In Summary
  • Wajumbe wasema hatua hiyo itasaidia kujiimarisha kiuchumi

Moshi. Licha ya takriban miaka 10 kupita kwenye hali ngumu ya madeni, Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU) kimeruhusiwa kukopa mpaka Dola 1 milioni za Marekani kwa ajili ya ununuzi wa kahawa msimu huu ili kukisaidia kujiimarisha.

KNCU kililazimika kuuza shamba lake la Garagarua mwaka jana lenye ukubwa wa heka 3,429 kwa Sh9.3 bilioni ili kulipa madeni.

Kati ya fedha hizo, Sh5.2 bilioni zililipwa Benki ya CRDB kama deni na riba ya mkopo, huku mwekezaji aliyekuwa amewekeza katika shamba hilo akilipwa Sh3 bilioni kama fidia.

Katika azimio lililopitishwa katika mkutano mkuu wa 34 wa KNCU, meneja wa chama hicho, Honest Temba alisema wataanza ununuzi wa kahawa mnadani muda mwafaka.

Katika msimu huu wa mwaka 2018/19, Serikali imetangaza kuanza kutumika kwa mfumo wa stakabadhi ghalani katika ununuzi wa kahawa hatua ambayo Temba alisema itaondoa madeni ya vyama vya msingi.

Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani Kilimanjaro, John Henjewele alivitaka vyama vya msingi kusimamia ubora wa kahawa kuhakikisha inaandaliwa kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa ili kupata bei nzuri sokoni.

“Tunakwenda kwenye biashara ya kimataifa, naomba vyama vya msingi vizingatie ubora kwani tunatambua ili kahawa iweze kupata bei nzuri lazima iwe na ubora wa hali ya juu,” alisema.

Naye mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Mwika Kusini Mashariki, Fanuel Silayo alisema uamuzi wa mkutano mkuu wa kukopa fedha benki kununua kahawa utaongeza faida kwa KNCU na kubadilisha muonekano wa chama.

jinamizi la madeni

Katika matumizi ya fedha za shamba la Garagarua, Sh133.5 milioni zilitumika kulipa kodi; ufuatiliaji na gharama za kitaalamu Sh236 milioni, ushuru wa stempu Sh93 milioni; na kodi ya ardhi Sh16 milioni.

Mwaka huu, chama hicho kilikuwa na mpango wa kuuza shamba lingine la Lerongo lenye ukubwa wa heka 581 ili kunusuru benki yake ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL) isifungwe.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT), iliipa benki hiyo miezi sita kuongeza mtaji wake kutoka Sh1.5 bilioni wa sasa hadi Sh5 bilioni, vinginevyo ingeifunga kama ilivyofanya kwa baadhi ya benki nchini.

Hata hivyo, akihutubia mkutano wa hadhara huko Serengeti mkoani Mara Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alizuia uuzwaji wa shamba hilo hadi Serikali itakapomaliza kuhakiki mali za vyama vya ushirika nchini.