In Summary
  • Waelezwa kuwa kushiriki katika tamasha hilo si lazima ushinde tuzo, bali kujifunza na kukutana na magwiji wa filamu kutoka maeneo mbalimbali duniani

Zanzibar. Tamasha la 21 la filamu za Zanzibar (ZIFF) linaendelea visiwani hapa katika viwanja vya Ngome Kongwe huku wasanii wa Bongo Movie wakionekana kwa nadra licha ya kuwa mara kadhaa kueleza kutaka kukuza soko lao la filamu.

MCL Digital imepiga kambi katika tamasha hilo na takribani siku tatu limewashuhudia wasanii wachache wa Bongo Movie ambao ni Mzee Chilo, Gabo, Natasha na Claud 112.

Mbali na wasanii hao, hata Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Saimon Mwakifamba naye haonekani katika tamasha hilo.

Baadhi ya wadau wa filamu waliozungumza na MCL Digital leo Jumatatu Julai 9, 2018 wamesema hali hiyo inaleta simanzi kwa kuwa wasanii hao wangeweza kutumia tamasha hilo kujitangaza kazi zao kutengeneza mtandao mpana.

“Wapo watengeneza filamu wengi wamekuja hapa tena wengi hata hawajaalikwa, nia ni kukuza mtandao wa mawasiliano na kuona fursa za soko,” amesema meneja wa tamasha hilo, Daniel Nyalusi.

Amesema wapo baadhi ya waliohudhuria wanatoka Haiti kwa ajili ya kusaka soko la filamu, sambamba na kuona wanayoyafanya wenzao.

“Wasanii na watengeneza filamu wa Kenya wamejitokeza kwa wingi na kazi zao wanatumia ZIFF kama sehemu ya kujitangaza,” amesema.

Akizungumzia kutoonekana kwa wasanii wa Bongo Movie katika tamasha hilo mkurugenzi wa ZIFF,  Frabrizio Colombo amesema, “Tatizo kubwa hapa ni kwa wasanii wetu wengi wao wanasubiri sisi waandaaji tuwaombe waje kushiriki katika tamasha hili baada ya wao waje kuomba ama kuja kujifunza.”

“Ninawalaumu kwa kuwa hawalichukulii tamasha hili kwa uzito. Kama wangekuwepo labda wangeweza kupata elimu na kubadilishana mawazo na magwiji mbalimbali waliofika.”

Akizungumzia hali hiyo Claud amesema wasanii wengi hawajaelewa fursa zinazopatikana katika tamasha hilo.

“Kushiriki ZIFF si lazima upate tuzo hilo si lengo. Lengo la kuja hapa ni kujifunza kwa kuwa kuna wageni wengi kutoka nchi tofauti,” amesema.