In Summary
  • Hayo yalisemwa na Balozi wa Uturuki nchini, Ali Davutoglu na kufafanua kuwa yanaruhusu ushindani wenye usawa sokoni jambo ambalo ni zuri.

Dar es Salaam. Serikali ya Uturuki imesema mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, ni mazuri na kuahidi kuendeleza diplomasia ya uchumi na Tanzania.

Hayo yalisemwa na Balozi wa Uturuki nchini, Ali Davutoglu na kufafanua kuwa yanaruhusu ushindani wenye usawa sokoni jambo ambalo ni zuri.

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa futari iliyoandaliwa na Shirika la Ndege la Uturuki (Turkish Airlines) kwa ajili ya wateja, mawakala wa tiketi, maofisa wa ubalozi na wadau wengine. “Unaweza kusikia watu wakisema wanaona mabadiliko ya mazingira ya biashara nchini, lakini mimi naona ndiyo sawa sasa kwani wafanyabiashara wengi wanalipa kodi stahiki jambo ambalo ni manufaa kiuchumi kwani sokoni kuna ushindani wenye usawa,” alisema.

Katika miaka 18 iliyopita, alisema biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki umeimarika na utaendelea kushamiri zaidi.

Naye meneja masoko wa Turkish Airlines, Taylan Saylam alisema mfungo wa Ramadhan ni wakati mahsusi kwa watu kukaa pamoja.