In Summary
  • Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Ngenya Yusuph alisema ili kufanikisha hilo, ofisi yake inatoa elimu juu ya umuhimu wa wazalishaji wa bidhaa au wanaoziingiza nchini kuwa na nembo ya ubora.

Arusha. Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limetoa miezi mitatu kwa wazalishaji wa bidhaa kuhakikisha wanajisajili bidhaa zao ili kupata nembo ya ubora.

Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Ngenya Yusuph alisema ili kufanikisha hilo, ofisi yake inatoa elimu juu ya umuhimu wa wazalishaji wa bidhaa au wanaoziingiza nchini kuwa na nembo ya ubora.

Dk Yusuph alisema baada ye elimu hiyo, kuanzia Novemba wataanza msako mkali mitaani, katika masoko na viwandani ili kubaini bidhaa ambazo hazina nembo ya ubora ya TBS kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Tume ya mionzi yatoa tahadhari

Wakati TBS ikitoa muda huo, Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (Taec) imewataka wananchi kuwa makini na bidhaa zinazoathiriwa na mionzi.

Imewataka watumiaji wa bidhaa ambazo zinahusiana na mionzi kuchukua tahadhali ya ubora wa bidhaa hizo ili kuongeza usalama wa afya zao.

Akizungumza wakati wa kutoa elimu kwa wananchi katika banda la Taec kwenye Maonyesho ya Wakulima (Nanenane) mkoani Arusha, Ofisa uhusiano wa Tume hiyo, Peter Ngamilo alisema elimu ya udhibiti wa viasilia vya mionzi vinavyoweza kupatikana kwenye mazao ya chakula na mifugo hivyo ni muhimu kuongeza usalama wa mtumiaji dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi.

Ngamilo alisema elimu ya teknolojia ya nyuklia inaweza kuwa mkombozi kwenye ukuaji wa uchumi utokanao na viwanda ikilenga matumizi salama ya teknolojia ili kuboresha na kuongeza ustawi kwenye sekta za afya, maji, kilimo, nishati na mifugo.

Alisema Tume pia imeshafanya upembuzi yakinifu katika hatua ya awali kwa kutumia teknolojia ya nyuklia/mionzi katika kuhifadhi vyakula, mazao na kuboresha bidhaa za viwandani ili kuzipa muda mkubwa wa matumizi na kuzikinga dhidi ya uharibifu unaoweza kusababishwa na bakteria.