In Summary

Hayo yalisemwa na mkurugenzi mkuu wa makumbusho hayo, Profesa Johannes Vogel alipokutana na katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi aliyepo nchini Ujerumani kwenye maonyesho ya kimataifa ya utalii. 

Dar es Salaam. Makumbusho ya Historia Asilia ya Berlin nchini Ujerumani yanapohifadhiwa masalia ya mijusi waliopatikana Mlima Tendaguru mkoani Lindi, imesema ipo tayari kushirikiana na Tanzania kufanya utafiti wa mabaki ya mijusi hiyo.

Hayo yalisemwa na mkurugenzi mkuu wa makumbusho hayo, Profesa Johannes Vogel alipokutana na katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi aliyepo nchini Ujerumani kwenye maonyesho ya kimataifa ya utalii.

Profesa Johannes alimueleza katibu mkuu kuwa shughuli kubwa inayofanywa na makumbusho hayo ni utafiti wa maendeleo ya sayansi, elimu na ufahamu wa dunia, viumbe na mazingira ili kumwezesha binadamu kutawala maisha yake.

“Hiki ndicho kitovu cha makumbusho hii. Tuna watafiti zaidi ya 300,” alisema Profesa Johannes.

Kwa upande wake, Milanzi alikubali kutoa ushirikiano kwa ajili ya ustawi wa sayansi na uchumi wa nchi zote mbili.