In Summary
  • Kampuni ya Emirates imekuwa kiungo muhimu katika biashara ya nyama kati ya Tanzania na Falme za Kiarabu

Dar es Salaam. Wakati baadhi ya kampuni zikisitisha safari zake nchini, Kampuni ya ndege ya  Emirates Tanzania imesema inaendelea kufanya vizuri kibiashara na kiuwekezaji kwa  kutoa huduma inayoendana na mahitaji ya wateja wake.

 Pia imejisifu  kufanya vizuri katika usafirishaji mizigo.

Akizungumza na wanahabari leo Septemba 11, Meneja wa Kampuni hiyo nchini,  Rashed Alfajeer amesema kampuni hiyo imeendelea kufanya vizuri na inajizatiti kuendelea kuwaunganisha Watanzania hasa wafanyabiashara katika  nchi zote 85 inapofika.

“Kadri yanavyotokea mabadiliko ya kimaendeleo na mahitaji, ndivyo umuhimu wa kuboresha huduma na uwekezaji unavyoongeka,” amesema Alfajeer.

Amesema Tanzania ni moja kati ya nchi muhimu katika biashara yao ndiyo maana ipo ndege inayofanya safari kila siku.

 “Ndege yetu aina ya Boeing 777 inabeba zaidi ya tani 100 za mizigo. Kwa mwaka jana pekee tumesafirisha tani milioni 2.3  kutoka Tanzania kwenda nchi za Falme za Kiarabu na Asia,” amefafanua.

Kuhusu kusafirisha mizigo kuingiza nchini anasema kwa mwaka jana pekee walisafirisha tani 4.5 milioni kutoka nchi za Falme za Kiarabu, India na Hong Kong.

Amefafanua kuwa Emirates imekuwa kiungo muhimu kwa wafanyabiashara wa nyama nchini kwani kiasi kikubwa cha mizigo waliyosafirisha mwaka uliopita ni nyama ya mbuzi na kondoo.

“Uhitaji wa nyama ya mbuzi na kondoo katika nchi za Falme na Kiarabu umewaunganisha wafanyabiashara wa Watanzania na wateja wao waliopo katika mataifa hayo,” amefafanua.