In Summary
  • Changamoto ya kiuongozi katika makampuni hayo yaliyounda ushirika wa kibiashara pia imesababisha kushuka kwa hisa za Nissan kwa asilimia 9.

Kwa miongo miwili, Carlos Ghosn aliweza kuziinua kiuchumi kampumi mbili za magari za Renault na Nissan.

Ghosn pia alifanikiwa kufanya miujiza ya kiuchumi katika teknolojia ya magari duniani. Alifanikiwa kuyaunganisha makampuni ya Ufaransa na Japan kuwa kitu kimoja kwenye ulimwengu wa ushindani.

Sasa Carlos yupo gerezani Tokyo Japan akituhumiwa yeye na kampuni ya Nissan kudanganya mapato yake kinyume cha sheria huku hali ya kushuka kwa mapato katika soko la dunia imekuwa ikiendelea katika biashara hiyo.

Kukamatwa kwa Ghosn kumepelekea kusuasua kwa ushirika kibiashara kati ya Ufaransa na Japan ujulikanao kama Franco-Japanese.

Hii imedhihirisha namna uongozi wake ulivyokuwa makini na wenye tija kwa kampuni zote alizozisimamia ambapo tangu akamatwe mwezi Novemba, hisa za Nissan zimeshuka kwa asilimia 9.

Kutokana na ukweli kwamba Ghosn hakuandaa mrithi wake atakayeweza kusimamia vizuri utendaji wa makampuni, hali hiyo imepelekea Nissan kufanya uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili bosi wao za uuzaji wa magari zaidi ya milioni 10 mwaka 2017 bila kushirikisha kampuni mwenza ya Renault jambo ambalo limepelekea hali ya kutoelewana baina ya kampuni hizo mbili.

Christopher Richter ambaye ni kaimu msimamizi wa tafiti katika kampuni ya uwekezaji na udalali, CLSA nchini Japan, amesema, umoja huo upo kwenye wakati mgumu hivyo kunahitajika maamuzi magumu kufanyika. “Wanahitaji kiongozi”, alisema.

Bodi ya wakurugenzi wa Nissan inakutana leo Jumatatu kuteua atakayechukua nafasi ya Ghosn ambaye tayari ameondolewa kwenye nafasi ya mwenyekiti wa bodi hiyo.

Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika, makampuni ya Nissan na Renault yapo kwenye mjadala wa kutengana ili kila moja iendelee na shughuli zake kwa kujitegemea.