In Summary
  • Byakanwa aliamuru Omary akamatwe kutokana na kushindwa kutatua malalamiko ya wafanyakazi ambayo yanaelekezwa katika ofisi yake.

 Amri iliyotolewa juzi na mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa kwa kamanda wa polisi mkoani hapa, Lucas Mkondya kumuweka ndani ofisa kazi wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote, Nadhiru Omary imeendelea kumganda mtumishi huyo.

Byakanwa aliamuru Omary akamatwe kutokana na kushindwa kutatua malalamiko ya wafanyakazi ambayo yanaelekezwa katika ofisi yake.

Mkuu huyo wa mkoa alitoa agizo hilo baada ya kufika kiwandani hapo kutokana na baadhi ya watumishi wa kiwanda hicho chenye wafanyakazi zaidi ya 1,000 kugoma kuendelea na kazi kwa muda usiojulikana kwa madai ya kunyanyaswa, kutolipwa mishahara kwa wakati na kufukuzwa kazi bila kuzingatiwa sheria za kazi.

Machi 3 Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alitembelea kiwandani hapo akazungumza na uongozi kisha alikutana na baadhi ya wafanyakazi wakiwemo madereva waliompa malalamiko ambapo aliahidi yatafanyiwa kazi baada ya kiwanda hicho kuanza uzalishaji Machi 15.