In Summary

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa ubadilishaji fedha za kigeni hasa katika maeneo ya mipakani ambako biashara nyingi zinafanyika

Dar es Salaam. Benki ya NMB imetanua wigo wa kubadilisha fedha katika matawi yake mbalimbali nchini.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa ubadilishaji fedha za kigeni hasa katika maeneo ya mipakani ambako biashara nyingi zinafanyika.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Julai 26, 2018 ofisa wa benki hiyo wa idara ya hazina na masoko ya fedha za kimataifa, Jeremiah Lyimo amesema maeneo ya mipakani yanatumiwa zaidi kibiashara na watu kutoka mataifa mbalimbali.

“Kutokana na hilo tumeamua kuongeza idadi ya sarafu ambazo mtu anaweza kubadilisha akiwa na fedha taslimu,” amesema Lyimo.

Amesema sarafu zilizoongezwa ni zile za nchi ya Kenya, Rwanda na Uganda kwa sababu nchi hizo zimekuwa zikifanya zaidi biashara na Tanzania.

“Ilikuwa ngumu watu kubadilisha fedha za jumuiya ya Afrika  Mashariki katika benki na maduka mengi lakini kuanzia sasa huduma hiyo inapatikana katika matawi yote ya NMB,” amesema.

Amesema mbali na ubadilishaji fedha pia wateja wataweza kutuma pesa katika nchi yoyote duniani kwa gharama nafuu na kupokea pesa bila makato.