In Summary

Awali, juzi mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyavina alifika katika soko hilo na kuwataka wafanyabiashara kupisha ukarabati baada ya moto huo kuteketeza kabisa zaidi ya vibanda 670 na mali nyingine za wafanyabiashara hao.

Dar es Salaam. Zikiwa zimepita siku mbili tangu kuteketea kwa moto soko maarufu la Kampochea lililopo Mbagala jijini Dar es Salaam, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limetaja mkakati linaokuja nao ili kuhakikisha kuwa maisha ya wananchi na mali zao eneo hilo yako salama muda wote.

Awali, juzi mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyavina alifika katika soko hilo na kuwataka wafanyabiashara kupisha ukarabati baada ya moto huo kuteketeza kabisa zaidi ya vibanda 670 na mali nyingine za wafanyabiashara hao.

Hata hivyo, akitembelea eneo hilo, kamishna wa Divisheni ya Operesheni wa jeshi hilo, Billy Mwakatale aliwatoa hofu wananchi akisema wana mpango wa kujenga kituo cha zimamoto maeneo ya Mbagala Kizuiani ili kuweza kukabiliana na majanga ya moto katika maeneo hayo kwa urahisi.

Mwakatale alisema wamegundua kumekuwapo na changamoto mbalimbali kuwahi kuzima moto katika maeneo hayo ikiwemo umbali, ubovu wa miundombinu na upatikanaji wa maji. “Unajua gari linatokea Tazara likiwa na mzigo mkubwa wa maji, huko barabarani linakutana na mambo mengi ikiwemo mashimo katika barabara, foleni na wakati mwingine tukifika maji yanatuishia katikati,” alisema kamishna huyo.

“Tayari katika ujenzi wa kituo hicho tumewashirikisha na wenzetu wa Dawasco kutuwekea miundombinu ya maji ili tatizo la kwenda kwenye uokozi na kukatikiwa na maji liwe historia kwani hata sisi hatupendi.” Ofisa mtendaji wa Charambe, Fikiri Mtanukila alitoa wito kwa Shirika la Umeme (Tanesco), kutembelea maeneo ya masoko mara kwa mara kwa kuwa katika mikusanyiko ya watu wa maeneo hayo hakukosi wale wanaochokonoa mifumo ya umeme ambayo baadaye inasababisha majanga ya milipuko ya moto.

Mtanukila alisema pamoja na kuwepo kwa taarifa ya tatizo la umeme katika soko hilo tangu awali, bado walikuwa wazito kutokea.