In Summary

Waziri awaonya watendaji wasio waadilifu kuwa vyombo vya dola vinawafuatilia kwa karibu

Zanzibar. Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Joseph Abdallah Meza amewataka washauri waelekezi wa kodi kuwa na uzalendo ili wafanyabiashara walipe kodi kwa hiari na wakati.

Meza alitoa kauli hiyo wakati akifungua mkutano wa siku moja kwa washauri hao, kikao ambacho kilifanyika juzi mjini Unguja.

Alisema kwamba Serikali imeweka mpango mkakati kuhakikisha ukusanyaji wa kodi unaimarika zaidi, ndiyo maana wakaanzisha utaratibu wa kuwapo kwa washauri hao hivyo ni vyema kufanya kazi ipasavyo ili kuimarisha makusanyo.

Alisema mara nyingi kumekuwepo tabia ya baadhi ya washauri wa kodi kukiuka utaratibu kwa kuwapotosha walipakodi sambamba na kuwashauri visivyo jambo ambalo limekuwa linapoteza mapato ya Serikali.

Meza aliwataka washauri hao kutoa elimu sahihi kwa walipakodi ili wajenge imani na Serikali sambamba na kuongeza walipakodi.

Kuhusu marekebisho ya sheria, Meza alisema ili yafanyike inategemea na mazingira yaliyopo kwa wakati huo.

Hata hivyo, Meza aliwataka kujiepusha na tabia ya kutengeneza sumu kwa walipa kodi kwa kuwa wengi ni wageni na kwamba, wanapodanganywa wanaambizana jambo ambalo husababisha taswira mbaya kwa nchi.

Pia, Meza alitumia nafasi hiyo kuwapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya kwani wamewasaidia walipa kodi namna ya kujua utaratibu.

Alisema nchi zote duniani zinaendeshwa kwa kodi hivyo kuwataka wananchi kuendelea kulipa kodi zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.

Washiriki wa mafunzo hayo, waliahidi kuendelea kufanya kazi na bodi hiyo sambamba na kuutaka uongozi wa ZRB kuwaangalia baadhi ya watendaji wao kwa kuwa wamekuwa na lugha isiyo rafiki kwa wateja wanapokwenda kupata huduma.

Pia, waliomba kupatiwa leseni za kazi kwa wakati ili waweze kuchangia uchumi na kuongeza kasi ya maendeleo.

Naye Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Khalid Salum Mohamed aliwataka watendaji wa bodi ya ZRB kuacha urasimu na udalali katika maeneo yao ya kazi badala yake, wahakikishe wanasimamia vyema majukumu waliyopangiwa ili kuvuka malengo ya ukusanyaji.

Awali, Dk Khalid akifungua kikao alisema katika bajeti ya mwaka huu wadau hao watambue wana wajibu wa kukusanya Sh485.4 bilioni kutoka vyanzo vyake, kwa sababu mapato hayo ndiyo msingi wa utekelezaji wa mipango ya kitaifa.

Dk Khalid alisema licha ya kuwa mwaka wa fedha 2017/18 bodi hiyo ilivuka malengo ya makusanyo, kisiwe chanzo cha watendaji kubweteka au kutumia mbinu za kusababisha kushuka kwa mapato.

Alionya kuwa Serikali ipo macho na vyombo vyake vinafuatilia mwenendo wa watendaji hao.

Alisema Zanzibar ina uwezo mkubwa wa kukusanya mapato zaidi iwapo watendaji watasimama katika uadilifu.