In Summary
  • Onyesho hilo lililokuwa linasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa muziki wa dansi, lilifana kufuatia watu wengi kujitokeza, huku safu ya uimbaji na unenguaji ikinogesha tukio hilo.

 Onyesho maalumu la kumuaga aliyekuwa kiongozi na mwimbaji nguli katika bendi ya The African Stars 'Twanga Pepeta', Ally Choki limefanyika jana Aprili 28, 2018 katika Pub ya The Jonz iliyopo Magomeni Mwembe Chai jijini Dar es Salaam.

Onyesho hilo lililokuwa linasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa muziki wa dansi, lilifana kufuatia watu wengi kujitokeza, huku safu ya uimbaji na unenguaji ikinogesha tukio hilo.

Safu ya uimbaji iliongozwa na Luiza Mbutu akisaidiana na Diof, Kalala Junior, Haji Bss na Piano huku wanenguaji wakiwa Super Nyamwela, Hamza Mapande, Mandela, Maria Saloma, Stella Manyanya, Fasha na Chiku Kasika.

Akizungumza na MCL Digital, mkurugenzi wa bendi hiyo, Asha Baraka 'Iron Lady'  amesema onyesho  lilikuwa maalumu kumuaga Choki ikiwa ni sehemu ya kutambua  mchango wake mkubwa alioutoa kwa bendi.

"Nashukuru safari hii nimemaliza salama kufanya kazi na Choki, maana Choki toka aanze kufanya kazi katika bendi hii hajawahi kumaliza mkataba, mara nyingi huwa anaachia kati, sasa hivi anayejitahidi kamaliza miaka mitatu,” amesema.

Naye Choki ameiambia MCL Digital kuwa baada ya kumaliza mkataba huo, hana mpango wa kuanzisha bendi kama alivyoeleza awali, bali anapumzika na kuangalia familia yake huku akiwa anafanya kazi na bendi nyingine.

Choki amesema atakuwa anafanya kazi na Bendi ya The Mafiki huku muda mwingi akiutumia kuangalia familia.