In Summary

Tayari Serikali imetangaza zabuni ya ujenzi wa awamu hiyo ambapo waliovutiwa na zabuni hiyo wanatakiwa kuwa na dhamana zenye thamani isiyopungua Sh480 milioni na kuwasilisha maombi yao kipindi kisichozidi Aprili 10.

Dar es Salaam. Wakati abiria 200,000 wanahudumiwa na Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) jijini Dar es Salaam kila siku kwa sasa, awamu ya pili ya mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mabasi hayo inayohusisha barabara ya kwenda Mbagala imeanza kupikwa.

Tayari Serikali imetangaza zabuni ya ujenzi wa awamu hiyo ambapo waliovutiwa na zabuni hiyo wanatakiwa kuwa na dhamana zenye thamani isiyopungua Sh480 milioni na kuwasilisha maombi yao kipindi kisichozidi Aprili 10.

Kwa mujibu wa tangazo la zabuni hiyo lililotolewa baada ya Serikali kupata mkopo kutoka Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), mradi utahusisha ujenzi wa jengo la biashara (Mbagala Complex) litakalokuwa na karakana, maduka, ofisi za utawala, maliwato na kituo cha abiria.

Vilevile, kutakuwa na vituo vinane vya abiria, kituo cha mafuta, kituo cha polisi, vibanda vya ulinzi, uzio na maegesho ya magari.

Ndani ya siku 730 za utekelezaji wa mradi huo zikiwamo 56 za maandalizi, pia kutakuwa na ujenzi wa vituo vya Kariakoo, Mbagala Zakhem, Mtoni Kijichi, Mtoni na Chang’ombe.

Licha ya kutangazwa na AfDB, maombi yote ya mradi huo yanatakiwa kupelekwa makao makuu ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ndani ya muda uliotolewa.

Mkurugenzi mtendaji wa Tanroads, Patrick Mfugale alisema wanasubiri kupokea maombi hayo kabla hawajatekeleza majukumu yao ya kumtafuta atakayeshinda na kumpa jukumu la kuutekeleza.

Ingawa zabuni hiyo ni ya kimataifa, waombaji ambao wanaweza kupata taarifa za ziada na kukagua nakala husika kutoka ofisi ya katibu mkuu wa ujenzi wanapaswa kutoka kwenye nchi wanachama wa AfDB pekee.

Kuanzia siku ya mwisho ya kupokea maombi ya zabuni hiyo, tangazo linasema mapitio yatafanywa kwa siku 120 kabla ya kutangazwa kwa mshindi.

Kabla ya kuwekwa kwenye tovuti ya benki hiyo, Oktoba 21, 2015 tangazo la zabuni hiyo lilitolewa katika tovuti ya Biashara ya Umoja wa Mataifa (UNDB).

Januari 2017, Rais John Magufuli alizindua awamu ya kwanza ya mradi huo iliyokuwa na urefu wa kilomita 20.9 kutoka Kimara mpaka Kivukoni.

Licha ya kuhudumia vituo vilivyopo kwenye Barabara ya Morogoro kuna njia za Morocco na Kariakoo. Baada ya kuanza kufanyakazi, njia nyingine inayofika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) iliongezwa.

Licha ya Tanzania, mradi kama huo upo kwenye mataifa mengine matatu ikiwamo Afrika Kusini na Misri.