wakati gani,” alisema Zubeir.

Mtaalamu huyo alisema uvunaji nazi wilayani Pangani umeshuka kutoka tani 34,600 mwaka 2012 kufikia tani 16,865.

Wasemavyo wananchi

“Nazi niliyoshika kwa kawaida nisingeinunua kwa sababu watu wa pwani aina hii tunaiita shorobero, yaani haifai kuungiwa lakini kwa sababu hakuna nazi nimelazimika kuinunua tena kwa Sh500,” alilalamika Mwanamkuu Khalid mkazi wa Barabara ya 10 jijini Tanga.

Naye mkazi wa Madina jijini hapa, Bakari Lunza alisema kuadimika kwa nazi kunawatia wasiwasi kwa sababu zitauzwa kwa bei ghali wakati wa Ramadhani.

Alisema nazi ambayo huuzwa Sh400 katika masoko ya jijini Tanga sasa inauzwa Sh1,000.

Hata hivyo, katibu tawala mkoani Tanga, Zena Said alisema Serikali haitawafumbia macho wafanyabiashara watakaopandisha bei bidhaa ikiwamo nazi wakati wa Ramadhani kwa visingizio mbalimbali.

Wauzaji wa nazi wa Soko Kuu la Ngamiani ambalo ni kituo kikubwa cha ununuzi na mauzo ya nazi, walieleza kuwa wamelazimika kupandisha bei kwa sababu zimeadimika.

Fadhili Ndalo (48), ambaye anafanya biashara ya nazi kwa zaidi ya miaka 15 sokoni hapo, alisema wachuuzi wanaopelekea bidhaa hiyo wamepandisha bei ya jumla kuanzia Sh600 hadi Sh800 kwa nazi kubwa, huku ndogo wakiuza Sh400.

Naye mfanyabiashara Suleyman Shaibu alisema soko hilo lina wachuuzi wapatao 40, lakini kutokana na kuadimika kwa nazi wiki moja sasa wenye bidhaa hiyo ni wafanyabiashara wachache.