In Summary
  • Akizungumza katika mkutano wa wadhibiti ubora wa shule kutoka wilaya za mikoa ya Manyara na Arusha uliofanyika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) jana, Nasha alisema Serikali imetenga Sh1 trilioni za maendeleo kwenye wizara hiyo katika bajeti ya mwaka huu.

Arusha. Naibu Waziri wa Elimu, William ole Nasha amesema Serikali imewekeza fedha nyingi kwa ajili ya kuinua kiwango cha elimu nchini, hivyo haitakubali kuwavumilia wadhibiti ubora wa shule nchini wasiotimiza wajibu wao.

Akizungumza katika mkutano wa wadhibiti ubora wa shule kutoka wilaya za mikoa ya Manyara na Arusha uliofanyika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) jana, Nasha alisema Serikali imetenga Sh1 trilioni za maendeleo kwenye wizara hiyo katika bajeti ya mwaka huu.

Nasha alisema Serikali imeamua kubadili utaratibu wa ukaguzi wa shule kwa kuondokana na ule wa zamani ambao ulionekana wa kuvizia kwa lengo la kupata makosa na kwamba mfumo mpya unalenga ushirikishwaji ili kuleta mabadiliko.

Mdhibiti wa ubora wa shule nchini, Augusta Lupokela alisema mfumo mpya unalenga kuboresha kiwango cha elimu katika ufundishaji na usimamizi.

Alisema ili kufikia malengo waliyojiwekea kila mdau ana nafasi yake katika kutekeleza mikakati hiyo, hivyo kuwataka kila anayehusika kutimiza wajibu wake.

Kaimu mkuu wa ATC, Dk Masudi Senzia alisema udhibiti ubora wa elimu utasaidia kuwaimarisha wanafunzi wakiwa ngazi za awali.