In Summary
  • Ghosn alikamatwa akishukiwa kutoa taarifa za uongo chini ya mapato yake halisi kwa takriban dola milioni 44. Mkurugenzi mwingine wa Nissan, Greg Kelly pia alikamatwa.
  • Rais wa Nissan, Hiroto Saikawa aliwaambia waandishi wa habari kuwa anaamini mamlaka makubwa yaliyokabidhiwa kwa mtu mmoja ni moja wa sababu iliyopelekea ufujaji huo.

Tokyo, Japan. Waendesha mashtaka jijini Tokyo Jumatatu walimkamata mwenyekiti wa kampuni ya kutengeneza magari ya Nissan Motor, Carlos Ghosn akishukiwa kutoa taarifa ambazo ziko chini ya mapato yake halisi.
Kwa muda mrefu Carlos Ghosn ameonyesha uongozi madhubuti akiwa kiongozi mkuu wa Nissan Motor, hivyo ni wazi kuwa kukamatwa kwake kutailazimisha kampuni hiyo kupitia upya mkakati wake wa kibiashara.
Ghosn alikamatwa akishukiwa kutoa taarifa za uongo chini ya mapato yake halisi kwa takriban dola milioni 44. Mkurugenzi mwingine wa Nissan, Greg Kelly pia alikamatwa.
Rais wa Nissan, Hiroto Saikawa aliwaambia waandishi wa habari kuwa anaamini mamlaka makubwa yaliyokabidhiwa kwa mtu mmoja ni moja wa sababu iliyopelekea ufujaji huo.
Ghosn alihamia Nissan akitokea kampuni mshirika ya utengenezaji magari ya Ufaransa ya Renault mwaka 1999 kwa lengo la kuikomboa kampuni hiyo iliyokuwa imekumbwa na matatizo ya kifedha akitumia njia ya kupunguza matumizi.
Aliendeleza ushirikiano kati ya kampuni za Nissan, Mitsubishi Motors na Renault ambayo serikali ya Ufaransa inamiliki hisa nyingi.
Kampuni ya Nissan imepanga kuanzisha jopo huru la wataalamu na wengineo haraka iwezekanavyo ili kuchunguza suala hilo.