In Summary
  • Meneja Kiongozi wa NSSF Mkoa wa Temeke, James Oigo alisema hayo hivi karibuni katika semina ya kutoa elimu kwa waajiri wa Wilaya ya Ilala iliyohusu mabadiliko ya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Dar es Salaam. Wakati taasisi na kampuni mbalimbali zikiwa zinashindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi katika Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa muda muafaka, shirika hilo linatarajia kuanza kupita kwenye ofisi hizo ili kuwasikiliza waajiri na kuwaelekeza namna ya kulipa malimbikizo hayo ya watumishi wao.

Meneja Kiongozi wa NSSF Mkoa wa Temeke, James Oigo alisema hayo hivi karibuni katika semina ya kutoa elimu kwa waajiri wa Wilaya ya Ilala iliyohusu mabadiliko ya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

“Wiki ijayo tutapita kwa waajiri na kuwasikiliza ili kujua wanalipaje malimbikizo ya michango ya wanachama, labda kuna changamoto zinazowakwamisha, lakini tutawapa fursa ya kueleza kwamba watakuwa na uwezo wa kuwasilisha kiasi gani kila mwezi,” alisema.

Oigo alifafanua kuwa, awali walitangaza majina ya wadaiwa sugu kwenye magazeti hatua ambayo ni ya mwisho katika kuwashinikiza waajiri kuwasilisha malimbikizo na kwamba baadhi wamelipa na wengine bado.

Akizungumzia waajiri ambao hawajapeleka michango NSSF licha ya kutangazwa, alisema watawafikisha mahakamani ingawa kuna changamoto kwani waajiri ni watu wanaowahudumia kila siku.

“Hatupendi tufike mahakamani kwa sababu hii ni hatua ya mwisho na ina changamoto nyingi, mojawapo ni kuleta uhusiano mbaya kati yetu na waajiri,” alisema.

Pia, aliwataka wanachama wao kufuatilia mienendo ya uwasilishwaji wa michango yao kila mwaka ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza baada ya kufikisha umri wa kustaafu.

Meneja wa NSSF Ilala, Christina Kamuzora alisema lengo ni kuwaelimisha waajiri kuhusu sheria hiyo iliyoanza kufanya kazi Aprili Mosi mwaka huu.

Alisema sheria hiyo imefanya idadi ya mifuko ya hifadhi ya jamii kuwa miwili ukiwamo wa PSSF unaowahudumia watumishi wa umma na NSSF ambao ni kwa ajili ya wafanyakazi kutoka sekta binafsi.