In Summary
  • Zabuni hiyo iliyotangazwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) Aprili 12 ilifungwa juzi ili kuanza upembuzi wa kumpata mshauri elekezi aliyekidhi vigezo.

Dar es Salaam. Kampuni 64 zimeomba zabuni ya kuishauri Serikali namna inavyotakiwa kutekeleza mradi wa gesi asili iliyosindikwa (LNG) Mkoa wa Lindi.

Zabuni hiyo iliyotangazwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) Aprili 12 ilifungwa juzi ili kuanza upembuzi wa kumpata mshauri elekezi aliyekidhi vigezo.

Licha ya tangazo la TPDC, zabuni hiyo pia ilichapishwa kwenye Jarida la Maendeleo ya Biashara la Umoja wa Mataifa (UNDB online) na tovuti wa wadhamini wa ambao ni Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB).

Akizungumza na Mwananchi jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Kapuulya Musomba alisema zipo kampuni za Kitanzania zilizoonyesha nia ya kuitaka zabuni hiyo hivyo zitapimwa kulingana na sheria ya ununuzi na uwezo binafsi.

“Zabuni hii ni ya kimataifa. Baada ya kupokea maombi kutoka kampuni 64 sheria inaelekeza hatua inayofuata. Sina uhakika kama wataalamu wa ndani wana uwezo nayo lakini wanaruhusiwa kuingia ubia na kampuni za nje ili kuwa na uwezo mkubwa zaidi,” alisema Musomba.

Ingawa mradi huo unafadhiliwa na AfDB, kipaumbele kitatolewa kwa wazawa waliothubutu kuomba kuutekeleza kama wana vigezo.

Tangazo la zabuni hiyo lililowekwa katika tovuti ya TPDC linaonyesha majukumu ya mshauri huyo yatakuwa matatu ambayo ni kutengeneza mpangokazi wa kitaalamu, kisheria na kibiashara kuhusu mradi huo.