In Summary
  • Tayari benki hiyo imeshawekeza zaidi ya Sh4.4 trilioni kwenye sekta ya nishati, maji, kilimo na barabara kwa lengo la kuchochea uchumi wa Tanzania ili ufikie lengo la kuwa nchi ya uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo 2025.

Dar es Salaam.Tanzania ni miongoni mwa nchi zinapatiwa fedha nyingi kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika kutekeleza miradi ya maendeleo.

Tayari benki hiyo imeshawekeza zaidi ya Sh4.4 trilioni kwenye sekta ya nishati, maji, kilimo na barabara kwa lengo la kuchochea uchumi wa Tanzania ili ufikie lengo la kuwa nchi ya uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo 2025.

Haya yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alipokutana na kufanya mazungumzo na  Mkurugenzi wa benki hiyo anayeiwakilisha Marekani, Steven Dowd Jijini Dar es Salaam leo.

Dk Mpango amesema Tanzania inapata fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maendeleo kutoka AfDB kutokana na vipaumbele vya Benki hiyo kuendana na vya Serikali ya Tanzania.

“Miradi inayotekelezwa kwa fedha za AfDB ni pamoja na wa kusafirisha umeme kutoka Mbeya, Sumbawanga hadi Nyakanazi utakao gharimu Dola za Marekani milioni 123, mingine ni ile ya ushirikiano na Sekta Binafsi (Dola 57.6 milioni), ujenzi wa barabara ya Nyakanazi hadi Burundi kupitia Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma na mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Msalato Jijini Dodoma ambao AfDB imeahidi kutoa Sh200 bilioni  kwa kuanzia,” amesema Dk Mpango.

Naye Mkurugenzi wa  AfDB anayeiwakilisha Marekani, Dowd amesema Tanzania imeonyesha dhamira ya dhati ya kufikia malengo iliyotarajia.

“Kwa msingi huo, bodi ya AfDB itaangalia namna ya kuendelea kuisaidia Tanzania katika miradi mikubwa ya nishati ya umeme na ujenzi wa reli ya kisasa,” amesema.

Pia, ameahidi kuwashawishi wawekezaji kutoka Marekani kuja kuwekeza Tanzania kwa kuwa kuna mazingira mazuri ya uwekezaji na kuishauri Serikali kuweka mazingira mazuri zaidi ya kimikataba kati yake na wawekezaji ili waweze kuwa na uhakika wa usalama wa uwekezaji wao.

Ameahidi pia kutumia ushawishi wake katika masuala ya biashara na uwekezaji ili wafanyabiashara wengi kutoka Marekani waweze kuwekeza mitaji na teknolojia hapa nchini.

Amesema Rais wa Marekani, Donald Trump ni mtu wa vitendo kuliko maneno na ameihakikishia Tanzania kwamba itapata ushirikiano mkubwa kutoka Marekani.

Akizungumzia maombi ya Serikali ya kutaka benki yake isaidie ujenzi wa miradi mikubwa ya maendeleo ikiwamo ya ujenzi wa reli ya SGR, ya kufua umeme kutoka Mto Rufiji na miundombinu mbalimbali, Dowd amesema wataijadili ili kuangalia namna ya kuifadhili.

Mkurugenzi wa AfDB Kanda ya Afrika, Dk Nyamajeje Weggoro, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki yenye hisa nyingi katika benki hiyo.

“Tanzania  inahisa takribani asilimia moja kati ya tano zinazomilikiwa na nchi nane za Uganda, Rwanda, Ethiopia, Kenya na Sudani Kusini na pia, inatekeleza miradi mbalimbali inayofadhiliwa na AFD,” alisema.