In Summary
  • Sampuli ikiwa imeharibika kuna vitu vilivyokuwa vinahitajika katika uchunguzi huwa havipatikani

Mbeya. Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, imesema bado kuna tatizo la uchukuaji na utunzaji wa sampuli zinazohitaji kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara. Imeeleza kuwa jambo hilo linatokana na watu wanaohusika na uchukuaji na uhifadhi wa sampuli hizo kutozingatia taratibu husika kutoka eneo la tukio, hivyo kusababisha mamlaka hiyo kushindwa kupata majibu sahihi ya uchunguzi.

Meneja wa mamlaka hiyo, Gaspar Gerald alisema hayo jana wakati akizungumzia mafunzo ya usimamizi wa sampuli za makosa ya jinai, sheria ya mkemia mkuu wa Serikali na kanuni zake kwa wadau ambao ni polisi, maofisa ustawi wa jamii na wauguzi wa hospitali wa kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini yaliyofanyikia jijini hapa.

Gerald alisema kuna baadhi ya sampuli zimepelekwa katika ofisi yake kufanyiwa uchunguzi lakini ilishindikana kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kutozingatiwa namna ya uchukuaji wa sampuli hizo eneo la tukio. “Utakuta sampuli haitoshi au imevurugika au imeharibika kabisa. Sasa sampuli ikiwa imeharibika kuna vitu vingine vilivyokuwa vinahitajika katika uchunguzi huo vilivyokusudiwa havipatikani,” alisema.

Mbali na hilo, alisema kuanzia Januari hadi Mei mwaka huu ofisi yake imelazimika kupeleka sampuli 100 jijini Dar es Salaam ili zifanyiwe uchunguzi kutokana na kukosekana kwa umeme mkubwa na wa uhakika kwani wanatumia umeme wa jenerata ambao hauwezi kusukuma mitambo mikubwa.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mafunzo hayo, alisema ofisi hiyo ni muhimu zaidi kuwasaidia wananchi na kwamba tatizo la umeme analifahamu na tayari alishaanza kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na ofisi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Mbeya.

Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi wa Kisayansi wa Makosa ya Jinai kutoka Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, William Nyamakomago alisema uwapo wa ofisi ya mkemia mkuu jijini hapa umelisaidia jeshi la polisi kutekeleza majukumu yake ya kiupelezi kwa muda mwafaka tofauti na awali.

Pia, Nyamakomago alisema kitendo cha ofisi ya mkemia mkuu wa Serikali kanda hiyo kuanzisha mpango wa kutoa mafunzo hayo utaimarisha ufanisi wa utendaji kazi utakaokuwa ukifuata taratibu na sheria muhimu za uchukuaji wa sampuli na vielelezo kutoka eneo la tukio.